Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Wassira atajwa vurugu za Chadema

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira, ametajwa kwamba anaongoza mtandao wa kukivuruga Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kupitia Baraza la Vijana la Chama hicho (BAVICHA).

Wassira ametajwa jana na Mwenyekiti wa BAVICHA, John Heche, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya CHADEMA, Kinondoni Dar es Salaam.

Chini ya mkakati huo, Heche alisema Wassira amekuwa akishirikiana na Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA aliyevuliwa uanachama, Juliana Shonza.

Kutokana na hali hiyo, amesema mtandao huo ambao umekuwa ukifadhiliwa na waziri huyo, utavunjwa kwa sababu wameshaufahamu.

Aliwataja wanachama wengine waliokuwa wakishirikiana na Shonza ili kuhakikisha wanaibomoa BAVICHA kuwa, ni wajumbe wa baraza hilo, Habib Mchange, Mtela Mwampamba, Joseph Kasambala na Ben Saanane.

Heche alisema Shonza kwa kutumia nafasi yake, alikuwa akishirikiana na baadhi ya watu kulisaliti baraza hilo kwa kuwatumia vijana wapenda mabadiliko.

“Katika kikao cha mkutano mkuu wa baraza hivi karibuni, tulijadili masuala mbalimbali ikiwamo tuhuma dhidi ya Shonza na alikutwa na makosa zaidi ya sita, ikiwamo kufanya mikutano na vikao vya siri kwa manufaa ya CCM.

“Shonza anadaiwa kukusanya vijana ambao ni wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali waliosimamishwa masomo au kufukuzwa vyuoni na kuwalaghai ili wakichafue chama na viongozi wa ngazi za juu.

“Shonza alifanya kazi hiyo kwa ushawishi wa hongo, ili vijana wakubali kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kutoa matamko machafu dhidi ya CHADEMA na viongozi wakuu akiwamo Katibu Mkuu, Dk. Wilbrod Slaa na Mwenyekiti wetu Freeman Mbowe.

“Katika hili tuna mfano hai ambapo katika kikao kilichofanyika katika Baa ya Highland Makumbusho kuanzia saa 9 hadi 11 jioni, aliwaita wanafunzi ambao ni viongozi wa CHASO (Umoja wa Wanavyuo wa Chadema), ambapo aliwashawishi wafanye mkutano na waandishi wa habari na kuisema vibaya Chadema.

“Desemba 6, mwaka jana, alifanya kikao kingine katika Hoteli ya MIC, hapa hapa Dar es Salaam, kuanzia saa 10 hadi saa 12 jioni kwa ajili ya kupanga njama za kukichafua chama na kutukana viongozi kwa manufaa ya CCM.

“Pia amekuwa akikutana na kufanya vikao vya siri na wenzake kupanga njama za kufanya hujuma dhidi ya CHADEMA na pia amekuwa akishiriki vikao vya kuanzisha chama kipya kinachoitwa CHAUMMA, amekuwa akishiriki katika makundi yaitwayo MASALIA na PM7 ambayo yote yalikuwa na lengo la kuvuruga chama na wanachama.

“BAVICHA imejiridhisha bila shaka, kwamba Shonza haendani na Katiba, falsafa, sera na maadili ya chama makini na tumaini la watu, CHADEMA.

Shonza ajibu mapigo

Akizungumzia uhusiano wake na Wassira, alisema hana mawasiliano yoyote na waziri huyo na kwamba hajawahi kukutana naye zaidi ya kumsoma na kupitia vyombo vya habari.

Pamoja na hayo, alisema atawasiliana na mwanasheria wake ili achambue kwa kina hatua alizochukuliwa na BAVICHA kisha atajua cha kufanya.

Wassira awashangaa Chadema

Naye, Wassira akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana kuhusiana na tuhuma dhidi yake, alikanusha madai hayo na kusema sasa Chadema kimepoteza mwelekeo.

“Hao ni waongo na nimeshawazoea kwa tabia yao ya kunisingizia pale wanapopata misukosuko, kwanza wanapoteza muda kunifikiria wakati wao wenyewe wamepoteza mwelekeo,” alisema Wassira.

Shibuda atema nyongo

Kwa upande wake, Mbunge wa Maswa Magharibi John Shibuda (CHADEMA), amejibu mapigo dhidi ya BAVICHA na kusema kuwa yeye ni jenerali wa kisiasa na kwamba vita iliyoanzishwa dhidi yake ataishinda bila kikwazo.

Alisema kwamba, pamoja na hatua hiyo ya kuhusishwa na vurugu za jumuiya hiyo hataweza kuyumba, badala yake atazidi kusonga mbele.

Shibuda aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu akiwa visiwani Zanzibar.

“Tuhuma walizozitoa dhidi yangu, nimezisoma katika vyombo vya habari na hiki walichokifanya hawa viongozi wa BAVICHA ni wazi wana lengo la kutaka kuchafua jina langu mbele ya jamii.

“BAVICHA walitakiwa kutumia busara na hekima katika kufanya uamuzi wowote, kwa ajili ya kujenga chama kwa kuwa wao ni mawazo mapya ya matumani mbadala, lakini sasa wamegeuka kuwa watu ambao wanatoa uamuzi wenye kukosa heshima kwa wakubwa zao.

“Kwanza nitatumia mwanasheria kupitia tuhuma zilizotolewa na viongozi wa BAVICHA, ili kuweza kuchambua hoja hizo kisheria na wakimaliza kazi hiyo nitazichukua na kuziwasilisha kwenye chama ili waweze kuzifanyia kazi na baadaye nitajua la kufanya,” alisema Shibuda.

CHANZO: MTANZANIA 8 JANUARI 2013

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO