Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Sakata la Gesi Mtwara: James Mbatia afungiwa ndani ya ofisi asidhuriwe na wananchi wenye hasira

Mbunge wa Kuteuliwa na Rais ambae pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Mh James Mbatia  anaelezwa kuwa ndani ya ofisi hii ya chama chake Mjini Mtwara jana jioni chini ya ulinzi wa Polisi huku umati wa watu wakiwa nje na kuomba ajitokeze aowambe radhi kwa kile walichodai wanaamini alitumwa kuwalaghai kwa kauli alizozitoa hiyo jana jukwaani.  (Picha hii na maelezo yake ni kwa mujibu wa Alexander Naveta)

Mwenyekiti wa NCCR Mgaeuzi, Mh James Mbatia

MWENYEKITI wa NCCR Mageuzi, James Mbatia jana alijikuta katika wakati mgumu baada ya kulazimika kufungiwa katika ofisi ya NCCR-Mageuzi wilaya ya Mtwara Mjini kutokana na baadhi wa wananchi walioudhuria mkutano wake wa hadhara uliofanyika uwanja wa Mashujaa, kutaka kumdhuru kwa madai kwamba hawakuridhishwa na hotuba yake.

Mbatia alianza kurushiwa chupa tupu za maji alipokuwa akitoka uwanjani hapo baada ya kukatisha hotuba yake kutokana na baadhi ya wananchi kupinga kauli zake kwa madai hawamuelewi.

Kauli inayodaiwa kumgharimu Mbatia ni ile ya ‘Iwapo gesi itatoka Mtwara’ ndipo wananchi hao walipoanza kupaza sauti wakisema “Hatukuelewi…hatukuelewi” hata hivyo Mbatia aliendelea kuhutubia hali iliyosababisha wananchi hao wapaze sauti zao kwa kuimba nyimbo.

“Haitoki… Hatoki…Haitoki…” sauti za wananchi zilisikika na hata Mbatia alipojaribu kuwatuliza wananchi hao kwa kusema ‘gesi kwanza…. Gesi kwanza” baadhi waliitikia na wengine waliendelea kusema hawamuelewi.

Hali hiyo ilimlazimisha Mbatia kukatisha hotuba yake saa 11.25 jioni na aliondoka uwanjani hapo kwa kutembea kwa miguu hali iliyotoa mwanya kwa wananchi kumrushia chupa tupu za maji. Mwenyekiti huyo akiwa ameambatana na wabunge wa chama hicho, Moses Machali (Kasulu Mjini) na Agripina Buyogela (Kasulu Vijijini) mkoani Kigoma, walielekea kituo cha polisi kilichopi karibu na uwanja huo na baadaye alielekea ofisi za NCCR Mageuzi wilaya.

Alipotafutwa jana kuzungumzia suala hilo, Mbatia hakupatikana kupitia simu zake zote za mkononi hata wabunge Buyogela na Machali pia simu zao zilikuwa zimefungwa.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara, Mary Nzuki alisema hakuwa na taarifa za Mbatia kunusurika kupigwa ila aliahidi kufuatilia suala hilo. “Ninachojua Mbatia yuko hapa kweli na amefanya mkutano wake, baada ya mkutano ule akiwa anatoka eneo la mkutano alikuwa anasindikizwa na wafuasi wake ambao walikuwa wanamshangilia. Sasa kama walipofika huko mbele walimgeuka hilo sijui”, alisema Nzuki.

Pinda afunguka

Wakati huohuo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amewasihi wakazi wa mikoa ya Kusini kuwa wavumilivu na kuruhusu mradi wa kusafirisha gesi kutoka mikoa hiyo kwenda Dar es Salaam ufanikiwe kwa kuwa una faida kubwa kwao.

Pinda alitaja manufaa hayo kuwa ni pamoja na ajira kwa vijana watakaoshiriki katika ujenzi huo, ujenzi wa viwanda na miundombinu na upanuzi wa Bandari ya Mtwara.

“Nilishangaa kuona wananchi wa Mtwara wanaandamana kupinga ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka huko kwenda Dar es Salaam. Mradi huo ndiyo utakuwa suluhisho la tatizo la umeme nchini, ”alisema Pinda na kuongeza:

“Wananchi wa Mtwara wawe wavumilivu, watanufaika sana na mradi huo. Mradi utajumuisha upanuzi wa Bandari ya Mtwara pamoja na ujenzi wa Viwanda mbalimbali vitakavyosaidia kukuza uchumi wa maeneo yao kwa kutoa ajira na kukuza biashara zao.”

Waziri Mkuu Pinda alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, alipokuwa akijibu maswali ya waandishi waliotaka kufahamu hatima ya mgogoro huo.

Alijibu maswali hayo baada ya kuzindua Makao Makuu ya Biashara ya Kampuni ya Vifaa vya Umeme ya Beko Grundig kutoka Uturuki inayofanya kazi zake nchini kwa kushirikiana na mwekezaji mzawa, Modern Holdings East Africa Ltd.

Pinda alisema pamoja na kwamba gesi asilia inayopatikana Mtwara ni mali ya Watanzania wote, wakazi wa mkoa huo hawapaswi kuwa na wasiwasi na mradi huo, kwani utawanufaisha kwa kiasi kikubwa kinyume na wanadhani.

Kauli hiyo ya Waziri Pinda inaungana na ile aliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete wakati wa salamu za mwisho wa mwaka jana ambapo alisisitiza kuwa mradi huo utawapa faida nyingi wakazi wa Mtwara na Watanzania wote.

Kauli za viongozi hao zilikuja baada ya wakazi wa Mtwara kuandamana wakipinga gesi asilia kusafirishwa kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam kwa maelezo kwamba kitendo hicho kitawafanya wasifaidike.

Waziri Pinda alisema kukamilika kwa mradi huo wa gesi kutasaidia kutatua tatizo la umeme nchini na kwamba ifikapo 2015 tatizo hilo litageuka historia, hali itakayochochea kasi ya uwekezaji nchini.

Aliongeza kuwa mbali na mradi huo wa gesi asilia, Serikali inaendelea kuboresha miradi mingine ya kuzalisha umeme ukiwamo ule wa makaa ya mawe uliopo Kiwira mkoani Mbeya.

Aliwataka wafanyabiashara wazawa kupanua wigo wa biashara zao kwa kuwekeza nje ya nchi zikiwemo nchi za bara la Ulaya kama Uturuki ili kuongeza ushindani wa biashara za kimataifa.

Naye Balozi wa Uturuki nchini Ali Davutogh alisema ongezeko la wawekezaji kutoka nchini kwake litakuza uhusiano wa kiuchumi baina ya nchi hizo mbili pamoja na kuongeza ajira, teknolojia na kukuza sekta ya viwanda nchini

Chanzo: MGAGANI HABARI.COM

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO