Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Ijue Sera ya Majimbo ya CHADEMA Inavyofafanuliwa Katika Andiko la Mh John Mnyika

 

Mwaka 2007 miaka miwili baada ya uchaguzi wa mwaka 2005 palijitokeza mjadala kuhusu sera ya majimbo. Mwaka 2012 ikiwa ni miaka miwili tena toka uchaguzi wa mwaka 2010 pameibuka kwa mara nyingine mjadala kuhusu sera ya majimbo kufuatia maandamano ya wananchi wa Mtwara juu ya madai ya gesi. Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospter Muhongo amenukuliwa na gazeti moja tarehe 29 Disemba 2012 akiponda sera ya majimbo ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwa ni mbovu na haitumiki kokote duniani; kauli ambayo haina ukweli kama nitavyoeleza katika makala hii.  Amedai madai ya rasilimali za wananchi wa eneo hayana msingi na kuwaita wote wenye kujenga hoja hiyo kuwa wanataka kuigawa nchi vipande vipande, majibu ambayo ni mwendelezo wa propaganda chafu.

Prof. Muhongo badala ya kujibu hoja za waandamanaji na wananchi wa Mtwara ameamua kuibua ‘vioja’ vya kuishambulia CHADEMA na sera yake ya majimbo. Wakati hata kwa sera za CCM na serikali ya sasa, maandamano ya wananchi wa Mtwara kutaka majibu toka  kuhusu manufaa ya miradi ya gesi  asili inayotoka katika maeneo yao ni matokeo ya madai ya ufisadi wa baadhi ya viongozi na udhaifu wa Serikali katika kuushirikisha umma katika michakato ya maamuzi ya  kisera na kitaasisi kuhusu rasilimali na miradi muhimu ya maendeleo. Aidha, ni matokeo pia Bunge kutokuisimamia kikamilifu Serikali kwa niaba ya wananchi kwa mujibu wa ibara ya 63 ya katiba wakati serikali inapoacha kufafanua masuala yanayohojiwa na wabunge na inapokwepa kutekeleza maazimio ya Bunge kuhusu sekta ya nishati ikiwemo sekta ndogo ya gesi asili.

Nashauri Rais Jakaya Kikwete apuuze majibu ya Prof. Muhongo na  atumie hotuba yake kwa taifa ya mwishoni mwezi huu wa Disemba 2012 kueleza kwa umma undani wa miradi husika ya gesi asili  na manufaa yake kwa wananchi wa

maeneo tajwa na nchi kwa ujumla; hatua ambayo alipaswa kuifanya tarehe 8 Novemba 2012 wakati wa uzinduzi wa mradi husika.

Nikirudi kwenye madai potofu ya Prof. Muhongo kuwa sera ya majimbo ni mbovu, haitumiki kokote duniani na itaigawa nchi vipande vipande, nirejee majibu yangu ya mwaka 2007 kwa wasome na wanasiasa wenye mtizamo kama wake. Nikumbushe tu kwamba madai potofu kama hayo yalishika kasi sana wakati wa uchaguzi mkuu 2005 kwa vijembe vya majukwaani. Hoja kuu ya kufahamu ni kwamba chimbuko la sera ya majimbo nchini ni falsafa ya CHADEMA ya nguvu ya umma. Kwani umma ndio unapaswa kuwa na mamlaka lakini pia umma ndio unapaswa kunufaika na rasilimali za nchi. Falsafa hii imeelezwa vizuri katika ibara ya 3 ya katiba ya CHADEMA ambayo nashauri Prof. Muhongo na wote wenye mtizamo kama wake waisome na kuielewa.

Niweke pia bayana kwamba katika chaguzi zote zilizopita CHADEMA haikuwa na ajenda ya majimbo kama ajenda inayosimama peke yake. Ilikuwa ni sehemu ya ajenda nyingine. Tulisema wazi kwamba tatizo la CCM ni kuwa huwa inakuja na ilani ya kuahidi kila kitu na hatimaye kutofanya chochote. Sisi tulisema mwaka 2005 kwamba pamoja na kuwa na sera nyingi lakini tutakuwa na vipaumbele vichache: wakati huo kipaumbele cha kwanza kilikuwa Mfumo Mpya wa Utawala. Mwaka 2010; kipaumbele cha kwanza kilikuwa fursa kwa kila mtoto wa kitanzania kupata elimu bora. Cha pili, fursa kwa kila mtanzania kupata huduma bora za kijamii. Cha tatu, kujenga kilimo bora na cha kisasa. Cha nne, fursa kwa kila mtanzania kujenga na kumilki uchumi imara na shirikishi. Kipaumbele cha tano kikiwa kujenga uongozi bora na mfumo mpya wa utawala.

Mwaka 2005, kwenye kipaumbele hicho cha MFUMO MPYA WA UTAWALA: tulikuwa na masuala matatu- Kwanza, Uongozi mpya kwa maana ya wananchi kuwaondoa viongozi walioko madarakani kwa maana wameshiriki ufisadi wa nyuma hivyo hawawezi kufanya mabadiliko yoyote ya maana; Pili; kusafisha mfumo wa utawala kwa maana ya kupambana na rushwa na ufisadi na Tatu; kutengeneza muundo mpya wa utawala ikiwemo kuanzisha muundo wa majimbo. Lakini kwa kuwa suala la majimbo lilipata ladha zaidi na mashambulizi mengi SERA/AJENDA MAMA ya MFUMO MPYA WA UTAWALA ikafunikwa kabisa. Sina nia ya kujadili katika makala ya leo kwa nini hali hii ilijitokeza wakati huo.

Mwaka 2010 tuliweka mkazo katika kunadi sera zenye kuhimiza mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili ya dola yaani serikali, bunge na mahakama. Kushughulikia mzigo mkubwa wa gharama za kozi za wananchi kutokana na ukubwa wa serikali kuu na mianya ya ufisadi. Kujikita katika kujenga taasisi na misingi ya uwajibikaji. Na katika muktadha huo, CHADEMA ikatangaza sera ya kuanzisha mchakato wa katiba mpya ndani ya siku 100 iwapo ingepewa ridhaa ya kuongoza nchi. Hata baada ya matokeo tata ya uchaguzi 2010, tulisusia hotuba ya Rais Kikwete ya kufungua bunge kwa kuwa nchi haikuwa na mfumo wa kikatiba wa kupinga matokeo ya urais mahakamani na tukataka mchakato wa katiba mpya uanzishwe; hatimaye umeanza.

Kwa hiyo katika mchakato huu wa katiba mpya, misingi ya sera ya mfumo mpya wa utawala inajitokeza kwenye maoni ya baadhi ya wananchi. Kwa kuwa Prof. Muhongo na wengine  wamezoea kutumia jina “Sera ya Majimbo”, bada ya ‘sera ya mfumo mpya wa utawala’ nami katika mjadala huu nitatumia jina hili ili twende vizuri kwa pamoja.

Suala la sera ya majimbo ni suala la kikatiba. Chama chochote cha siasa kinauza kwa wananchi matakwa yake kama kikipewa ridhaa na wananchi; matakwa hayo yanaweza kutokana na misingi ya chama husika ama matakwa wa wananchi ama matakwa ya viongozi wa chama husika. Lakini baada ya uchaguzi zipo sera ambazo utekelezaji wake lazima urudi tena kwa wananchi kupata ridhaa ya pamoja mathalani CCM wamejikuta suala la mahamakama ya kadhi linapaswa kurudi kwa wananchi ingawa lilikuwa katika ilani ya chama chao ya mwaka 2005. Lakini mambo mengi chama hutekeleza kwa kwenda kwa wawakilishi wa wananchi yaani bunge. Kadhalika, suala la kuunda kwa majimbo ni suala la mabadiliko ya katiba hivyo kwa vyovyote vile CHADEMA ingepaswa kurudi kwa wananchi. Hata ndani ya chama kwenyewe; misingi ya sera ilikubaliwa kwa pamoja lakini tafsiri ya kina katika chaguzi zilizopita kila mtu alikuwa anaifanya kwa mujibu wa mahali. Ni kawaida ya sera na ilani kutoa matamko ya ujumla, maelezo zaidi yanakuwa katika mikakati, programu ya utekelezaji na shughuli mbalimbali.

Madai ya Prof. Muhongo kwamba sera ya majimbo haitumiki kokote duniani si sahihi. Suala la sera ya majimbo sio geni duniani. Nchi kadhaa za Afrika zinafuata mfumo huu mathalani Afrika ya Kusini, Ethiopia nk. Ulaya nchi nyingi zinafuata mfumo huu. Marekani ya Kaskazini, Australia . Kwa kweli dunia kwa ujumla wake inatambua umuhimu wa majimbo. Wengine wamekuwa na majimbo kutokana tofauti za kimbari/kinasaba(ethnic federalism); wengine ni sababu tu za kurahisisha utendaji(functional federalism) na wengine ni umbali tu wa kiographia(geographical federalism). Kwa hiyo wote wanachambuia majimbo ni vyema  wakachambua pia ufiderali unafanyaje kazi katika nchi hizi. Faida na hasara zake. Hata katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ukiangalia hata muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni aina ya ufiderali ingawa ni ufiderali tenge, ndio maana wengine tunataka serikali ya shirikisho!.

Madai yake mengine potofu ni ya kuwa sera ya majimbo ni mbovu na kwamba itaigawa nchi vipande vipande. Prof. Muhongo aisome misingi ya Sera ya majimbo ya CHADEMA na kuangalia ni vipi ni sehemu ya falsafa ya nguvu ya umma na kwa vipi inaendana na misingi ya CHADEMA, kwa vipi inaweza kusaidia utekelezaji wa sera za CHADEMA na kwa ujumla ni namna gani ni silaha ya nyongeza katika kukabiliana na ujinga, umaskini na maradhi na hatimaye kuleta maendeleo ya nchi na wananchi.

Kwa mtazamo wangu, hii ni misingi ya “Sera ya Majimbo” ambayo inadhihirisha kwamba sera hii ni bora na inalenga kuiunganisha nchi kinyume na madai potofu ya Prof. Muhongo na wengine.

Msingi wa kwanza ni kujenga uwezo wa kisiasa,uongozi na uwajibikaji. Sera ya majimbo inaelekeza taifa kuwa na viongozi wa kuchaguliwa moja kwa moja na wananchi katika ngazi mbalimbali. Hii ina maanisha kwamba kwa muktadha wa sera ya majimbo ofisi na vyeo vya mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya, katibu tarafa vitafutwa. Hawa uzoefu unaanyesha kwamba wamekuwa wakiongeza mzigo wa gharama kutokana na mwingiliano kati yao na wakurugenzi mathalani wa halmashauri ambao ni waatalamu wanaofanya kazi chini ya viongozi wa kuchaguliwa. Uzoefu unaonyesha kwamba kwa kuwa mikono ya mhimili wa serikali ngazi ya chini viongozi hawa wamekuwa sababu ya serikali kuu kuingilia serikali zingine na kimaamuzi na kimwelekeo.

Matokeo yake ni kuwa nchi nzima inaendeshwa na ikulu Dar es salaam hata katika mambo ya kawaida kabisa. Urasimu huu umekuwa kikwazo cha maendeleo. Nguvu ambayo viongozi hawa wamepewa toka wakati wa muundo wa kikoloni wa kutawala kwa kutumia mawakala umewafanya wawe miungu watu na wanyanyasaji.

Ndio maana katika maandamano ya wananchi wa Mtwara kati ya madai yao ni pamoja na kumwomba Rais Jakaya Kikwete awaondolee mkuu wa mkoa Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia kutokana na lugha aliyotumia dhidi yao. Majibu ya mkuu wa Mkoa madai hayo ya wananchi kama alivyonukuliwa na chombo kimoja cha habari tarehe 29 Disemba 2012 ni kwamba ‘niliwasamehe kuwaita wananchi hao wapuuzi, nilipaswa kuwaita wahaini’. Kwa kifupi ni viongozi wa namna hiyo wakuteuliwa  hawahitajiki. Pamoja na kuondoa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, Sera ya majimbo inataka mameya wachaguliwe na wananchi moja kwa moja badala ya mabaraza ya madiwani ili kuongeza uwajibikaji. Kwa kifupi, msingi huu wa sera unachochea hamasa ya uongozi na kuweka viongozi wenye kuwajibika kwa watu. Hii ndiyo falsafa ya nguvu ya umma katika vitendo.

Msingi wa pili ni kushusha na kugawanya madaraka(devolving and separation of powers). Kwamba uzoefu unaonyesha kuwa majimbo yanapopewa madaraka nayo yanatoa madaraka kwa ngazi ya chini yake na kuendelea mpaka chini kabisa. Serikali kuu inapohodhi mamlaka kadhalika ngazi za chini zinahodhi mamlaka ya ngazi za chini. Hoja inatolewa kwamba je kwa nini njia isingekuwa serikali huru za mitaa? Hiyo ni njia moja lakini mamlaka(mandate) ya serikali ya mtaa huwa katika maeneo machache tena ya utekelezaji zaidi tofauti na mfumo wa majimbo. Mfumo wa majimbo unahusisha ni masuala gani ambayo majimbo inaweza kuyashughulikia moja kwa moja kama ambavyo masuala yanavyogawanywa kwa misingi ya yale ya muungano na yasiyo ya muungano. Lengo ni kuifanya serikali ya fideresheni ishughulike na mambo machache na kila eneo lisimamie mambo yake kwa mujibu wa mazingira ya maeneo husika. Hii ndio nguvu ya umma! Kwa msingi huu, ushiriki na ushirikishwaji wa wananchi katika mipango na miradi ya maendeleo ungekuwa mpana; hivyo maandamano na madai ya wananchi kama ilivyotokea kwenye Mtwara kuhusu gesi na maeneo mengine ya nchi kuhusu rasilimali zingine ikiwemo ardhi, madini, misitu, maji nk yasingekuwa masuala yanayojirudia rudia mara kwa mara.

Msingi wa tatu ni kupanua umoja na mshikamano miongoni mwa watanzania na kuvunja dhana ya ukabila. Mfumo wa sasa wa kugawa wilaya pamoja na sababu zingine zinazotolewa na serikali umekuwa ukilalamikiwa kuwa umejikita katika kugawa wilaya kwa mujibu wa makabila-mfano Rombo ya warombo, Ukurewe ya wakerewe-mifano ni mingi kweli kweli. Huku ndiko kuigawa nchi vipande vipande kama alivyodai Prof. Muhongo ambapo kimsingi kunafanywa na Serikali inayoongozwa na CCM.  Sera ya majimbo inayopigiwa upatu na CHADEMA inalenga kuvunja mshikamano wa kiwilaya na badala yake kutengeneza fungamano la kimajimbo- mathalani jimbo la Kaskazini linaweza likajumuisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga-hii ni jimbo la wamasai, wairaq, wabarabaig, wachaga, wapare, wabondei nk. Jimbo la Ziwa ni mikoa ya Karagwe, Mara, Mwanza nk., hii ina maanisha wasukuma, wahaya, wakurya nk. Lengo ni kutengeneza kizio(unit) kipya cha utambulisho chini ya Taifa(Tanzania) yaani walazi wa Jimbo fulani na kufanya watu wajinasabishe kabisa na majimbo yao. Hii ni kwa sababu majimbo yanakuwa na upekee wake ambao mtu anapenda ‘kujinasabisha’ nao. Mathalani jimbo moja linaweza kuwa na sheria za ajira zenye kuvutia zaidi nk .Hii ndio nguvu ya umma!

Msingi wa nne ni kuweka utamaduni wa ushindani na upekee ndani ya nchi. Kama ambavyo nchi zinavyoshindana ndivyo ambavyo majimbo yenye taratibu tofauti za kibiashara, ajira, uwekezaji, makazi na kadhalika zitakavyoshindana. Serikali ya majimbo inatoa mwanya ya majimbo kujiamulia mwelekeo wake katika masuala fulani fulani. Mathalani jimbo moja linaweza kupiga marufuku uvutaji sigara; majimbo mengine yanaweza kuiga ama yanaweza kutofuata. Hata katika michezo nakadhalika, ushindani utaongezeka maradufu. Kila jimbo litataka kujifananisha na mafanikio fulani fulani. Dhana ya ushindani na upekee imeshindikana katika mazingira ya sasa ambapo kila halmashauri inaongozwa na maelekezo ya Dar es salaam na inajivunia mafanikio ya nchi kwa ujumla wake. Katika kuendeleza dhana hii potofu Prof. Muhongo amejibu tangu wakati wa ukoloni tulikuwa tukiendesha nchi kwa katani na akawataka wananchi wa Mtwara warudishe mapato ya katani. Prof. Muhongo anapaswa kuisoma historia ya Mtwara toka wakati wa ukoloni atagundua kwamba mikoa ya Kusini nayo ilikuwa na nafasi yake katika uchumi na biashara. Huu ni mjadala mwingine, hata hivyo suala la msingi hapa ni umuhimu wa ushindani. Hata binadamu, ukipewa uhuru wa kujiamulia una uwezo wa kufanya vitu vya pekee zaidi kuliko ukiwa sehemu ya mfumo mpana. Hii ni saikolojia ya maendeleo.Hii ndio falsafa ya nguvu ya umma!

Msingi wa sita ni kupanua vyanzo vya mapato. Majimbo yanapopaswa kujitegemea kwa aina fulani moja kwa moja yanapaswa kuanza kutafuta njia za kujitegemea. Hii itasaidia vyanzo vya mapato kupatikana.Hii ni kutokana na kanuni ya mwitu(the law of the jungle). Sasa hivi kila mahali wanaitazama Dar es salaam ikusanye pesa nchi nzima na kutoka kwa wahisani na kila eneo lina achama mdomo kwa ajili ya kupokea! Mwaka 2005 Wapinzani wa hoja hii walitoa hoja kwamba lipo jimbo ambalo halina raslimali na walitolea mfano wa jimbo la kusini. Hawa ni watu ambao pengine walikuwa hawafahamu kwamba Tanzania ina raslimali kila mahali. Wananchi wengi wamekuwa wakilalamika kuwa mikoa ya kusini haina maendeleo. Wakati huo tuliwaeleza ukweli ni kwamba tafiti zinaonyesha mikoa ya kusini ina rasilimali na mali asili nyingi sana tatizo kubwa ni miundo mbinu. Tuliwapa mfano kuwa  Jimbo la Pwani ya Kusini kwa mfano lina mikoa ya Lindi, Mtwara na maeneo mengine yana  rasilimali kama madini, bandari, uvuvi, nishati ya gesi,kilimo cha korosho, mikoko pamoja na utalii. CHADEMA imeendelea kuwaeleza wananchi umuhimu wa mfumo mpya wa utawala kwani kila jimbo lina rasilimali za kutosha ila kwa kuwa serikali ya CCM imekuwa ikiwahadaa wananchi  na kuwafanya wabweteke kisaikolojia ili wasijiletee maendeleo, imekuwa ikipinga vikali serikali ya majimbo.  Baada ugunduzi wa ziada wa gesi, sasa hoja imebadilika kutoka Kusini haina rasilimali; sasa lugha ni kuwa Kusini haipaswi kudai manufaa ya rasilimali hizo kwa kuwa ni za nchi nzima. Hata kama kungekuwa hakuna maliasili: ukweli unabaki kwamba nchi duniani ambazo hazina maliasili lakini zimeneemeka kutokana na kutoa huduma tu! Lakini kwa upande mwingine kama sehemu ya sera ya majimbo lipo pato ambalo litakusanywa serikali kuu na kusaidia katika maeneo ambayo yanamapungufu. Hivyo, Prof. Muhongo atambue kwamba hata katika sera ya majimbo, upo mfumo mpya wa utawala ambao unawezesha rasilimali za nchi kutumika kwa manufaa ya watanzania wote na si watanzania wa eneo fulani pekee ila mfumo huo unahakikisha hata watanzania wa maeneo yenye rasilimali  wananufaika na rasilimali ambazo Mungu amewajalia katika maeneo yao.

Msingi wa saba ni muundo mpya unaosaidia utekelezaji wa majukumu. Hapa ni mjadala wa kipi kinaanza muundo ama majukumu(stucture or function). Sera ya majimbo inachukua mtazamo wa kwamba yote yanakwenda pamoja. Wachambuzi wengi wamekuwa wakitoa hoja kwamba matatizo ya msingi ya mwananchi ni hali mbaya ya maisha, kipato duni, uchumi mbovu, elimu duni nk. Na wanachotaka wananchi ni suluhisho la haya matatizo ya msingi sio ‘porojo’ za sera.

Lakini ukweli ni kuwa kuna uhusiano wa moja kwa moja na kimatokeo baina ya masuala haya(Direct and causality relationship). Kwa mfano, asili ya wananchi wa Geita au Kilwa kuwa na uchumi mbovu ni sera mbovu ya madini au sera ya nishati iliyopitishwa na Dar es salaam lakini pia mfumo mbovu wa mgawanyo wa mapato unaosimamiwa toka Dar es salaam na kwa hulalishwa na sheria na mikataba mibovu. Pengine wananchi wa Geita au Kilwea na Jimbo lao au Kanda yao wanajua zaidi ni ambacho wanataka; sehemu ya tiba ni kuwapa sehemu ya mamlaka ya kujiamulia mambo yao. Wajikaange kwa mafuta yao!.

Tatizo la elimu pengine ni maagizo ya waziri toka Dar es salaam ambaye hajui kabisa hali ya Mwanza ni tofauti na Mtwara. Sasa hata elimu aamue waziri Dar es salaam? Changamoto ya nchi yetu ni wananchi kukosa motisha(motivation) na hisia za umiliki( sense of ownership). Ujinga, Umaskini, Maradhi ni matokeo tu, chanzo ni uongozi. Kuweka uongozi bora ni suala moja. Kushughulikia mfumo na muundo wa uongozi/utawala ni sehemu ya suluhisho.

Upo wasi wasi wa kufanya hivi kwamba kuna kutengeneza matabaka. Hata sasa matabaka katika nchi yetu yapo, tena mabaya zaidi. Maana haya ni ya mtu na mtu. Afadhali utofauti wa kisera kati ya jimbo na jimbo kuliko mtu na jirani yako!. Kuna hofu kwamba yapo majimbo yatakayojitenga. Katika muundo wa Tanzania ya jimbo lenye makabila mbalimbali haliwezi kujitenga ilihali jeshi, mambo ya nje na masuala kadhaa nyeti yako kwenye kapu moja. Huku ni kuhofia kivuli! Huku ni kuyaficha majimbo ambayo ni siri ya maendeleo ya nchi na wananchi.

Msingi wa nane ni kupunguza ukubwa na gharama za uendeshaji wa serikali. Serikali ya majimbo haiongezi ngazi yoyote ya utendaji kwa kuwa inavunja ngazi ya mkoa(ambayo inazidi kuongezwa kila wakati) na kutengeneza ngazi ya jimbo(majimbo ni machache kutegemea na makubaliano ya kikatiba). Wakati huo huo ukubwa wa serikali kuu utapunguzwa kwa kuwa wizara zitabaki chache za mambo ya federesheni mathalani ulinzi, mambo ya nje, fedha. Wizara nyingine zote zinakuwa katika ngazi ya majimbo husika kwa mujibu wa utaratibu wa majimbo husika. Kutokana na ukaribu wa utoaji huduma na utendaji mwishowe gharama za utendaji zitakuwa ndogo kuliko Dar es salaam inavyoendesha nchi mzima katika kila jambo. Mathalani utoaji wa pasi za kusafiria (passport), vibali vya elimu na mambo mengine mengi. Serikali ya majimbo itahakikisha mfumo wa utendaji unatukuwa mdogo kwa kujenga mifumo iliyokaribu zaidi. Hii ndio nguvu ya umma!

Msingi wa tisa ni wananchi kunufaika kutokana na matunda ya raslimali za eneo lao. Mfumo wa sasa ambapo raslimali zote zinamilikiwa na “Dar es salaam” kwa maana ya serikali kuu, unafanya wananchi wasinufaike na raslimali za maeneo yao kikamilifu. Mathalani kodi za madini, mbuga za wanyama nk sehemu kubwa inakuja serikali kuu na ama kugawanywa katika mfumo ambao haunufanishi maeneo husika ama kutumika katika matumizi ya anasa ya serikali kuu. Mathalani pamoja na kuchimba madini yenye thamani Geita ni moja ya wilaya maskini kabisa. Wanaofaidi madini ya Geita wako Dar es salaam. Serikali ya majimbo itakuwa na sehemu ya mamlaka ya ugawanyaji wa mapato yanayotoka katika eneo husika. Pamoja na kukusanya mapato ya pamoja ya serikali kuu. Hii ndio nguvu ya umma          ! Na hapa hoja ya ukabila isiingizwe kwa kuwa watanzania wa maeneo hayo ni watu wa makabila mbalimbali ambao ni wakazi wa maeneo husika.Hali iko hivyo vile vile kwa upande wa gesi asili, ndio maana kabla ya kufafanua kuhusu miradi iliyoanza hivi sasa, Rais na Waziri Muhongo waeleze mapato na manufaa ambayo wananchi wa maeneo husika na nchi kwa ujumla imepata kutoka gesi ilipoanza kuvunwa katika mikoa ya Kusini mwaka 2004 na hatua ambazo Serikali imechukua mpaka dhidi ya madai ya ufisadi wa baadhi ya viongozi katika mapato ya rasilimali hizo muhimu za taifa. Serikali ieleze imefikia wapi katika kurejesha kiasi cha dola milioni 20.1 (zaidi ya Bilioni 30)  zilizopunjwa kifisadi katika mauzo ya gesi asili huku miradi ya maendeleo katika maeneo ambayo gesi hiyo imetoka kama Songosongo na maeneo mengine nchini ikiwa na upungufu wa fedha.

Kwa upande wangu hata baada ya maandamano na mkutano wa wananchi wa Mtwara walioufanya wa tarehe 27 Disemba 2012 na madai potofu ya Prof. Muhongo ya tarehe 29 Disemba 2012;  nitaendelea kutekeleza kusudio langu nililolieleza tarehe 26 Disemba 2012 la kutumia kifungu cha 10 cha Sheria ya ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kutaka nakala ya mkataba wa mkopo wa masharti kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.225 (shilingi trilioni 1.86) kutoka China.

Nitataka pia nakala za mikataba wa mradi wa miundombinu ya gesi asilia ambayo itahusisha ujenzi wa mitambo ya kusafishia gesi asilia katika mikoa ya Lindi na Mtwara na ujenzi wa bomba kuu la kusafirishia gesi asilia la inchi 36 kutoka Mtwara kupitia Lindi, Pwani hadi Dar es Salaam lenye umbali wa kilometa 532.

Hii ni kwa sababu mpaka sasa Wizara ya Nishati na Madini haijatekeleza pendekezo nililowasilisha bungeni tarehe 27 Julai 2012 kwamba kutokana na unyeti wa mradi huo kwa mustakabali wa nchi na maisha ya wananchi wa sasa na baadaye Serikali ilipaswa kuwasilisha bungeni na kuweka wazi kwa umma mkataba wa mradi husika mwa manufaa ya wananchi wote.

John Mnyika

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO