MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (CHADEMA) maarufu kwa jina la ‘Sugu’, ameishukuru Kampuni ya Coca Cola kwa kuwachangia sh milioni tano kwa ajili ya kusomesha watoto 360 watakaotoka kila kata katika jimbo lake.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Sugu alisema katika jimbo hilo wameanzisha mfuko wa kusaidia watoto wasiojiweza unaoitwa Mbeya Education Fund ambao kila mdau anayeguswa na elimu ni muhimu kuuchangia bila kujali itikadi ya chama.
“Sisi Mbeya tumeanzisha mfuko wa elimu ambao tumeanza kuchangisha fedha kwa ajili ya kusomesha wanafunzi wasiojiweza ambapo Coca Cola wametusaidia shilingi milioni tano zitakazotuwezesha kuanza na kusomesha watoto 100 ingawa lengo ni 360. Kila kata watatoka wanafunzi 10,” alisema Mbilinyi.
Mbali na kampuni ya Coca Cola, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) imetoa sh milioni mbili, Benki ya CRDB tawi la Mbeya sh 200,000, Mwakikomo Store ya Mwanjelwa sh 150,000, Access Communication wametoa kompyuta moja kwa ajili ya kuanza kufanyia kazi katika ofisi ya mfuko huo.
Mbunge huyo amewashukuru wote waliochangia mfuko huo na kuwataka wadau wengine popote walipo ndani na nje ya Mbeya wawaunge mkono kwa kuchangia kupitia benki ya CRDB tawi la Mwanjelwa, akaunti namba 01J50421214700.
Tanzania Daima, 14 Januari 2013
0 maoni:
Post a Comment