Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limefuta miradi yote ya kuunganisha umeme nchini kutokana na kukabiliwa na ukata

Hayo yalibainishwa bungeni jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, January Makamba, alipokuwa akiwasilisha maoni ya kamati hiyo.

Alisema licha ya shirika hilo kuongeza bei ya umeme kwa asilimia 40.29 mapato ya shirika hilo yameendelea kuwa madogo na hivyo kulazimika kufuta mradi huo.

“Lengo la serikali ni kufikia walau asilimia 30 ya kaya za Watanzania wanaoutumia umeme ifikapo mwaka 2015. Ili kufikia lengo hili ilikadiriwa TANESCO iunganishie wateja wapatao 137,000 kwa mwezi Machi, mwaka huu.

“Kutokana na hali hii haitaweza kuwafikia kwani inashidwa kulipia vifaa vya kutosha na kwa wakati,” alisema.

Aidha alisema kutokana na ukosefu huo wa fedha, shirika hilo linashindwa kufanya ukarabati wa uhakika wa mifumo na miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme na hivyo kuongeza tatizo la upatikanaji wa umeme.

“Shirika kwa sasa linaelemewa na mzigo mkubwa na hali hii ikiendelea shirika litashindwa kutimiza wajibu wake. Kama hii haitarekebishwa haraka, iko hatari ya nchi kuingia kwenye mgao mkubwa wa umeme wakati wa kiangazi,” alisema.

Alieleza kuwa kutokana na hali hiyo, kamati hiyo imependekeza serikali ikamilishe dhamana ya mkopo wa sh bilioni 408 haraka kama ilivyoahidi, ili kulinusuru shirika hilo.

“Pamoja na kutegemea chanzo cha maji ambacho ni bei nafuu, kamati inarudia ushauri kwamba kuanzia sasa iwekeze kwenye vyanzo vingine vya kuzalisha umeme kama gesi, makaa ya mawe, urani, upepo na joto ardhi,” alisema.

Kutokana na tatizo la transfoma nyingi kuungua, alisema kamati hiyo inashauri TANESCO kuhakikisha kuna akiba ya transfoma za kutosha nchini, ili kunapotokea hitilafu kusiwepo na muda mrefu wa kusubiri.

Makamba alisema kutokana na unafuu wa bei ya umeme utakaozalishwa katika mradi wa maji Ruhudji (megawati 358) na Kiwira (megawati 400), kamati imeshauri TANESCO ndiyo iwekeze katika mradi huo kwa kiwango kikubwa kuliko wawekezaji binafsi.

Aidha alisema katika kufanikisha jambo hilo, serikali inapaswa kukopa pesa za kutekeleza mradi huo kwa kuzingatia vipaumbele ilivyojiwekea.

Pamoja na hayo, alisema mpango wa umeme wa dharura haujatekelezwa kwa kasi na kiwango kama kilichoahidiwa na serikali bungeni mwaka jana.

Alisema katika megawati 572 zilizoahidiwa kuzalishwa kati ya Agosti hadi Desemba mwaka jana, ni megawati 342 ndizo zilizozalishwa.

“Aidha fedha sh bilioni 408 ambazo serikali iliahidi kuidhamini TANESCO kukopa kugharamia awamu ya kwanza ya mpango wa dharura, mpaka sasa hazijapatikana,” alisema.

Waziri Nundu na kashfa mpya

Kamati ya Miundombinu, imeeleza kuwa Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu, anakwamisha ujenzi wa gati 13 na 14 katika Mamlaka ya Bandari.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Peter Serukamba, alisema waziri huyo ameingilia suala hilo na kutaka gati hizo kujengwa na mwekezaji binafsi.

“Makubaliano kati ya Waziri wa Uchukuzi na Mwekezaji ambaye ni China Merchants Holdings (Internatinal) Company Limited hayajazingatia maslahi ya mamlaka na taifa,” alisema.

Alisema katika makubaliano hayo, mwekezaji huyo ndiye atakayejenga, kumiliki, kuendesha gati hizo na kuzikabidhi kwa Wizara ya Uchukuzi baada ya miaka 45.

“Makubaliano hayo pia yanasema mwekezaji hatawajibika kwa lolote kutokana na hasara ambayo Wizara ya Uchukuzi itapata kutoka kwa mdau mwingine yeyote kutokana na shughuli zitakazokuwa zinafanywa na mwekezaji huyo,” alisema.

Chanzo: Tanzania Daima, 21 April 2012

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO