KWA kutumia mabango, lengo likiwa kutangaza kazi zao, waganga wengi wa tiba asilia wamekuwa wakijinadi kuwa wanatoa tiba ya kurefusha maumbile ya siri ya wanaume, kukuza makalio au matiti.
Katika mitaa ya miji na majiji nchini, siyo jambo la ajabu kukutana na mabango hayo, ambayo hata hivyo kushamiri kwake kunaleta picha kwamba ni kutokana na uhitaji mkubwa wa huduma hiyo nchini, huku watoa huduma husika wakinufaika kwa kujikusanyia kiasi kikubwa cha fedha kutoka kwa wahitaji.
Pia dawa zinazodaiwa kukuza makalio maarufu kama ‘mchina’, zimekuwa gumzo baada ya kuingia nchini, huku zikielezwa kukosa ubora na kwamba zina madhara makubwa.
Lakini, sasa unaweza kuachana na dawa hizo za Kichina, baada ya kugundulika mmea wenye uwezo wa kukuza makalio, matiti, pamoja na kurefusha uume.
Taarifa za kiutafiti zinautaja mti huo kwa jina la Mvunge, ukiwa na uwezo wa kukuza makalio, matiti na kurefusha uume.
Kaimu Msajili wa Tiba Asili na Tiba Mbadala nchini, Dk Naomi Mpemba anasema kuwa mmea huo ambao huwa ni mti mkubwa upo na kwamba una uwezo mkubwa wa kukuza maumbile hayo.
Anabainisha kuwa mmea huo ambao hukua na kuwa mti mkubwa huzaa matunda yanayotumika kama dawa na unapatikana wilayani Korogwe Mkoa wa Tanga, Pwani, Mbeya, Morogoro na baadhi ya mikoa nchini.
“Tulifuatilia na kutambua kuwa mti huo upo maeneo hayo na unatumiwa zaidi na waganga, hata picha za mti huo tunazo,” anasema Dk Mpemba na kuongeza:
“Jina jingine unaitwa Miegeya, mara nyingi unastawi katika maeneo yenye ardhi ya unyevunyevu, una tabia ya kustawi kama Mwembe na matunda yake huonekana kufanana na Mbuyu.”
Hata hivyo, anasema kuwa asilimia kubwa ya waganga wa tiba asili na tiba mbadala wanaotumia dawa hiyo ni wale wasiokuwa na usajili kutoka baraza hilo, hivyo kufanya huduma hizo kinyume cha utaratibu.
“Kwa mujibu wa masharti yaliyopo katika agizo la Serikali kwa waganga hao, miiko, maadili na utendaji wa kazi zao umeelekeza kuwepo na usiri na kuaminiwa, kwa hiyo sisi tunaamini wanaojitangaza kutibu mambo hayo ni matapeli,”anasema Dk Mpemba.
Wasiwasi
Huku akionyesha wasiwasi wa kutoa picha za mti huo, Dk Mpemba alisema kwamba endapo utaonekana wazi kupitia vyombo vya habari, jamii inaweza kuathirika kwa sehemu kubwa kuutafuta.
Dk Mpemba alitahadharisha kuwa matumizi ya mmea huo siyo mazuri kwa vijana, badala yake akasisitiza matumizi ya lishe bora kupitia vyakula vinavyojenga mwili.
“Suluhisho ni lishe na siyo kuhangaika na dawa za ajabu, tatizo lenu vijana vyakula ni chipsi, mayai, nguvu zikiwaishia matokeo yake ndiyo mnaanza kutafuta dawa za kurefusha sehemu za siri, haitawasaidia, dawa ni lishe tu,”alisisitiza Dk Mpemba.
Mkuu wa Kitengo cha Utafiti wa Tiba za Asili wa Taasisi ya Utafiti wa Tiba nchini NIMR, Dk Hamis Malebo, alisema Nimr inaufahamu mmea huo, ingawa haijaufanyia utafiti wa kuthibitisha uwezo wake huo.
Alisema mmea huo kisayansi unaitwa Kigelia Africana na unapatikana katika maeneo mengi ya Afrika.
“Masuala ya tiba asilia yanaweza wakati mwingine kuwa na utata na sisi hatuwezi kusema sana kwa sababu hatujafanya utafiti,” alisema Dk Malebo.
Alisema Nimr haiwezi kuzungumza kwa undani kwa sababu bado haijawathibitisha watu waliowahi kupata tiba ya mmea huo, wala haijahakiki chochote kuhusu matunda au mizizi ya mti huo kufanya kazi.
CHAMA
Mkurugenzi wa Kampuni ya Boresa na Mratibu wa Chama cha uratibu wa dawa za tiba asili Tanzania, Boniventura Mwalongo anasema:
“Serikali ifanye majadiliano na kuchunguza, kisha ieleze sasa kama mwanaume kuwa sehemu fupi za siri ni tatizo, au mwanamke kuwa na makalio madogo ni tatizo kwa sababu ya mazingira yalivyo kwa sasa kwenye jamii.”
Mwalongo alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kusema kuwa uchunguzi unahitajika, ili kutofautisha ugonjwa na maumbile ambayo mtu alizaliwa nayo, ili kutoa msaada wa huduma hiyo kama walivyo wagonjwa wengine.
“Kwa sasa kinachofanyika ni utapeli tu, kwa sababu huwezi kujua kama ni ugonjwa au ni maumbile. Kwa nini mtu aongezewe ukubwa wa maumbile yake wakati alizaliwa hivyo?” alisema akihoji na kuongeza:
“Endapo itabainika kweli kuna ugonjwa, watu wanapungua ukubwa wa sehemu zao za siri, basi kunahitajika huduma hiyo.”
Mwalongo alisema kuwa mbali na kuwepo kwa dalili za uhitaji wa huduma hiyo nchini, haoni kama kuna ulazima wa Serikali kushughulikia suala hilo, badala yake akataka iwekeze katika matibabu ya huduma nyingine.
“Kuna magonjwa mengi sana ya zamani na yaliyoendelea kuibuka kwa sasa, kuna magonjwa yanayosababishwa na unywaji na ulaji mbovu, dhambi na ukosefu wa mazoezi, ili kuepusha gharama ya magonjwa haya Serikali inatakiwa kuwekeza elimu kwa jamii,”alisema Mwilongo.
Kauli ya Serikali
Mbali na kukithiri kwa matibabu ya dawa hizo, Serikali imeendelea kutoa onyo kali kwa waganga wote wanaotoa huduma bila kusajiliwa kama ilivyoagizwa.
Matumizi mengine ya Mvunge
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili unaonyesha kuwa mti huo umekuwa ukitumika kwa miaka mingi, ambapo baadhi ya wazazi ama vijana binafsi huamua kwenda kwa wataalamu wa tiba za asili na kupatiwa huduma hiyo baada ya kubainika kuwa maumbile yao kuwa madogo isivyo kawaida.
Mti huo pia unaelezwa kutumika kuponya wazee ambao viungo vyao vimepoteza uhalisia wake pamoja na kutibu ugonjwa wa kuziba njia ya haja ndogo, ukipata umaarufu katika maeneo ya Wilaya za Handeni, Kilindi na Bagamoyo mkoani Pwani,ambapo hupatikana zaidi maeneo ya mabondeni.
Mizizi, matunda, mbegu za matunda, magamba ya mti na majani vyote hutumika kama dawa na chakula.
Matunda yaliyoiva na mabichi ya mti huo ni sumu kwa binadamu, lakini baadhi ya watu hukausha matunda hayo na kuyachanganya katika pombe za kienyeji ili kuongeza ladha.
Karibu kila sehemu ya mti huu hutumika kama dawa ya asili, kwa mfano kulainisha chakula, kutibu kushindwa kupumua, kutibu majeraha na maradhi ya ngozi.
Utafiti wa mti huo katika kutibu bakteria, fungasi na uvimbe unaendelea kufanyika katika nchi za Korea, Japan na India.
Ushuhuda
Mmoja wa watu wanaotoa tiba hiyo ya asili wilayani Handeni Mkoa wa Tanga, akifahamika kwa jina la Dk Ramadhani Chenyewe, anasema kuwa ametibu watu wengi wakiwamo vijana na wazee kutoka ndani na nje ya wilaya hiyo, waliohitaji kuimarishwa nyeti zao.
Chenyewe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Waganga wa Jadi (MACO) wilayani Handeni, anafafanua kwamba, kwa kutumia dawa hiyo msimu wa mvua nyingi, nyeti hukua kwa haraka katika muda usiozidi mwezi mmoja, kutokana na tunda la mti huo kukua haraka.
“Hilo jambo ni la kweli wengi ninaowatibu wana tatizo uume ni mdogo, na wengine nao ni wazee ambao wanaona mabadiliko katika sehemu hizo kwa kuwa ndogo, tofauti na awali. Basi wakija huwa ninangalia kwanza kama kweli ni ndogo, baada ya kuthibitisha ndipo ninamuongezea,” anasema Dk Chenyewe.
Aliongeza: “Nimewasaidia wengi, tiba yenyewe ni kwamba unakwenda kwenye mti kabla ya kufanya chochote, unaufanyia kitu kama tambiko, baada ya hapo ndipo shughuli ya tiba zinaanza kwa kutumia pia matunda ya mti huo ambayo yanakua kwa urefu.”
Hata hivyo, anaonya kuwa kazi hiyo inahitaji uangalizi mkubwa kwa vile inaweza kuwa kubwa kupita kiasi, hali inayoweza kusababisha madhara kwa mwenza.
Amewataka wanajamii kuacha kwenda kwa waganga kukuza nyeti zao kwa nia ya tamaa ya kutaka kuwakomoa wenzi wao, akisema hilo siyo kusudio la kuanzishwa kwa tiba hiyo ya aina yake.
Mmoja wa watu waliopatiwa tiba hiyo ya kukuza nyeti, ambaye ni mkazi wa mjini Handeni, aliyeomba jina lake lisitajwe, anasema kwamba alikwenda kwa waganga hao kutokana na kuona kiungo chake hakilingani na vya wenzake.
“Mimi wakati tunacheza na wenzangu hasa kwenda kuogelea, nilikuwa nashangaa mbona ya kwangu ni ndogo sana ukilinganisha na wenzangu. Nikamweleza babu yangu, ambaye naye aliniangalia kisha akanishauri twende kwa mganga ambaye anakuza kwa kutumia yale Mavungwe,” anasema kijana huyo mwenye umri wa miaka 27.
Kijana huyo anadai kwamba alitibiwa na kufikia malengo yake kwa muda wa mwezi mmoja, tangu kufanyiwa tiba katika mti huo maarufu sana kwa waganga wa jadi mkoani Tanga.
Chanzo: Mwananchi
0 maoni:
Post a Comment