Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Serikali Yataja Manufaa kwa WanaMtwara Gesi Ikipelekwa Dar es Salaam

SERIKALI imetaja manufaa na faida ambazo wanatarajia kuzipata wananchi wa Mtwara pamoja na Lindi endapo gesi itasafirishwa kwenda Jijini Dar es Salaam.


Imesema Mkoa wa Mtwara ndipo utakapo jengwa mtambo mkubwa wa kusafishia gesi hiyo kabla ya kusafirishwa kwenda jijini Dar es Salaam kwa matumizi ya uzalishaji umeme na matumizi ya moja kwa moja viwandani.


Kauli hiyo imetolewa jana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alipokuwa akizungumza katika Kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na Kituo cha Radio One jijini Dar es Salaam.


Naibu waziri huyo ameweka wazi kuwa mkoani Mtwara licha ya Serikali kupanga kujenga viwanda vingine kadhaa, inajenga mtambo wa megawati 250 ambao utakuwa ukizalisha umeme na mwingine kujengwa mkoani Lindi eneo la Somanga Funga utakao kuwa ukizalisha megawati 520.


Akifafanua zaidi Simbachawene alisema eneo la Mikindani katika Kijiji cha Msijute mkoani Mtwara kinatarajiwa kujengwa kiwanda kikubwa cha saruji Afrika Mashariki na Kati chenye uwezo wa kutoaji ajira kwa watu 6000 jambo ambalo ni manufaa ya Wanamtwara.


Alisema pia tayari kuna wawekezaji wa viwanda vya mbolea wamejitokeza kujenga viwanda mkoani Mtwara na Serikali itaviacha vinu vya kuchimba na kusindika gesi eneo hilo jambo ambalo bado ni manufaa makubwa kwa wananchi.


“Viwanda vya kusindika gesi hii vimepangwa kujengwa maeneo ya Lubasi, Kishere, Mchinga Bay, Lindi, Sudi Bay, Airport pamoja na Mikindani…viwanda vyote hivi vitatoa ajira kubwa sana,” alisema Naibu Waziri.


Alisema licha ya manufaa hayo, gesi itakapopelekwa Dar es Salaam itazalisha umeme wa uhakika pamoja na kutumika moja kwa moja viwandani jambo ambalo litailetea taifa tija kubwa ikiwa ni pamoja kupunguza ukali wa maisha.


“Ni kweli gesi imepatikana Mtwara lakini ni lazima uipeleke sokoni ili iweze kupata soko (wateja)…Dar es Salaam ndio kwenye soko, huwezi ukaiacha Mtwara ambako hakuna soko; mbali na kuzalisha umeme kuna viwanda 37 na hoteli kadhaa zinataka ziitumie moja kwa moja ni lazima iletwe huku, Mtwara pale hakuna soko,” alisema.


Aidha alitolea mfano kuwa zipo nchi mbalimbali ambazo zimegundua gesi lakini zimelazimika kuisafirisha kwa mabomba kwenda eneo la soko. Alibainisha kuwa nchi ya Urusi inasafirisha gesi yake hadi nchini Ujerumani huku Iran ikisafirisha hadi India gesi yake kutafuta soko lilipo.


Alisema miundombinu mikubwa ya umeme ipo jijini Dar es Salaam hivyo kuna kila sababu ya gesi hiyo kuletwa jijini humo ili iweze kuzalisha umeme na matumizi ya viwandani moja kwa moja pamoja na matumizi mengine, ambapo tayari wateja wamepatikana.


Aidha aliongeza kuwa uzalishaji umeme wa kutosha kwa kutumia gesi utapunguza bei ya umeme na kuuzwa kati ya senti 6 na 8 za Marekani jambo ambalo litapunguza ugumu wa maisha na pia bei ya bidhaa nchini.


Pamoja na hayo amevitaka baadhi ya vyama vya siasa na taasisi zisizo za Serikali (NGO’s) zinazowapotosha Wanamtwara juu ya mradi huo kuacha kitendo hicho kwani hakuna asiyejua umuhimu wa gesi hiyo kuja Dar es Salaam.


“Hivi ni nani asiyejua kuwa tatizo la kutokua na umeme wa uhakika nchini ndilo linalokwamisha uchumi wa nchi…Tanzania inapoteza bilioni 4.5 kwa ajili ya kununua mafuta ya kuzalisha umeme kwenye mitambo yake, sasa gesi itaokoa fedha hizi,” alisema Simbachawene.


Hata hivyo amesema Serikali haiwezi utekeleza mradi huo kwa nguvu bali itaendelea kuwaelimisha Wanamtwara umuhimu na manufaa ya gesi hiyo kuletwa Dar es Salaam na inaimani wataelewa na malumbano kumalizika.

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO