ASKARI wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Arusha PC Samson (20) amefariki dunia akisafirisha mirungi.
Kufariki kwa PC Samson kulitokea juzi katika eneo la Mdori mkoani Manyara baada ya kupata ajali ya gari alilokuwa akilitumia kusafirisha mirungi hiyo kutoka Arusha.
Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya habari eneo hilo la Mdori wilayani Babati zilieleza jana kwamba ajali hiyo ilitokea saa 12:30 asubihi.
Chanzo cha habari kilichoshuhudia tukio hilo kilisema kuwa gari hilo liliacha njia na kuanguka pembeni mwa barabara, hatua iliyosababisha shehena ya mirungi iliyobebwa kumwagika nje.
Wakati taarifa kutoka Mdori zikieleza hayo, mtoa taarifa mwingine kutoka Majengo Kata ya Elerai Arusha alidai kwamba gari hilo lilionekana saa 10 alfajiri likielekea barabara kuu ya Arusha - Babati.
Hata hivyo chanzo hicho kutoka Arusha nacho kilieleza kwamba shehena hiyo ya mirungi ilikuwa mali ya mmoja wa wafanyabiashara wa mirungi jijini hapa (kwa sasa jina linahifadhiwa).
Naye Kamanda wa Polisi Manyara, Akili Mpwapwa alikiri tukio hilo lilitokea saa 12:30 asubuhi eneo la Mdori wilayani Babati.
Alilitaja gari lililotumika kusafirisha mirungi hiyo kuwa ni Toyota Carrina namba T. 588 AUW ambalo linadaiwa kuacha njia na kupinduka kutokana na mwendo kasi.
“Pamoja na kifo cha PC Samson mtu mwingine anayedaiwa kuwa dereva wa gari hilo Hussein Bakari (20-30) ambaye ni mkazi wa Arusha naye alifariki dunia papo hapo.
“Taarifa tulizozipata zinadai kwamba askari huyo alikuwa likizo,” alisema Kamanda Mpwapwa.
Hivi karibuni Jeshi la Polisi mkoani Arusha lilikamata shehena ya mirungi ya thamani ya Sh milioni 40 ikiwa imejazwa kwenye gari ya Canter wilayani Longido.
Iliandikwa Jumamosi, Januari 19, 2013 na Eliya Mbonea wa tanzania Daima, Arusha
0 maoni:
Post a Comment