HALMASHAURI ya Jiji la Arusha, imeshindwa kupokea ruzuku ya Sh milioni 200 kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo baada ya kupata hati chafu kwa mwaka 2012. Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa juzi na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Omar Mkombole, wakati wa kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa.
Mkombole alitoa kauli hiyo baada ya kuhojiwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, aliyetaka kujua kwanini hawajaweza kuandaa mpango kabambe utakaotumiwa kuandaa mpango mji.
Akitoa maelezo yake mbele ya wajumbe wa kikao hicho akiwamo Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, alisema wameshindwa kufikia malengo hayo kutokana na kupewa hati chafu.
“Mwaka jana tumepewa hati chafu hivyo imetufanya kushindwa kuandaa master plan na imetufanya kukosa ruzuku ya shilingi milioni 200 za Wizara ya Ardhi,” alisema Mkombole.
Katika hatua nyingine, Katibu wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALAT), Tawi la Arusha, Khalifa Idda, alisema siri za kuepukana na kuendelea kupewa hati chafu ni wafanyakazi kuwa na umoja.
“Mkiweza kushiriki ALAT mtakuwa na nafasi ya kujadili mafanikio na changamoto za waliovuka na walioshindwa. Ni vema halmashauri na wataalamu wakatumia vema Jumuiya hii,” alisema Idda
.Chanzo: Mtanzania
0 maoni:
Post a Comment