Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

JULIANA SHONZA ALIYEFUKUZWA BAVICHA AJITETEA KWA KUFURUMUSHA MATUSI NA KASHFA VIONGOZI WAANDAMIZI WA CHADEMA

Mchange na wenzie
Aliyekuwa Makamu Mwenyekiti BAVICHA kabla ya kufukuzwa kwenye umoja huo mapema mwezi huu, Bi Juliana Shonza (pichani) ameandika waraka mrefu akifafanua kile alichokiita ni tamko lake kutoa ufafanuzi dhidi ya taarifa batili zilizoelezea kufukuzwa kwake ambako kumepelekea pia kupoteza sifa za uanachama wa CHADEMA kwa mujibu wa taarifa ya awali ya Mwenyekiti wa baraza hilo Ndg John Heche. Ifuatayo ni tamko hilo la Juliana ambalo limesheheni tuhuma mbali mbali, kashfa na maneno mengine yasiyofaa kuzungumzwa na mtu anaedai bado ni kiongozi halali. Chukua muda usome hii hapa chini….
*****************************************************************************************
TAMKO LA KUTOA UFAFANUZI DHIDI YA TAARIFA BATILI ZILIZOZALISHWA NA
MWENYEKITI WA BAVICHA BWANA: JOHN HECHE [WEGESA CHARLES SUGUTA] KUHUSU KUVULIWA UANACHAMA WA BAVICHA, NA KUSHABIKIWA NA MH. FREEMAN MBOWE, MWENYEKITI CHADEMA TAIFA
Nawashukuru sana wanahabari, kwa kuchukua muda wenu kuja kunisikiliza. Natambua mnakiu ya kusikiliza mambo mengi ya kuwaeleza kutokana na taarifa zilizosambaa kuhusu hiki kichefuchefu kinachosambazwa kwa makusudi na virusi vichache vilivyojivika ngozi ya ukombozi.
Nimepokea simu nyingi kutoka kwa watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania wakitaka kupata ufafanuzi baada ya kupata taarifa kupitia vyombo vya habari kuwa nimevuliwa uanachama na U-Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa.
Kama mlivyo ninyi, nami pia nimeyasikia hayo kupitia vyombo vya habari, maana sijapata barua au mawasiliano yoyote toka kwa Mwenyekiti wa BAVICHA, Ndugu Wegesa Suguta (John Heche) aliyetoa tamko hilo.
Kwanza kabisa naomba kuweka wazi kwamba sijawahi pewa shutuma zozote au mashitaka yoyote yale yanayohusiana na hicho alichokiongea.
Niliamua kupuuzia kwa sababu namjua Heche ni mlopokaji, kiongozi asiyejua wajibu wake, anayetumikia wasiomchagua, mtu asiye na malengo na mtegemezi wa siasa ili kuendesha maisha yake na ya familia yake.
Pia nilimpuuza kwa sababu najua sio Mwenyekiti aliyechaguliwa kidemokrasia, aliwekwa kwa matakwa ya wakubwa zake ambao wanamtumia kwa malengo yaliyokusudiwa, ikumbukwe kuwa vijana watatu, Habibu Mchange, Mtela Mwampambwa na Grayson Nyakarungu walienguliwa kimizengwe ili Heche ashinde, hivyo kwetu sisi yeye ni sawa na Mwenyekiti wa kuteuliwa. Hivyo sikumjibu mtu asiyekuwa na sifa sawa na zangu katika harakati za kusaka demokrasia ya kweli.
Lakini kitendo cha Mwenyekiti wangu, Mh. Freeman Mbowe kujitokeza kupitia gazeti mojawapo na kudai madai yangu ni ya kitoto, kwanza kimenifedhehesha, ni dharau kwa vijana walioniona nina sifa na ukomavu na kunipa kura nyingi ili niwe Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa.
Pili ni kama anahalalisha kikao batili, kilichokiuka kanuni na katiba ya CHADEMA ili kuhalalisha matakwa yao yenye lengo la kuminya demokrasia na uhuru wa kujieleza ndani ya chama.
Tatu anahalalisha hoja za vijana, ambazo ndio uhalisia kuwa Heche hakuwa na sifa, na uwezo, hivyo alibebwa na Mh. Mbowe ili akae pale kwa malengo yake.
Ndio maana nilisema ukiona kifaranga kimepanda juu ya figa ujue mama yake yuko chini, hivyo mama yake kifaranga kajitokeza kuhalalisha kifaranga chake kupanda juu ya figa.
MADAI YA ALIYODAI MH. MBOWE KUWA NI YA KITOTO
Niseme wazi kwamba nimesikitishwa mno na madai aliyoyatoa Mwenyekiti wangu wa CHADEMA Mh Freeman Mbowe kupitia gazeti la Mtanzamia la tarehe 12/01/2013 kwamba madai yangu ni ya kitoto .
Kwanza niweke wazi kabisa kwamba namuheshimu sana Kiongozi wangu huyu mkuu ambaye ndiye alipaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba haligawi baraza la Vijana na chama kwa ujumla, ahakikishe kuna utawala bora ndani ya chama, na utendaji haki, lakini cha kushangaza ameibuka kumtetea Heche kwa hoja za mwegemeo wa upande mmoja bila kuangalia maelezo ya upande wa pili.
Niweke wazi kabisa kwamba kauli aliyoitoa dhidi yangu ni yakiushabiki maana kama ni madai yangu kuhusu namna ninavyohujumiwa kupitia kwa Katibu Mkuu yeye anayo nakala ya malalamiko [ushahidi upo], lakini hakuna hatua ambayo ameichukua.
Namshangaa Mwenyekiti kudai madai yangu ni ya kitoto sasa sijui ni madai yapi anayazungumzia ? madai ya kitoto ni yapi? na madai ya kikubwa ni yapi ? na je madai ya kitoto ni haya mimi kuhoji kwanini hatuweki akiba kwenye akaunti kwa ajili ya uchaguzi 2015 kama tulivyokubaliana kwenye baraza kuu mara baada ya uchaguzi wa 2010.
Naomba niwajulishe wanachadema kuwa, nimejitahidi sana kushauri juu ya
1; Uanzishwaji wa chuo cha mafunzo ya uongozi kwa makada wa CHADEMA , badala yake ni matumizi mabaya ya fedha za ufadhili wa wadau tofauti na hasa mfadhili mkuu ndugu SABODO. Hii ingesaidia pia kulea ki-mfumo wa maadili ya uongozi kwa vijana wa umoja wa wanafunzi wa CHADEMA wa vyuo vikuu yani “ CHASO” ambapo mimi ni mwasisi wa mkakati huu nchini.
2; Chama kwa ujumla kutokuwa na jengo letu na hasa makao makuu yetu. Ni aibu kwa chama kikubwa kama CHADEMA kuwa na ofisi tulizopanga na kulipa mamilioni ya fedha za ruzuku na misaada kwa manufaa ya Mwenyekiti Freeman Mbowe na Mkurugenzi wa fedha wanaomjua mmiliki wa jengo la makao makuu. Kimsingi mimi natambua chama kina uwezo mkubwa wa kuwa na majengo yetu.
3; kupunguza mshahara wa katibu mkuu Ndugu Dk. Slaa ambao ni zaidi ya milioni saba kwa mwezi na marupurupu kibao ili pesa hizo na mamilioni zielekezwe kujenga chama mikoani kama kweli tunataka 2015 tuingie Ikulu.
4; kuhakikisha pesa zilizochangishwa kwenye M4C zinatumika ipasavyo na si kama zitumikavyo kipindi hiki ambapo ni kama tumelewa wingi wa watu kwenye mikutano ya hadhara.
5; Kitendo cha Mwenyekiti wa chama kufumbia macho hatua ya ndugu Slaa-katibu mkuu kujikopesha pesa ya ruzuku ya watanzania zaidi ya shilingi milioni mia na arobaini.
7; Hatua ya mwenyekiti ndugu Heche kulipwa mshahara na marupurupu hali kanuni za chama haziruhusu huku Mbowe akifumbia macho wakati viongozi wa mikoa na wilaya hawapewi pesa na vifaa vya uenezi.
8; kitendo cha mchumba wa Dk. Slaa,; Josephine Mushumbushi kuzunguka mikoani na kulazimisha kupokelewa kama mke wa mfalme na kuendesha vikao vya ndani na mikutano ya hadhara yenye kulenga kuwajenga wagombea ubunge anaowataka yey e na katibu mkuu kwa mwaka 2015.
Ndugu wanahabari, je hizi ndo hoja za kitoto anazodai Mh. Mbowe? Hivyo basi namtaka Mh. Mbowe sasa asikimbilie kujibu hoja kiushabiki. Ajitahidi kuwa na fikra na Busara ili kukisaidia chama kuvuka kwenye daraja la sasa la pepo kufukuzana. Atambue Baraka anazozitoa wanachama wafukuzwe hovyo na kunyanyaswa ni hatari kwa kuwa anaandaa kundi kubwa nje ambalo litageuka mwiba siku za usoni.
UHALISIA ULIOPO
Ndugu waandishi wa habari, Naomba kuweka wazi kwamba mimi Juliana Shonza ni Makamu Mwenyekiti halali wa baraza la vijana (BAVICHA). Taarifa zozote zile mlizozisikia kuhusu kuvuliwa kwangu uanachama, naomba kwa nguvu moja kupitia taaluma yenu muwaambie watanzania kwamba wazipuuze. Ni taarifa zilizotolewa na kikundi cha kihuni kilicho lenga kutimiza matakwa ya wakubwa wao. Kikundi hicho hakina mamlaka ya kikatiba yoyote yale ya kunivua uongozi huu nilio nao.
Kuthibitisha hilo kuwa ni kikundi mufilisi, hadi ninapoandika waraka huu kwenu sijapewa barua yoyote ile inayonitaarifu kuwa nimevuliwa uongozi wangu. Hii ni wazi wanatambua kuwa wanachemka, wanatengeneza makundi kwa maslahi wanayoyaona yanawafaa.
Sikuchaguliwa ili niwe chombo cha kuwatumikia watu, na badala yake nilichaguliwa ili niwatumikie vijana wa CHADEMA na watanzania kwa ujumla, na pale nilipoona kuna ukiukwaji na kuhoji ndio chanzo cha mizengwe na matamko ya Ndugu Wegesa (John Heche).
Nimekuwa nikiwasumbua viongozi wenzangu kuhusu kutengeneza kadi za BAVICHA na kusajili wanachama katika mfumo mzuri (database) ili tuwe na kumbukumbu ya wanachama wetu lakini yote yameshindikana kwa sababu amekuwa akiendeshwa na mfumo dume kandamizi kwa mwanamke, mara nyingi nimemshauri kwa ajili ya maendeleo ya Baraza na nimekuwa nakwamishwa na Mwenyekiti na Katibu na hata leo sisi wote ni wanachama kwa kufikirika (imagination), kwa kuwa bado hatuna kadi za uanachama kwa vijana wa BAVICHA zaidi ya kutambulika na katiba ya chama.
KUKIUKWA KWA KATIBA
Ndugu wanahabari, ni wazi kuwa katiba pamoja na mwongozo wa baraza letu la vijana bavicha ulikiukwa katika kikao walichokiita kamati tendaji iliyokaa tarehe 05/01/2012 ambayo iliongozwa na Bwana Wegesa Suguta (John Heche) kama Mwenyekiti, hali inayonilazimu kusema wazi, bila kumung’unya maneno kwamba maamuzi yaliyotolewa na kikao hicho yalikwisha pangwa na viongozi wa kitaifa hayakuwa halali.
Nasisitiza kwamba ni ukweli ulio wazi kwamba agenda na maazimio ya kikao hicho yalikwisha amuliwa hata kabla ya kikao hicho kwasababu kubwa mbili
1;Taarifa za kufukuzwa kwetu zilikwisha anza kusikika kwenye mitandao ya kijamii kama vile jamii forum na facebook mwezi mmoja kabla ya kikao cha kamati tendaji batili.
2;Pili ushahidi wa kimazingira kwa maana ya ukiukwaji mkubwa wa kikatiba na mwongozo wa Baraza letu la Vijana uliofanyika siku ya kikao.
Ndugu wanahabari ikumbukwe kuwa pamoja na uwepo wa taarifa za kikao mwezi mmoja kabla binafsi nililetewa taarifa hizo siku mbili kabla ya kikao, tena kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi {sms} na baadae kupigiwa simu na Katibu wa Baraza Bwana Munishi ikinitaka kuhudhuria kikao hicho kutokana na kuwa nje ya Dar-es –salaam kwa mambo yakifamilia zaidi niliwataarifu viongozi wenzangu kwa utaratibu maalumu wa mawasiliano ya kiuongozi kwa maana ya kuwatumia barua ya udhuru wakutohudhuria kikao.
Lakini chakushangaza na kustaajabisha kwa viongozi wenzangu hawa ambao kwa namna moja ama nyingine napata ugumu wakuelewa kama kweli wana sifa za kuitwa viongozi tena wa idara nyeti sana katika ustawi wa chama chetu ,kwa makusudi kabisa ama kwakutumwa kufanya hivyo ama kwa utashi wao mdogo wa kiupembuzi yakinifu waliamua kuvunja na kukiuka katiba ya chama na kujipa vyeo vya kiunyampara kwakuamua kuchukua maamuzi yakutuvua uanachama wa kufikirika wa baraza mimi na vijana wenzangu Ndugu Mwampamba na Mchange ambao nao hawakupewa nafasi yakusikilizwa, ambao moja kwa moja tunapoteza sifa yakuwa wanachama wa CHADEMA.
Ndugu wanahabari naomba sasa nijikite katika katiba ya chama changu na mwongozo wa baraza la vijana sura ya sita kipengele cha 6.5 ambacho kinasema taratibu zifuatazo lazima zifuatwe katika kuchukua hatua za kinidhamu. 6.5.2 kwa mujibu wa ibara 5.4.3 na .4.4 ya katiba, mwanachama yeyote hatachukuliwa hatua za kinidhamu ama kuonywa ama kuachishwa ama kufukuzwa uanachama bila kwanza
{a} kujulishwa makosa yake kwa maandishi na kutakiwa kutoa majibu katika muda usiopungua wiki mbili.
[b] kupewa nafasi yakujitetea katika kikao kinachohusika.
{c} Mwanachama atajulishwa kwa maandishi uamuzi wa kikao mnamo wiki mbili baada ya kusikilizwa.
Ndugu waandishi wa habari,Niseme wazi kwamba hakuna kifungu kilichofatwa kati ya hivyo niliyoviainisha hapo juu, hakuna barua yeyote niliyojulishwa ya hayo waliyoyaita mashitaka yangu zaidi yakuyasoma na kuyasikia kwenye vyombo vya habari baada ya wao na kikao chao haramu kuchukua maamuzi yakunivua uanachama wa Bavicha .
Sikupewa nafasi yakujitetea maana sikuwepo kwenye kikao, barua ya udhuru wakutohudhuria walikuwa nayo. Na vile vile mpaka leo hii sijajulishwa kwa maandishi uamuzi wa kikao hicho batili badaa yake viongozi wenzangu hawa wameamua kuujulisha umma wa Watanzania na wanachadema kwa ujumla pasipo kunijulisha mimi kwanza.
Ukiangalia pia kifungu cha 6.5.6 cha katiba kinasema KIONGOZI YEYOTE hatachukuliwa hatua za kinidhamu bila kwanza kupewa mashitaka kwa maandishi na mamlaka husika na kupewa nafasi ya kujibu kwa maandishi. Sasa basi namtaka Bwana Wegesa Suguta awaeleze umma wa watanzania kama alivyokurupuka kuwaeleza kwamba Shonza amevuliwa uanachama wa Chadema ni wapi na lini yeye kama Mwenyekiti nilipewa barua ya hayo wanayoyaita mashitaka, na ni lini niliwapa majibu ya mashitaka hayo.
UHALALI WA KIKAO CHA KAMATI TENDAJI
Ndugu wanahabari ikumbukwe kwamba kikao cha juu kuliko vyote kwenye ngazi ya chama husika ni Mkutano Mkuu ambao ndio ulioniweka madarakani kutokana na kuwa na imani na mimi na kikatiba ndio haswa ulipaswa kuniandikia mashitaka, kunijadili, kunihoji na kutoa maazimio ambayo yangepelekwa kamati kuu ambao kimsingi ndiyo yenye mamlaka ya mwisho yakumvua mtu yeyote uanachama wake baada ya kujiridhisha na taarifa na uchunguzi kutoka kwenye kikao husika kilichomwandikia mwanachama mashitaka na kumuhoji.
Ndugu wanahabari ifahamike wazi kwamba kikatiba kuna ngazi mbili tu zinazoweza kumvua mtu uanachama wake ambazo ni ngazi ya tawi na ngazi ya kamati kuu. Hivyo basi namtaka sasa Bwana Wegesa Suguta auambie umma wa watanzania kwamba ni lini kamati tendaji ya vijana iligeuka ama kukaimishwa madaraka ya ngazi ya tawi, ngazi ya mkutano mkuu ama kamati kuu yakuwa na uwezo wakumvua kiongozi uanachama wake?
Ndugu waandishi wa habari, Wajumbe wa kamati tendaji kikatiba ni makatibu wa kamati za uratibu za mikoa lakini badala yake Bwana Wegesa Suguta (John Heche) amekuwa akiwaita wenyeviti wa mikoa na sababu kubwa ikiwa ni kwamba wengi wa wenyeviti hao hawastahiri kuwepo bavicha kutokana na kwaba umri wao kuwa zaidi ya miaka 35 hivyo kupoteza sifa zakuwa viongozi wa bavicha ambayo katiba inamtaka mwanabavicha yeyote kuwa na miaka 18-35, hivyo basi kwakuhofia kupoteza nafasi zao hulazimika kukubaliana na lolote lile ambalo bwana Wegesa Suguta analitaka hata kama wakijua kwamba ni kinyume kabisa na matakwa ya katiba na mwongozo wa baraza. Hivyo kumpa Heche mwanya wakuamua lolote lile analotaka ama kutumwa kulifanya.
Kutokana na hilo natangaza wazi kwamba kikao cha kamati tendaji kilichopita ni batili, chenye wajumbe batili, kimesimamiwa na viongozi batili kwa maana ya mwenyekiti na katibu wake maana wameshindwa kuheshimu misingi ya kikatiba katika namna ya demokrasia ya chama chetu hivyo basi nachukua nafasi hii kuutangazia umma wa watanzania na wanachadema kwa ujumla wao kwamba maamuzi ya kamati tendaji yaliyotangazwa na kiongozi kilaza na daraja la viongozi wa juu bwana Wegesa Suguta ni batili.
Ndugu wana habari, sifa ya Mwalimu ni kuweza kubadilisha hali ya umbumbumbu wa wanafunzi wake, Heche kama kiongozi, na Mwalimu kitaaluma (nina wasiwasi na ufaulu wake katika huo ualimu) alipaswa kuwa mfano bora kwa vijana wa Chadema kuwaelekeza na kuwafundisha namna yakuheshimu misingi ya kikatiba ambayo kama chama na baraza tumejiwekea na tunapaswa kuifuata ni wazi kuwa Heche ameshindwa kuwa mfano bora kwa vijana, hajui kanuni za BAVICHA wala katiba ya CHADEMA, mkurupukaji, mropokaji, mwenye uwezo mdogo wa kufikiri, dikteta anayetumia mamlaka asiyokuwa nayo (akipewa mamlaka atatuchinja huyu) hivyo hafai kuwa hata Mwenyekiti wa serikali za mtaa, wala kuaminiwa popote kupewa nafasi ya kiuongozi. Ni wazi ubongo wake yeye na katibu baraza bwana Munishi haujapewa tohara la kisiasa, ifike mahali wakubali kufundwa unyagoni na manyakanga wa kisiasa.
KUHUSU KUVULIWA UANACHAMA WA BAVICHA;
Ndugu wanahabari, kuhusu kuvuliwa uanachama wa Bavicha ambao moja kwa moja napoteza sifa ya kuwa mwanachadema namshangaa kiongozi huyu ambaye sifa yake kuu siku zote ni ukurupukaji kwakusema kwamba nimevuliwa uanachama wa Bavicha huku akijua wazi Bavicha haijawahi kuwa na kadi za baraza.
Katika mwongozo wa baraza la vijana kipengele cha 4.4 KUJIANDIKISHA UANACHAMA
4.4.1 inasema ili kijana aruhusiwe kujiunga bavicha ni lazima awe na sifa zifuatazo
[a] Awe mwanachama wa CHADEMA
[b] Awe na umri kati ya miaka 18 na 35
[c] Awe anakubaliana na misingi ya mwongozo wa BAVICHA
4.4.2 Inasema kijana aliyekidhi matakwa hayo hapo juu, atanunua kadi ya uanachama wa BAVICHA
Kutokana na kipengele hicho namtaka bwana Wegesa Suguta auambie umma wa watanzania na wanachadema kadi yake yeye ya baraza la vijana ni namba ngapi na aliichukulia wapi? Aueleze umma wa watanzania kadi yangu ya baraza la vijana ni namba ngapi na niliichukulia wapi?
Ndugu waandishi wa habari,Ni dhahiri baraza la vijana chadema hatuna kadi ambayo kimsingi ndiyo utambulisho wa mwana bavicha endapo akishakidhi sifa zilizoainishwa hapo juu. Na ni wazi kwamba vijana wote wa chadema tuna sifa za kuwa wana Bavicha lakini si wanachama wa BAVICHA kutokana na kwamba nimekuwa nikimwambia mara kwa mara umuhimu wa kuirasimisha na kuianzisha ili iwe taasisi kamili kwa kuwa na kadi za vijana kama mwongozo wa vijana unavyojieleza.
UELEWA WANGU KUHUSU KUNDI ANALOLIITA NDUGU WEGESA SUGUTA (JOHN HECHE) NI “MASALIA”
Ndugu waandishi wa habari, Hakuna kundi linaloitwa masalia ndani ya Chadema na BAVICHA. Gazeti la MWANAHALISI ndilo lililoandika kuwa vijana wote waliofutwa na kuondolewa kwenye uchaguzi wa BAVICHA mwaka 2011 ni MASALIA ya Zitto yanayopukutishwa Chadema. Kimsingi gazeti hili lilikuwa linafanya kazi yake ya kipropaganda ndani ya CHADEMA ili kukigawa Chama. Lilikuwa linatimiza wajibu wake wa kupika mpasuko ndani ya chama tena kwa kuhusisha na viongozi wakubwa ndani ya chadema.
Ni aibu kubwa sana na ni hatari kuona kiongozi kama Wegesa Suguta anakuwa mstari wa mbele kushabikia neno masalia, huku akijua wazi kufanya hivyo ni kuligawa baraza la vijana. Kwa nguvu moja nalaani kitendo hiki cha kipuuzi kinachofanywa na Mwenyekiti huyu wa BAVICHA cha kuchekelea upuuzi uliopikwa na gazeti la Mwanahalisi.
Naomba atumie rasilimali za chama kujenga umoja wa vijana imara, tushirikiane kuimarisha Bavicha yenye tija kwa chama na sio kusherekea mpasuko ndani ya baraza la vijana.
UELEWA WANGU KUHUSU KITU KINACHOITWA PM7
Ndugu waandishi wa habari, Naomba kunukuu maneno ya mtu maarufu sana mitandaoni na kwenye uga wa habari Mzee mwanakijiji anasema”Uongozi imara sio kutegeana, kunyemeleana na kufukuzana. Uongozi imara ni kushirikiana”.PM7 ni jina lenye maana ya “PATRIOTIC MOVEMENT” yaani harakati za kizalendo kwa mujibu wa Ndugu Ben saanane ambaye alitumwa na kiongozi wa juu wa chama kuja kulitekeleza kwa vijana walioenguliwa kwenye uchaguzi wa BAVICHA mwaka 2011 na wanaoonekana kusigana na kiongozi huyo kimawazo. PM7 ni wazo liliobuniwa na kiongozi mmoja wa juu wa chama akishirikiana na Ben saanane wakinuia kutega mtego wa kuwanasa vijana wanaoonekana wapo tofauti kimawazo na kiongozi huyo wa chama.
Kwa kuwa wazo hilo lilikuwa halina manufaa kwa chama, halikutekelezwa. Kiongozi huyo bila kumung’unya maneno ameamua kuwa tumia vijana hao kuandaa kikao batili cha kamati tendaji ya John heche ili awafukuze vijana hao. Hii ni hatari sana kuona kiongozi wa chama unageuka simba na kuanza kuwawinda watoto wake ili uwamalize kisiasa kwa sababu zako binafsi.
MAAJABU KATIKA MEDANI ZA SIASA ZA BAVICHA MWAKA 2013
Ndugu waandishi wa habari.
1. Hii ni ajabu sana katika kikao cha kamati tendaji batili, Ambao hatukuhojiwa ni watu wawili, mimi Juliana Shonza na kijana mmoja anaitwa Exaud Mamuya. Lakini Mimi Juliana Shonza nimehukumiwa bila hata kusikilizwa wala kupewa mashitaka na chombo chochote katika chama.
Wakati huo huo Exaud Mamuya hajahukumiwa kwa madai hakufika kwenye kikao.
Hii ni dhahiri huu ni mkakati wa kipuuzi ambao unaendeshwa na watu wapuuzi tena kwa misingi ya kikabila na kikanda.
2. Muasisi mwenza wa PM7 na kibaraka wa kiongozi wa juu wa chama aliyetumika kutoa shutuma chafu kwa Naibu Katibu Mkuu. Kijana anayefahamika kwa jina la Ben Saanane ameachwa kwa madai yeye amekiri mbele ya hiyo kamati tendaji kwamba ni kweli alinuia kumchafua Naibu Katibu Mkuu wa chama na kukivuruga chama. Wakati tuhuma zake zinafanana na za Mchange na Mwampamba.
3. Mkakati wa John heche na vibaraka wake umejikita kutukuza ukanda ndani ya chama tena wa wazi wazi. Ukanda huu umejidhihirisha kwenye kutoa hukumu batili za tuhuma kama ifuatavyo.
-Vijana waliohukumiwa wote ni wale wanaotokea Mbeya, Mbozi na Kibaha. Wakati -Vijana wa Kilimanjaro wameachwa kwa madai wao wametoa ushirikiano.
Waliohukumiwa ni:
_Mtela mwampamba-Mbozi, mbeya
_Habib Mchange-Kibaha, pwani
_Juliana Shonza-Mbozi, mbeya
- Joseph kasambala – mbeya mjini (kasimamishwa)
- GWAKISA Mwakasendo –Rungwe, mbeya (kasimamishwa)
Pamoja na wanachama watatu waliopo mbeya mjini waliofukuzwa uanachama.
Waliosamehewa ni:
_Ben saanane-Kilimanjaro
_Exaud Mamuya-Kilimanjaro.
Hii ni dhamira ya wazi kabisa kwamba CHADEMA sasa ni chama cha kikanda, Viongozi wa chadema wanatumika kutangaza ukanda kwa watanzania. Kwa maana hiyo wale wote wasio wakaskazini ndani ya Chadema tusitegemee kutendewa haki.
MAMBO NILIYOMSHAURI HECHE NA KUMUONYA
Ndugu waandishi wa habari, Sisi kama vijana tusigeuze siasa kuwa ajira wala chombo cha kuendeshea maisha, ni moja ya vikwazo katika kukuza demokrasia ya kweli, maana wengi wanaendekeza njaa na uhitaji wa maisha yao ili kupindisha ukweli.
Moja ya maswali yangu kwa Mwenyekiti ni kitendo cha kubinafsisha gari alilotoa Naibu Katibu Mkuu kwa ajili ya BAVICHA na badala yake akalifisadi, akafanya mali yake binafsi na kumuweka Mdogo wake Chacha Heche kuwa dereva wake, nimekuwa nikipinga matumizi mabaya ya rasilimali hiyo kwa manufaa binafsi, na badala yake gari hiyo ifanye kazi iliyokusudiwa, huu ni msingi wa kuonyesha tofauti yetu na wanaotumia rasilimali za serikali (Taifa) kwa manufaa binafsi nay a familia zao.
Pia nilimshauri Mwenyekiti awe na kipato halali kama katiba ya chama inavyosema Sura 10 MAADILI YA VIONGOZI ibara ya 10 kifungu cha (6) kinasema Kiongozi anatarijiwa kujitosheleza yeye na familia yake kwa mapato halali ili kutokuwa ombaomba kwani tabia hiyo itadhoofisha uwezo wake wa kutoa uamuzi sahihi, ili kuwa mfano bora wa uwajibikaji kwa vijana, kama ambavyo Mwalimu Nyerere alivyosema kipimo cha Utu ni kufanya kazi, badala yake ametelekeza taaluma ya ualimu, aliyotumia pesa za walipa kodi kwa kusoma na muda wote ni kupiga soga bila uzalishaji na kujipatia kipato halali, na badala yake anategemea mshahara usio halali kuishi, ni wazi Mwenyekiti ni cheo cha kisiasa na hatakiwi kulipwa mshahara, wala kulipiwa nyumba kwa mujibu wa kanuni. Badala yake majibu anafikiri ni kufanya njama na waliopindisha taratibu hizo ili alipwe mshahara kwa maslahi yao ya kisiasa. Na tumekuwa tukilipinga hilo kwani tunataka tuwe mfano wa utawala bora kwa vitendo na si maneno peke yake.
MWISHO:
Ndugu waandishi wa habari,Nipo kwenye mchakato na wanasheria wangu kushughurikia swala la kumpeleka mahakani Bwana John heche na gazeti la Tanzania daima toleo namba 2958 kwa kuniita msaliti wa chadema, natumiwa na CCM na kuwa nina mahusiano (natumiwa)na Wassira tena bila kunihoji mimi Juliana Shonza. Kwa maana hiyo wamenichafua na kunidhalilisha mbele ya umma wa watanzania.
Pili naomba kuweka wazi kwamba natarajia kuomba ufafanuzi wa kikatiba juu ya shutuma zilizotolewa kwenye vyombo vya habari dhidi yangu na bwana Wegesa Suguta (John heche) ili aseme ni aminisho lipi la kuthaminisha na kusakidikisha mtazamo wa maono yake ili bongo za watanzania zijue ukweli.
Mimi Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA natangaza rasmi Mtela Mwampamba na Habib Mchange ni wanachama hai na halali wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Hivyo nawaomba waendelee na kazi zao za ujenzi wa chama kwenye majimbo yao na taifa kwa ujumla. Nawaomba wananchi na wanachama wote wa chadema waendelee kuwa na imani dhidi ya vijana hawa. Kama mlivyomwamini Mwampamba na kumpa kura 32000 na kama mlivyo mwamini Mchange na kumpa kura 10400 kwenye uchaguzi wa Ubunge mwaka 2010. Vivyo hivyo naowaomba muendelee kushirikiana nao kuhakikisha wanatimiza adhima ya ukombozi mwaka 2015.
Wenu katika ujenzi wa demokrasia makini
Juliana Daniel Shonza
Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO