Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Lema afunga sekondari Arusha

 lema press

MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema, ameifunga Shule ya Sekondari Korona iliyopo Kata ya Engutoto jijini hapa, ambayo ilizinduliwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, mwaka 2011.

Lema alifikia uamuzi huo katika kikao cha pamoja cha mashauriano shuleni hapo na Kaimu Mkuu wa Shule hiyo, Eusebi Maeda, kilichohudhuriwa pia na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji ambaye ni Ofisa Utumishi, Eliphas Mollel na Ofisa Elimu Sekondari, Violet Muwowoza.

Alisema kuwa aliifunga shule hiyo kutokana na kukabiliwa na matatizo mengi yaliyosababisha wanafunzi kushindwa kusoma tangu ifunguliwe Januari 14, mwaka huu.

Matatizo hayo ni pamoja na umbali unaosababisha wanafunzi na walimu kutembea kilometa 6.5 hadi kufika shuleni hapo, hivyo kuwa na muda mfupi wa masomo.

Shule hiyo pia haina huduma ya maji safi baada ya bomba lililokuwepo kukatwa na mamlaka ya maji kutokana na deni la sh 340,000. Pia, pamoja na walimu watano waliopo, mkuu wa shule na msaidizi wake hawaonekani.

Kati ya wanafunzi 1,200 wa kidato cha kwanza hadi cha tatu wa shule hiyo ni wanafunzi 118 pekee ndio wanaohudhuria masomo.

Lema aliwaagiza wanafunzi hao wafike ofisini kwake na wazazi wao kesho, huku akimtaka Diwani wa kata hiyo, Anthony Male, kwa kushirikiana na ofisa Elimu kuwahamishia kwa mafungu wanafunzi hao katika shule nyingine zilizomo ndani ya Jiji la Arusha.

Mbunge huyo aliahidi kutoa pampu ya kuvutia maji, vifaa vya kuzalisha umeme wa jua pamoja na matofali 3,000 na kwamba atashirikiana na mkuu wa wilaya na mkoa kuhakikisha shule hiyo inaboreshwa ndani ya miezi mitatu ili kutoa fursa ya kuchukua wanafunzi wa bweni.

Naye Ofisa Elimu Sekondari, Violet Muwowoza, alijitetea kuwa yeye angeomba kwanza afuate  taratibu za kuandika barua kwa Ofisa Elimu Kiongozi ambaye ana mamlaka ya kufunga shule, jambo ambalo Lema alisema aendelee na taratibu zake wakati wanafunzi hao wakiendelea na masomo katika shule nyingine.

Aidha katika utetezi wake juu ya changamoto za shule hiyo, Ofisa Elimu huyo alisema alikwisha kuwahi kupeleka mapendekezo katika vikao vya baraza la jiji vya kununua magari ya wanafunzi lakini yakapingwa na kusema hata hivyo wengi wa wanafunzi waliopelekwa katika shule hiyo wanatoka shule za mchepuo wa Kiingereza, ndiyo maana hawaripoti shuleni hapo.

Kaimu Mkurugenzi alimuomba Lema asubiri kiitishwe kikao cha dharura cha baraza la madiwani wa jiji, alichodai huenda kitatoka na suluhisho zuri zaidi kuhusiana na shule hiyo.

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO