SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa kushirikiana na Kampuni ya Wings of Kilimanjaro ya nchini Australia, wameandaa safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro itakayowashirikisha watalii zaidi ya 100 ambao watashuka toka kwenye kilele cha mlima huo kwa kutumia miavuli maalumu.
Aidha, shughuli hiyo inayotarajiwa kukusanya dola milioni moja (sh bilioni 1.5) ambazo zitatumika kusaidia miradi ya wananchi wanaoishi kuzunguka hifadhi mbalimbali za taifa nchini.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini hapa juzi, Meneja Uhusiano wa Tanapa, Pascal Shelutete na Meneja Mradi wa kampuni hiyo, Adrian Mgrae, walisema fedha hizo zitaelekezwa kwenye miradi mbalimbali ya kukabiliana na umaskini vijijini, uharibifu wa mazingira na misaada ya kibinadamu.
Walisema misaada hiyo inajumuisha uchimbaji wa visima vya majisafi ya kunywa, kuboresha miundombinu ya elimu na kusaidia waathirika wa ukimwi, ikisimamiwa na mashirika yasiyo ya kiserikali ya One Foundation, Plant with Purpose na Worldsave International.
Watalii hao wanaotarajia kupanda mlima huo kupitia njia ya Machame kuanzia Januari 29, wanatarajiwa kushuka kwa kuruka na miavuli hiyo maalumu kati ya Februari 5 na 6 kulingana na hali ya hewa itakavyokuwa kwenye kilele cha Kibo.
Shelutete alisema watalii hao wanaotarajiwa kupanda mlima huo kwa siku saba, watatua kwa miavuli hiyo kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Umbwe na Chuo cha Ufundi stadi cha Kibosho wilayani Moshi, hivyo kuwahimiza wananchi kujitokeza kujionea tukio hilo la kihistoria.
Meneja Uhusiano huyo wa Tanapa alisema tukio hilo pia linatarajiwa kutoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 600 ambao watawahudumia watalii hao.
Mkurugenzi wa kampuni ya uwakala wa Utalii ya Top of Africa ya mjini Moshi, Silvanus Mvungi ambaye ndiye aliyeandaa safari ya watalii hao, alisema kuwa katika kuhakikisha usalama wa wageni hao kutakuwa na helkopta maalumu kwa ajili ya uokoaji ambayo itakuwa tayari muda wote mpaka kukamilika kwa shughuli hiyo.
Meneja Uhusiano wa Tanapa,Pascal Shelutete akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha juu ya watalii 100 watakaopanda mlima Kilimanjaro
Paula Mcrae ambaye ni Meneja mradi akiongea na wanahabari
Mkurugenzi wa Wings of Kilimanjaro Australia
Stori na Grace Macha, Arusha, Picha: Kilimanjaro Skydive, Jamii Blog
0 maoni:
Post a Comment