Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Maggid Mjengwa - Gesi Yetu Na Alichoniambia Profesa Chachage Jana Usiku...

Ndugu zangu,

Gesi Yetu Na Alichoniambia Profesa Chachage Jana Usiku...

Ndugu zangu,

Profesa Chachage ananiambia: " Binadamu havunjwi kwa pesa wala kwa mabavu"

Jana kuamkia leo nimelala usiku wa manane, nilikuwa naongea na Profesa wangu Chachage. Napata tabu kumwita marehemu, maana, unapomsoma Chachage unaona jinsi fikra zake zilivyo hai kuliko labda za walio hai.

Naam, jana usiku, baada ya kutafakari sana yanayotokea Mtwara na hususan sakata la gesi, niliamua kupekua kwenye maktaba yangu, huko nikakutana na maandiko ya Profesa Chachage. Ikawa ndio chakula changu cha kulalia. Hakika, ilikuwa ni kama nazungumza na Profesa Chachage.

Na kwa anachozungumza kupitia kitabu chake cha ' Makuadi wa Soko Huria', Profesa amenishawishi nipange safari ya kwenda Lindi na Mtwara. Nitapenda nikutane na baadhi ya aliokutana nao huko, maana, mazungumzo na watu hayo yamo kitabuni pia. Na majina ya watu hao yanafahamika.

Naamini, kuwa ukitaka kujua unakokwenda, angaza kwanza ulikotoka, ndipo utaelewa ulipo, na labda kwanini uko hapo. Kisha utapata mwanga wa unakokwenda.

Chachage alikiona kile ambacho wengi hawakukiona, wachache walikiona, lakini hawakutaka kukiona. Kinachotokea Mtwara na Lindi leo Profesa Chachage alikiona, na ushahidi uko kwenye maandiko yake. E nendeni mkayasome.

Chachage aliweka kando usomi wake, aliwasikiliza watu wa Mtwara na Lindi. Kupitia maandiko yake, Profesa Chachage anatuma nafasi adimu ya kuwasikiliza Watanzania wa Mtwara na Lindi. Walichokisema Wazee wale wa Mtwara na Lindi miaka ile, ndicho kinachotokea sasa, walishaziona ishara.

Lakini wanasiasa waliwabeza, na ndilo kosa linalotaka kurudiwa sasa, kuwabeza watu wa Lindi na Mtwara kuhusiana na suala gesi. Ninapomsoma Chachage, na ninapoona ya sasa, mimi kama Mtanzania, siioni njia nyingine ya kumaliza kadhia hii ya gesi kwa amani bila Serikali na Wananchi wa Lindi na Mtwara kupitia wawakilishi wao, kukaa chini na kuzungumza.

Siku zote naamini, kuwa ' Kila kitu inazungumzika, ni namna tu ya kuutafuta msogeleo sahihi ( approach)'.

Hebu nikumegee kidogo alichoambiwa Profesa Chachage na watu wa Lindi;

" Wanataka kufuga kamba! Hawa walioumbwa na Mwenyezi Mungu. Tunasikia kwamba wanataka kuchimba mahandaki Rufiji yote na kutuhamishia twende tukaishi kwingine. Tukaishi wapi? Hawa wamekusudia kuangamiza maisha yetu na kututokomeza tupotee kabisa katika uso wa dunia hi!"

" Naye Makamu wa Rais (Marehemu Dr Omar Juma) alifika hapa na kihelikopta chake, kimezunguka leo kwenye vijiji vingi tu na kila alipokwenda , tunavyoambiwa , alikwenda kuhutubia. Hapa kwetu, badala ya kutusikiliza tuna nini cha kumwambia, alikuja akahutuhutubia kule shuleni.

Tulikuwa umati mkubwa tu, hata watu wa vitongoji na vijiji vya karibu walikuwepo. Haikuuwa hotuba, bali matusi kwa kadri tunavyofahamu sisi. Alidai ( Makamu wa Rais) kwamba sisi watu wa Rufiji ni wavivu na ndio maana hatuna maendeleo. Alidai kwamba rasilimali tunazo lakini tumezikalia, na ni kutokana na tabia zetu za ushirikina. sasa tunapinga mradi ambao utaikoa nchi yetu kwa kuiletea fedha nyingi za kigeni.

Alihitimisha hotuba yake kwa kudai kwamba kutokana na kupinga kwetu maendeleo ndio sababu tulikuwa tunaishi kwenye madungu na kushindwa hata kuwanunulia wake zetu nguo za ndani! Kama haya si matusi ni kitu gani? Na Kiongozi kama yeye kuthubutu kusema vile? Na hao wabunge wetu walitikisa vichwa kwa kuitikia pale mbele , kama vile sisi hatukuwachagua!" (Chachage; Makuadi wa Soko Huria, Ukurasa wa 152)

Naam, kuna mengi kwenye maandiko ya Chachage, nitazidi kuyachambua, yatusaidie kuyaelewa yanayotokea sasa, ili tupate mwanga wa tunakokwenda.

Maggid Mjengwa

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO