Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

MAONI YA CHADEMA JUU YA KATIBA MPYA YA TANZANIA

MAONI YA CHADEMA JUU YA KATIBA MPYA YA TANZANIA
Chadema wakienda kutoa maoni ya katiba
A. JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA MUUNDO WAKE
1. Kutakuwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo itakuwa ni shirikisho lililoundwa na nchi ya Tanganyika na nchi ya Zanzibar.
2. Kutakiwa na haki kamili ya kila nchi inayounda Jamhuri ya Muungano kujitoa katika Muungano lakini haki hiyo itatumiwa kwa masharti kwamba uamuzi wa kujitoa katika Jamhuri ya Muungano lazima upate ridhaa wa upande husika kwa kura ya maoni (referendum/plebiscite) kwa idadi isiyopungua theluthi mbili ya kura zote halali.
3. Kutakuwa na Serikali ya Muungano ambayo itakuwa na madaraka juu ya mambo ya Muungano pekee. Mambo ya Muungano yatakuwa yafuatayo:
(a) Mambo ya nje yanayohusu masuala ya diplomasia lakini yasiyohusu ushirikiano wa kimataifa;
(b) Ulinzi na usalama isipokuwa kwa masuala ya polisi na magereza;
(c) Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano (Supreme Court of the United Republic);
(d) Uraia na uhamiaji;
(e) Sera za fedha na sarafu;
(f) Sera za biashara ya kimataifa na masuala ya forodha;
(g) Masuala ya ithibati ya elimu ya juu.
4. Kutakuwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ambaye atakuwa Mkuu wa Serikali ya Muungano, Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Ulinzi ya Jamhuri ya Muungano.
5. Rais wa Jamhuri ya Muungano atachaguliwa na Wajumbe wote wa Bunge la Muungano, Bunge la Tanganyika, Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wenyeviti, mameya na magavana wote.
6. Rais wa Jamhuri ya Muungano atachaguliwa kwa kipindi kimoja cha miaka mitano na anaweza kuchaguliwa kwa kipindi kingine kimoja cha miaka mitano, na atachaguliwa kwa msingi wa kuachiana zamu ya kushikilia madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano Kati ya nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano.
B. MUUNDO WA VYOMBO VYA UTEKELEZAJI WA MAMLAKA YA NCHI
Shughuli zote za mamlaka ya nchi katika Jamhuri ya Muungano zitatekelezwa na kudhibitiwa na vyombo vitatu vyenye mamlaka ya utendaji, VYOMBO vitatu vyenye mamlaka yanutoaji haki na vyombo vitatu vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma.
1. Vyombo vyenye mamlaka ya utendaji vitakuwa ni Serikali ya Tanganyika; Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
2. Vyombo vyenye kutekeleza utoaji wa haki vitakuwa ni Mahakama ya Serikali ya Tanganyika, Mahakama ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mahakama Kuu ya Serikali ya Muungano.
3. Vyombo vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma vitakuwa ni Bunge la Tanganyika, Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Bunge la Jamhuri ya Muungano.
C. MGAWANYO NA UTENGANISHO WA MADARAKA
Mfumo wa sasa wa kikatiba umeondoa mgawanyo na utenganisho wa madaraka kati ya mihimili mikuu ya dola. Mfumo huu umeruhusu Serikali na hasa ofisi ya Rais kuwa na mamlaka makubwa juu ya mihimili mingine, yaani Bunge na Mahakama. Hali hii imeondoa udhibiti wa mamlaka na uwajibikaji katika mfumo mzima wa uongozi na utawala katika nchi yetu. Katiba Mpya iweke utaratibu ufuatao wa mgawanyo na utenganisho wa madaraka baina ya mihimili ya dola:
1. Dhana na nafasi ya Rais kama sehemu ya Bunge iondolewe katika mfumo wetu wa kikatiba bali abakie kama Mkuu wa Serikali.
2. Dhana na nafasi ya mawaziri - ambao pia ni wakuu wa Idara za Serikali - kama Wabunge iondolewe bali Bunge libakie kuwa la Wabunge na mawaziri wawajibike kwa Bunge hilo.
3. Rais asiwe na mamlaka ya kuteua Wabunge na Katibu wa Bunge ili hadhi ya Bunge kama chombo cha uwakilishi wa wananchi na uwajibishaji wa Serikali ilindwe.
4. Rais asiwe na mamlaka au uwezo wa kuvunja Bunge kwa sababu yoyote ile. Aidha, ili kuhakikisha Bunge linakuwepo muda wote ili kuisimamia Serikali muda wote, uchaguzi wa Bunge au sehemu yake utenganishwe na uchaguzi wa Rais.
5. Rais asiwe na mamlaka ya kupanga mishahara, posho na marupurupu ya Wabunge, bali kazi hiyo ifanywe na Tume huru ya Utumishi wa Bunge.
6. Mfumo mzima wa uteuzi wa Jaji Mkuu na majaji wengine wote wa Mahakama za juu ubadilishwe ili kuhakikisha Mahakama ina viongozi na watendaji wenye uadilifu, uwezo wa kitaaluma na uzoefu wa kiutendaji katika utoaji wa haki. Ili kutekeleza jambo hili, mfumo wa uteuzi wa majaji unapaswa kuwa kama ifuatavyo:
(a) Wanaotaka kuteuliwa kuwa majaji wa Mahakama ya Tanzania wapeleke maombi katika, wasailiwe na kuchujwa na, Tume huru ya Utumishi wa Mahakama katika mchakato ulio wazi;
(b) Majina ya Waombaji wenye sifa stahili za kuteuliwa majaji yapelekwe kwa Rais ili aweze kufanya uteuzi kutokana na mapendekezo ya Tume huru ya Utumishi wa Mahakama;
(c) Watakaoteuliwa na Rais wapelekwe Bungeni ili Bunge liridhie uteuzi wao kwa kutumia mchakato ulio wazi na baada ya kusikiliza maoni ya wadau wengine (confirmation hearings);
7. Rais asiwe na mamlaka ya kumwondoa, kumsimamisha au kumpatia kazi nyingine Jaji wa Mahakama ya Tanzania bali utaratibu wa kushughulikia nidhamu ya majaji uwe huru na wa wazi ili kuhakikisha uhuru wa Mahakama unalindwa kama ifuatavyo:
(a) Hoja yoyote ya kumwondoa Jaji wa Mahakama ya Tanzania ipelekwe kwa maandishi katika Tume huru ya Utumishi wa Mahakama;
(b) Tume huru ya Utumishi wa Mahakama ifanye uchunguzi wa awali (preliminary inquiry) ili kujiridhisha kwamba kuna sababu za msingi za kuanzisha uchunguzi wa kina wa kinidhamu juu ya Jaji husika;
(c) Tume huru ya Utumishi wa Mahakama iunde Tume huru ya Uchunguzi ya Kijaji (Judicial Commission of Inquiry) itakayojumuisha majaji kutoka ndani na nje ya Tanzania ili kufanya uchunguzi wa tuhuma dhidi ya Jaji husika;
(d) Tume ya Uchunguzi ya Kijaji ifanye uchunguzi wake kwa kufuata utaratibu ulio wazi na huru na utakaohakikisha Jaji husika anapatiwa fursa kamili ya kusikilizwa na ya kujitetea;
(e) Endapo Tume ya Uchunguzi ya Kijaji itathibitisha tuhuma dhidi ya Jaji husika basi Jaji huyo atalazimika kujiuzulu, na endapo Tume haitathibitisha tuhuma hizo basi Jaji ataendelea na madaraka yake lakini atakuwa na haki ya kulipwa fidia na/au gharama zake;
8. Rais asiwe na madaraka ya kuongeza muda wa ajira ya Jaji kwa sababu yoyote ile, na wala asiwe na mamlaka ya kupanga mishahara, posho na marupurupu ya majaji bali kazi hiyo ifanywe na Tume huru ya Utumishi wa Mahakama.
9. Rais asiwe na mamlaka ya kuteua watendaji wengine wote wa Mahakama wasiokuwa majaji bali watendaji hao wateuliwe na Tume huru ya Utumishi wa Mahakama kwa kufuata utaratibu wa wazi.
D. SERIKALI YA TANGANYIKA
1. Kutakuwa na Rais wa Tanganyika ambaye atakuwa Mkuu wa nchi na Mkuu wa Serikali ya Tanganyika.
2. Rais wa Tanganyika atakuwa na mamlaka na atatekeleza madaraka yote ya Serikali ya Tanganyika juu ya mambo yote yanayohusu Tanganyika.
3. Madaraka ya Serikali ya Tanganyika yatatekelezwa ama na Rais mwenyewe moja kwa moja au kwa kukasimu madaraka hayo kwa mawaziri ambao hawatazidi kumi na nane na hawatapungua kumi na tano au kwa watu wengine wenye madaraka katika utumishi wa Serikali ya Tanganyika kama itakavyowekwa katika sheria iliyotungwa na Bunge.
4. Madaraka ya Serikali ya Tanganyika katika majimbo yatatekelezwa na Serikali za majimbo zilizochaguliwa na wananchi wa majimbo husika na halmashauri za Serikali za mitaa katika majimbo hayo.
5. Rais wa Tanganyika atakuwa na mamlaka ya kuteua mawaziri wasiopungua kumi na tano na wasiozidi kumi na nane pamoja na manaibu mawaziri lakini uteuzi huo utapaswa kuthibitishwa na Bunge la Tanganyika baada ya utaratibu wa wazi wa kusikiliza maoni ya wadau (confirmation hearings).
6. Rais wa Tanganyika atateua watu wengine katika utumishi wa Serikali ya Tanganyika katakana na mapendekezo atakayopelekewa na tume huru za kitaalamu kama itakavyoelekezwa na sheria mahsusi iliyotungwa na Bunge la Tanganyika lakini uteuzi huo utapaswa kuthibitishwa na Bunge la Tanganyika.
7. Rais wa Tanganyika atakuwa na mamlaka kutangaza hali ya hatari kutokana na matukio au maafa yasiyotokana na nchi ya Tanganyika kuwa au kuingia vitani na nchi nyingine au kikundi cha watu ndani ya nchi ya Tanganyika.
8. Rais wa Tanganyika atakuwa na uwezo wa kutoa msamaha kwa watu waliopatikana na hatia na kuadhibiwa na mamlaka za utoaji haki za Serikali ya Tanganyika lakini uwezo huo utatekelezwa baada ya kupokea mapendekezo ya mamlaka zenye madaraka ya kusimamia urekebishaji wa tabia za wahalifu za Serikali ya Tanganyika.
9. Rais wa Tanganyika hatakuwa na kinga dhidi ya mashtaka ya jinai na madai kwa kosa ama jambo lolote atakalolitenda wakati akiwa Rais wa Tanganyika lakini mashtaka ya jinai yataendeshwa dhidi ya Rais baada kwanza ya Bunge la Tanganyika kupitisha azimio la kumwondoa Rais madarakani na endapo hoja ya kumshtaki itatolewa na kupitishwa na Bunge hilo.
10. Rais wa Tanganyika hatakuwa na mamlaka ya kutangaza vita wala kutangaza hali ya hatari isipokuwa kutokana na majanga, maafa au matukio yasiyokuwa ya kijeshi.
E. TAWALA ZA MAJIMBO NA SERIKALI ZA MITAA
1. Nchi ya Tanganyika itagawanywa katika maeneo kumi ya kikanda yatakayojulikana kama Majimbo kama ifuatavyo:
(a) Jimbo la Nyanza Magharibi ambalo litaundwa na mikoa ya sasa ya Kagera, Geita na Shinyanga;
(b) Jimbo la Nyanza Mashariki litakaloundwa na mikoa ya sasa ya Mara, Mwanza na Simiyu;
(c) Jimbo la Ziwa Tanganyika litakalojumuisha mikoa ya sasa ya Kigoma, Katavi na Rukwa;
(d) Jimbo la Kati litakaloundwa na mikoa ya sasa ya Tabora, Singida, Dodoma na Iringa;
(e) Jimbo la Kaskazini litakaloundwa na mikoa ya sasa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara;
(f) Jimbo la Pwani ya Kaskazini litakaloundwa na mikoa ya sasa ya Tanga, Wilaya za Bagamoyo, Chalinze, Kibaha, Kisarawe na Mkuranga katika Mkoa wa sasa wa Pwani na Wilaya za Gairo, Kilosa, Mvomero, Morogoro na Kilombero katika Mkoa wa sasa wa Morogoro;
(g) Jimbo la Mji Mkuu wa Dar es Salaam;
(h) Jimbo la Pwani ya Kusini litakaloundwa na mikoa ya sasa Lindi, Mtwara na Wilaya za Rufiji na Mafia katika Mkoa wa sasa wa Pwani, na Wilaya ya Ulanga katika Mkoa wa sasa wa Morogoro;
(i) Jimbo la Nyanda za Juu Kusini litakaloundwa na mikoa ya sasa ya Mbeya, Njombe na Ruvuma;
2. Majimbo yataongozwa na Gavana atakayechaguliwa moja kwa moja na wananchi katika Jimbo husika.
3. Miji, manispaa na jiji ndani ya majimbo itaongozwa na Meya atakayechaguliwa moja kwa moja na Wananchi katika Mji husika;
4. Maeneo yasiyokuwa Miji, manispaa na majiji itaunda halmashauri za wilaya zitakazoongozwa na Mwenyekiti atakayechaguliwa moja kwa moja na Wananchi katika halmashauri husika;
5. Halmashauri za Wilaya, Miji, manispaa na majiji zitakuwa na mamlaka ya kuteua na kuajiri watendaji wakuu, watendaji na watumishi wote katika maeneo yao kwa kadri itakavyoonekana inafaa na mamlaka hizo.
6. Kila Jimbo litakuwa na Baraza la Kutunga Sheria la Jimbo (Provincial Legislative Assembly) litakalochaguliwa moja kwa moja na Wananchi kwa utaratibu utakaowekwa na sheria iliyotungwa na Bunge la Tanganyika.
7. Majimbo yatakuwa na mamlaka ya kutoza kodi za aina mbali mbali katika maeneo yao na vile vile yatakuwa na haki ya kupata sehemu ya kodi itakayotozwa na Serikali Kuu kutoka ndani ya eneo la mamlaka ya Jimbo kwa kiwango kisichopungua asilimia arobaini ya kodi yote itakayokusanywa na Serikali Kuu katika Jimbo.
F. BUNGE LA TANGANYIKA
1. Kutakuwa na Bunge la Tanganyika ambalo litakuwa na sehemu mbili, yaani Bunge la Wananchi/Wawakilishi na Baraza la Majimbo.
2. Bunge la Wananchi/Wawakilishi litakuwa aina zifuatazo za Wabunge:
(a) Wabunge watakaowakilisha majimbo ya uchaguzi ambao idadi yao haitazidi Mia moja na hamsini;
(b) Wabunge watakaowakilisha halmashauri za wilaya ambao watachaguliwa kutoka miongoni mwa wanawake na ambao idadi yao haitazidi hamsini;
(c) Wabunge watakaotokana na orodha ya vyama vya siasa vilivyoshiriki kwenye uchaguzi wa Wabunge na kupata sio pungufu ya asilimia mbili ya kura zote zilizopigwa kwa ajili ya Wabunge katika uchaguzi huo. Idadi ya Wabunge hawa haitazidi hamsini na angalau nusu yao watatokana na watu waliogombea uchaguzi wa Wabunge katika majimbo ya uchaguzi na wakashindwa kwa kiasi kidogo cha kura; wakati nusu nyingine ya Wabunge hawa watatokana na uteuzi wa vyama vyao vya siasa hata hawakushiriki katika uchaguzi wagombea;
3. Majimbo ya uchaguzi kwa ajili ya Bunge la Wananchi/Wawakilishi yatagawanywa au mipaka yake kurekebishwa na Tume Huru ya Uchaguzi kwa kuzingatia idadi ya wakazi kama itakavyothibitishwa na sensa ya watu na makazi, na Majimbo yote ya uchaguzi yatakuwa na idadi sawa ya wakazi.
4. Bunge la Wananchi/Wawakilishi litakuwa na mamlaka ya kutunga sheria zote zinazohusu masuala ya kodi na fedha kwa ujumla na sheria nyingine zozote ambazo zitaanza kutumika baada ya kupitishwa na Bunge la Majimbo na kupata kibali na/au ridhaa ya Rais wa Tanganyika. Hata hivyo, sehemu yoyote ya Bunge la Tanganyika itakuwa na uwezo wa kutunga sheria ili mradi tu sheria hiyo haitatumika hadi hapo itakapopitishwa na sehemu nyingine ya Bunge na kupata kibali na/au ridhaa ya Rais wa Tanganyika.
5. Bunge la Majimbo litakuwa na wajumbe wasiozidi hamsini watakaochaguliwa kwa utaratibu ufuatao:
(a) Wajumbe thelathini watakaowakilisha Majimbo kumi ya nchi ya Tanganyika kwa utaratibu kwamba kila Jimbo litakuwa na wajumbe watatu na sio chini ya mjumbe mmoja kati yao atakuwa mwanamke;
(b) Wajumbe watakaotokana na watu waliokuwa wagombea katika uchaguzi wa Rais wa Tanganyika na kupata idadi isiyopungua asilimia tano ya kura zote zilizopigwa katika uchaguzi huo;
(c) Wajumbe watakaotokana na watu waliokuwa wagombea katika uchaguzi wa magavana wa Majimbo kumi ya Tanganyika na kupata idadi isiyopungua asilimia thelathini ya kura zote zilizopigwa katika Jimbo husika lakini hawakuchaguliwa katika uchaguzi huo;
(d) Wajumbe Watakaoteuliwa kutokana na orodha ya vyama vya siasa kwa kufuata uwiano wa kura zote ambazo kila chama cha siasa kilichoshiriki katika uchaguzi wa Wabunge wa Majimbo kitakuwa kimepata katika uchaguzi huo;
6. Bunge la Majimbo litakuwa chombo cha uwakilishi wa Majimbo na litakuwa na mamlaka ya kutunga ama kupitisha sheria, kuridhia mikataba ya kimataifa na kupitisha majina ya watu wote Watakaoteuliwa na Rais kushika madaraka katika utumishi wa umma katika nchi ya Tanganyika.
G. BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO
1. Kutakuwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano ambalo litakuwa na idadi sawa ya Wajumbe kutoka Tanganyika na Zanzibar na ambao watapatikana kwa utaratibu ufuatao:
(a) Wajumbe kumi kutoka kila upande wa Jamhuri ya Muungano ambao watachaguliwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Wawakilishi Zanzibar;
(b) Wajumbe ambao walikuwa wagombea nafasi ya Rais wa Tanganyika au Rais wa Zanzibar ambao walipata si chini ya asilimia tano ya kura zote halali zilizopigwa katika uchaguzi huo na ambao hawakuchaguliwa;
2. Bunge la Jamhuri ya Muungano litakuwa na mamlaka ya kutunga sheria zinazohusu mambo ya Muungano na pia kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma zinazohusu mambo ya Muungano.
H. MAHAKAMA ZA JAMHURI YA MUUNGANO
Mamlaka za utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zitakuwa kama ifuatavyo:
(a) Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
(b) Mahakama ya Tanganyika;
(c) Mahakama ya Zanzibar.
1. Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano (Supreme Court of the United Republic) itakuwa ndio Mahakama yenye mamlaka ya juu kabisa katika Jamhuri ya Muungano.
2. Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano itakuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi zote zinazohusu masuala ya Muungano na pia itakuwa Mahakama ya rufani ya mwisho ya kesi zote ambazo adhabu yake kifungo cha maisha au kifo.
3. Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano itakuwa na majaji tisa na itaongozwa na Rais wa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano na Makamu wa Rais ambao watateuliwa kwa kanuni kwamba endapo Rais atatoka upande mmoja wa Muungano basi Makamu wa Rais atatoka upande mwingine wa Muungano.
4. Mahakama ya Tanganyika itakuwa na sehemu tatu, yaani Mahakama za Mahakimu, Mahakama Kuu ya Tanganyika (High Court of Tanganyika) na Mahakama ya Rufani ya Tanganyika.
5. Mahakama ya Rufani ya Tanganyika itakuwa ndio Mahakama ya mwisho ya rufaa kwa kesi zote zinazoanzia Mahakama za Mahakimu na Mahakama Kuu ya Tanganyika, isipokuwa kwa kesi zinazohusu mambo ya Muungano na kesi zote ambazo adhabu yake ni kifungo cha maisha au adhabu wa kifo.
6. Majaji wote wa Mahakama Kuu ya Tanganyika na Mahakama ya Rufani ya Tanganyika watateuliwa kwa utaratibu kwamba:
(a) Mtu yeyote mwenye sifa za kushika madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu au Jaji wa Mahakama ya Rufani atatakiwa kuomba kuteuliwa Jaji kwa Tume huru ya Utumishi wa Mahakama;
(b) Baada ya kupokea maombi, Tume huru Utumishi wa Mahakama itafanya usaili na kuchuja Waombaji wenye sifa stahili kwa kutumia utaratibu wa wazi na kisha itapeleka majina ya Waombaji wenye sifa kwa Rais wa Tanganyika kwa ajili ya uteuzi;
(c) Baada ya Rais wa Tanganyika kufanya uteuzi wa majaji wenye sifa kutokana na mapendekezo ya Tume huru ya Utumishi wa Mahakama, majina ya majaji walioteuliwa yatapelekwa kwenye Bunge la Tanganyika kwa ajili ya kupitishwa kwa utaratibu wa wazi wa kusikiliza maoni ya wadau (confirmation hearings);
(d) Mtu yeyote aliyeteuliwa Jaji wa Mahakama ya Tanganyika hatashika madaraka ya Jaji wa Mahakama ya Tanganyika hadi kwanza uteuzi wake utakapothibitishwa na Bunge la Tanganyika.
7. Umri wa Jaji wa Mahakama ya Tanganyika kustaafu kwa lazima itakuwa ni miaka sabini lakini Jaji ataweza kustaafu kwa hiari atakapofikisha miaka sitini na tano. Jaji wa Mahakama ya Tanganyika hataweza kuongezewa muda wa kuendelea kushikilia madaraka ya Jaji baada ya kufikisha muda wa kustaafu kwa lazima.
8. Kutakuwa na Tume huru ya Utumishi wa Mahakama ya Tanganyika ambayo wajumbe wake watakuwa wafuatao:
(a) Jaji Mkuu wa Tanganyika ambaye atakuwa Mwenyekiti;
(b) Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanganyika;
(c) Mtu aliyepata kushika madaraka ya Jaji Mkuu wa Tanganyika;
(d) Mtu aliyepata kushika madaraka ya Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanganyika;
(e) Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika;
(f) Mtu anayeshikilia madaraka ya Mkuu wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu kinachotoa shahada za sheria zinazotambuliwa na mamlaka ya ithibati ya Tanganyika;
(g) Rais au Mwenyekiti wa Chama cha Majaji wa Tanganyika;
(h) Wajumbe wengine wawili Watakaoteuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watu wanaofahamika kutokana na utaalamu wao katika masuala ya kisheria na watakaothibitishwa na Bunge.
I. MFUMO WA UCHAGUZI KATIKA JAMHURI YA MUUNGANO
Mfumo wa uchaguzi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utafuata misingi ifuatayo:
1. Kila raia wa Jamhuri ya Muungano aliyetimiza umri wa miaka kumi na nane atakuwa na haki ya kupiga kura na kugombea nafasi yoyote ya uongozi wa kuchaguliwa katika Jamhuri ya Muungano.
2. Haki ya kupiga kura na kugombea kuchaguliwa katika nafasi yoyote ya uongozi haitafungwa na masharti yoyote yanayohusu uanachama wa chama cha siasa au mahali pa kuzaliwa kwa mgombea husika.
3. Mamlaka husika zitaweka utaratibu wa kisheria wa kuwawezesha watu wenye haki ya kupiga kura lakini wanaishi nje ya Jamhuri ya Muungano au walioko chini ya usimamizi wa vyombo vya kurekebisha tabia za wahalifu kutimiza haki yao ya kupiga kura.
4. Chaguzi zote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zitafanyika chini ya usimamizi wa Tume huru ya Uchaguzi ya Tanganyika na Tume ya Uchaguzi Zanzibar.
5. Tume huru ya Uchaguzi ya Tanganyika itakuwa na Wajumbe wafuatao:
(a) Wajumbe kumi na tano watakaopendekezwa na vyama vya siasa vyenye uwakilishi katika Bunge la Tanganyika kwa kufuata uwiano wa Wabunge katika Bunge;
(b) Wajumbe watatu watakaopendekezwa na vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu lakini ambavyo havina uwakilishi katika Bunge la Tanganyika;
(c) Mjumbe mmoja atakayependekezwa na Chama cha Mawakili wa Tanganyika;
(d) Mjumbe mmoja atakayependekezwa na taasisi zisizokuwa za kiserikali;
(e) Mjumbe mmoja atakayependekezwa na vyama vya kitaaluma vya taasisi za elimu ya juu zinazotambuliwa na mamlaka ya ithibati ya Tanganyika;
(f) Wajumbe wawili watakaopendekezwa na taasisi za kidini;
(g) Wajumbe wawili watakaopendekezwa na Tume huru ya Utumishi wa Mahakama ambao watakuwa majaji wastaafu wa Mahakama ya Rufani ya Tanganyika.
6. Wajumbe wa Tume huru ya Uchaguzi watachagua Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume kutoka miongoni mwao, ili mradi Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti watakuwa ni watu wenye sifa ya kushikilia madaraka ya Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanganyika.
7. Wajumbe wa Tume huru ya Uchaguzi hawatashikilia madaraka ya Mjumbe wa Tume kabla uteuzi wao haujathibitishwa na Bunge la Tanganyika.
8. Tume huru ya Uchaguzi itakuwa na mamlaka ya kuteua mtu yeyote mwenye sifa kuna Mkurugenzi wa Uchaguzi na Mtendaji Mkuu wa Tume.
9. Tume huru ya Uchaguzi itakuwa na mamlaka ya kuteua watendaji wake yenyewe katika ngazi zote kuanzia ngazi ya taifa, Jimbo, Wilaya na katika Majimbo ya uchaguzi. Wasimamizi wa uchaguzi katika ngazi ya majimbo, majimbo ya uchaguzi na wilaya watakuwa ni watumishi wa Tume huru ya Uchaguzi wakati wasimamizi wasaidizi na wasimamizi wa vituo watakuwa watu walioteuliwa na Tume kwa utaratibu wa wazi na kwa vyovyote vile hawatakuwa watu walioko katika Utumishi wa umma;
J. ULINZI WA HAKI ZA BINADAMU KATIKA JAMHURI YA MUUNGANO
1. Katiba itatambua na kulinda haki na uhuru muhimu wa binadamu zinazotambulika Kama haki za binadamu za kizazi cha kwanza, yaani haki zote zilizoainishwa katika Sehemu ya Tatu ya Sura ya Kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, na zile zilizoainishwa katika mikataba mbali mbali ya kimataifa ya haki za binadamu.
2. Katiba itatambua na kulinda haki zote za binadamu zinazotambulika Kama haki za kizazi cha pili za binadamu kama zilivyoainishwa katika ibara ya 11 ya Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano, na zilizoainishwa katika mikataba mbali mbali ya kimataifa inayohusu haki za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. Haki hizo ni pamoja na:
(a) Haki ya Mtu kufanya kazi;
(b) Haki ya kupata elimu;
(c) Haki ya kupata msaada kutoka kwa jamii wakati wa uzee, maradhi au hali ya ulemavu na katika hali nyinginezo za mtu kuwa hajiwezi.
3. Katiba itatambua kwamba Wananchi ndio wamiliki wa rasilimali asilia za maeneo wanakoishi Kama vile ardhi, madini, mafuta, gesi asilia, misitu/wanyama pori na rasilimali uvuvi na kwamba jukumu la Serikali ni kuwezesha Wananchi wa maeneo husika kunufaika na umilikaji huo wa rasilimali asilia.
4. Wananchi hawatanyang'anywa rasilimali zao asilia na mamlaka za Serikali matumizi na watu au taasisi nyingine ya rasilimali asilia za Wananchi bila kwanza Wananchi watakaoathiriwa na unyang'anyi au matumizi hayo kutoa ridhaa yao baada ya kupatiwa taarifa zote na kamili zinazohusu matumizi yanayotarajiwa ya rasilimali hizo na athari za matumizi hayo kwa mazingira, kiuchumi na kijamii (the right of prior informed consent).
5. Wananchi, Kama wamiliki wa msingi wa rasilimali asilia, watakuwa na haki ya kulipwa mrahaba kwa ajili ya matumizi ya watu au taasisi nyingine ya rasilimali asilia za Wananchi, wakati mamlaka za Serikali za mitaa, Majimbo na Serikali Kuu zitakuwa na haki ya kutoza kodi mapato yatakayotokana na matumizi ya rasilimali hizo.
6. Haki za binadamu zilizotambuliwa na Katiba hazitawekewa vizingiti au kuminywa kwa kutumia sheria za kawaida za Bunge au vizingiti vilivyowekwa na Katiba yenyewe (clawback/derogation clauses) ambavyo havilingani na misingi inayokubalika ya kimataifa inayohusu haki za binadamu.
Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO