Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Wabunge waanza kujiandikisha JKT

jkt

JKT wakiwa kwenye mazoezi kwa ajili ya ukakamavu wa kulijenga taifa Tanzania, Wabunge wameanza kujiandikisha tunaamini watafanikiwa kwa kiasi kikubwa .

*******************

WABUNGE vijana katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wameanza kujiandikisha tayari kwa kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa Mujibu wa Sheria kwa ajili ya mafunzo yatakayoanza Machi mwaka huu.

Taarifa ambazo Mwananchi Jumamosi ilizipata juzi, zimeeleza kuwa, idadi ya wabunge ambao tayari wamejiandikisha kujiunga na JKT hadi sasa ni zaidi ya 31, huku wengine wakiendelea.

Kujiandikisha kwa wabunge hao ili wajiunge na JKT kunafuatia wito uliotolewa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Julai mwaka uliopita, alipowasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake katika Bunge la Bajeti mjini Dodoma.

Kwa nyakati tofauti wabunge vijana kutoka CCM, Chadema na NCCR- Mageuzi walilithibitishia gazeti hili kuwa tayari wamejiandikisha katika Ofisi ya Katibu wa Bunge kwa ajili ya mafunzo hayo.

Imebainishwa kuwa, miongoni mwa wabunge waliojiandikisha, wamo pia ambao waliwahi kupitia mafunzo hayo, ikielezwa kuwa wamefanya hivyo wakitaka kwenda kujikumbushia.

Hata hivyo, Kaimu Katibu wa Bunge, Eliakimu Mrema hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo akieleza kuwa linaweza kuzungumziwa na Spika wa Bunge kwa kuwa ndiye anayezungumzia masuala ya wabunge.

“Sisi kazi yetu ni utendaji tu na masuala ya wabunge, Spika ndiye anayezungumzia,”alisema Mrema.

Alipotakiwa kuzungumzia taarifa hizo, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema kwamba ni mapema mno kuzungumzia suala hilo kwa kuwa hawajapata idadi kamili.

“Tukiwa Dodoma (bungeni), ukituuliza tutakuwa tayari kutoa taarifa kamili, lakini kwa sasa ni mapema kuzungumzia suala hilo,”alisema Ndugai na kuongeza:

“Watu ni rahisi kusema, lakini wakati mwingine utekelezaji ni mgumu kama unavyosema kwani, ukisikia moja ya uamuzi mgumu, hili ni mojawapo.”

Ndugai alisema kuwa mafunzo hayo hayatawahusu wabunge ambao waliwahi kupitia JKT siku za nyuma na kwamba ni maalumu kwa wabunge vijana.

“Naomba usubiri Dodoma, tutakuambia hali ilivyo,” alisema Ndugai.

Katibu wa wabunge wa Chadema, David Silinde alisema kuwa wabunge vijana wa chama hicho, tayari wameshajiandikisha na kuwasilisha majina yao kwa Katibu wa Bunge kwa ajili ya mafunzo hayo. “Sisi tumeshajiandikisha katika awamu ya kwanza na ya pili na majina tumeshayawasilisha kwa Katibu wa Bunge kwa ajili ya utekelezaji,” alisema Silinde.

Silinde ambaye ni Mbunge wa Mbozi Magharibi, alitaja wabunge wa Chadema ambao tayari wameshajiandikisha pamoja na yeye mwenyewe kuwa ni Mariam Msabaha (Viti Maalumu), Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini), Ezekiah Wenje (Nyamagana) na Godbless Lema (Arusha Mjini).

Alisema wengine ni Raya Ibrahim (Viti Maalumu), Sabrina Sungura (Viti Maalumu), Cecilia Pareso (Viti Maalumu) na Joshua Nassari (Arumeru Mashariki).

“Hayo majina wabunge saba walijiandikisha awamu ya kwanza na wawili wamejiandikisha awamu ya pili kwa ajili ya mafunzo hayo,” alisema Silinde.

Mbunge wa Kasulu Mjini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, Moses Machali alisema kuwa naye tayari ameshajiandikisha kujiunga na JKT katika Ofisi ya Katibu wa Bunge na kwamba yupo tayari kujiunga na mafunzi hayo.

“Mimi tayari nimeshajiandikisha, tunasubiri tu kwenda kwenye mafunzo hayo,”alisema Machali.

Mbunge mwingine aliyejiandikisha ni Deo Filikunjombe wa Ludewa na Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (wote wa CCM).

Akizungumzia hatua hiyo, Nchemba alisema kuwa naye pia ameshajiandikisha na kwamba wabunge wengi wa CCM, ambao ni vijana, watajiunga na mafunzo hayo.

“Mimi niko tayari na kwamba tutakwenda kwa wingi kwa kuwa kuwepo kwa JKT ni kutekeleza Ilani ya chama changu, lakini naona muda waliotupangia ni mdogo, nitaomba uongezwe,”alisema Nchemba.

Alisema yeye kama mbunge na pia Naibu Katibu Mkuu wa CCM, atahimiza wabunge wote wa CCM, ambao ni vijana kujiunga na mafunzo hayo na kwamba ni lazima wote wajiunge.

Kwa mujibu wa waziri Nahodha, ingawa JKT ipo tayari kuchukua vijana 20,000 kwa wakati mmoja, lakini haitaweza kufanya hivyo kutokana na gharama za kuendeshea mafunzo hayo kuwa kubwa.

Kwa mwaka huu, tayari JKT imetangaza kusajili vijana 5000 kati ya 41,348 waliohitimu Kidato cha Sita na kwamba Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, imeweka vigezo maalumu vya kuwapata vijana hao kwa kuzingatia makundi ambayo mchakato wa kuyatangaza unaendelea.

Mafunzo hayo kwa mujibu wa sheria yatafanyika kwa miezi sita katika kambi za Bulombora na Kanembwa (Kigoma), Mlale (Ruvuma), Mafinga (Iringa), Msange (Tabora) na Oljoro (Arusha).

Picha na Stori: Gazeti la Mwananchi, Januari 20, 2013.

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO