Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Wananchi waua tena polisi Kagera

KWA mara nyingine Jeshi la Polisi mkoni Kagera, limepata pigo kutokana na askari wake wawili kuuawa kikatili na wananchi wilayani Karagwe wakidhani kuwa ni majambazi na kisha gari lao kuteketezwa kwa moto.

Tukio hilo linakuja zikiwa ni wiki chache tangu wananchi wenye hasira kuua askari wengine wawili wilayani Ngara na kuteketeza kituo cha polisi cha Mugoma mnamo Desemba 15, mwaka jana.

Akizungumza na Tanzania Daima, Kamanda wa Polisi Mkoa Kagera, Phillip Kalangi, alisema tukio hilo lilitokea Januari 6, mwaka huu, saa 2:30 usiku katika kijiji cha Kasheshe, kata ya Rugu, upande wa wilaya ya Karagwe wakati walipofika kijijini hapo kumfuatilia mtu mmoja aliyekuwa na meno ya tembo.

Askari waliouawa ni SGT Thomas Migiro mwenye namba E1446 mwenyeji wa mkoani Mara na Koplo Damas Kisheke mwenye namba E 8889 mkazi wa Kamachumu Muleba mkoani hapa wote wakiwa watumishi wa jeshi hilo kituo cha wilayani Ngara.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, askari walikuwa watatu ila mmoja wao, Bryston aliyekuwa na bunduki alikimbia na kuwaacha wenzake wakisulubishwa.

Habari zaidi zinasema kuwa katika tukio hilo gari la askari Damas aina ya IPSUM lilichomwa moto na wananchi hao.

Askari inasemekana walifika wilayani humo na kufanikiwa kumsaka hadi kumkamata mtuhumiwa aliyekuwa na meno ya tembo saba na kuanza kuondoka eneo la tukio.

Hata hivyo, taarifa zilizolifikia gazeti hili kutoka eneo la tukio zinadai kuwa polisi hao walikuwa na biashara yao binafsi na mmoja wa wananchi wa kijijini hapo, ambaye inasemekana kuwa walitaka kumdhulumu.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa mwananchi huyo aliwapigia simu baadhi ya wanakijiji kuwa akiwataarifu kuwa amevamiwa na majambazi ambao wanaondoka kuelekea Ngara.

Kwamba wakati askari hao wakiwa safarini kurudi Ngara, walikuta mawe na magogo yakiwa yamepangwa barabarani huku wananchi wakiwataka washuke kutoka kwenye gari, amri ambayo waliikataa na hivyo mmoja wao kufyatua risasi iliyomjeruhi mwananchi mmoja.

Majeruhi alitajwa kuwa ni Jovinary Gabanu (35), aliyepigwa risasi katika sehemu ya kiganja cha mkono ambaye amelazwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Nyakahanga.

Hatua hiyo ilizua vurugu na hivyo wananchi kuanza kuwashambulia askari hao hadi kuwaua ingawa muda mfupi baadaye askari wenzao walifika eneo la tukio na kutuliza vurugu.

Baadaye Mkuu wa Wilaya hiyo, Dary Rwegasira, alifika eneo la tukio kuwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi.

Kamanda Kalangi alisema kuwa askari Bryton aliyekimbia alipatikana usiku huo saa tisa na miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali Nyakahanga ikisubiri utaratibu wa kusafirishwa.

Chanzo: Tanzania Daima

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO