Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

CHADEMA kutoa tamko juu ya hukumu ya Lema kesho Jumamosi katika mkutano mkubwa wa hadhara utakaofanyika viwanja vya NMC-Unga Ltd, Arusha

IMGP0810 KUFUATIA Mahakama Kuu kanda ya Arusha kutengua matokeo yaliyompa Ubunge wa Arusha Mjini, Mh Godbless Lema jana asubuhi, chama hicho kimepanga kufanya mkutano wa hadhara kesho Jumamosi April 7 katika uwanja wa NMC Jijini Arusha ili kuwaeleza wananchi nini kinafuata baada ya mtu wao waliyemchagua kuwawakilisha Bungeni kubatilishwa na Mahakama.

Akizungumza na mamia ya wafuasi wa chama hicho waliofurika kwenye eneo la Ngarenaro zilipo ofisi za chama, Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Hai, na Kiongozi Mkuu wa Kambi rasmi ya Upinzania Bungeni, Mh Freeman Mbowe aliwataka wananchi hao wawe wavumilivu ili busara iweze kutumika kuamua jambo hilo, na kuwahidi kesho Jumamosi watataarifiwa nini kinafuata baada ya uamuzi wa Mahakama.

“Nimewasiliana na viongozi wenzangu (wa chama), wanasheria wa chama na wakili aliekuwa anasimamia shauri hili, na kushauriana busara za kulielekeza taifa. Mkutano huu (wa jana ofisini) hauwezi kutengua maamuzi ya Mahakama hata kama ni sawa au si sawa” alisema Mbowe

Akifafanua zaidi baada ya wananchi kupaza sauti wakitaka uchaguzi urudiwe ili wapige kura za hasira, Mh Mbowe aliwataka wawe watulivu na wavumilivu katika kipindi hiki kigumu.

“Tunapaswa kupitia hukumu kwa kina, CHADEMA kama chama makini na shirikishi tunahitaji muda wa kutafakari nini cha kufanya. Jumamosi (kesho) tutakuwa na Mkutano Mkubwa wa hadhara pale NMC na ndipo tutawajulisha maamuzi ya chama kuhusu hatua zinazofuatia.” aleleza Mbowe.

Mbowe alisema kufuatia hukumu hiyo ya Mahakama, Mh Godbless Lema, CHADEMA, na wananchi wa Arusha kwa ujumla wanayo haki ya ama kukata rufaa au kuamua kuingia kwenye uchaguzi mwingine kama sheria inavyoelekeza kuwa ndani ya muda wa siku 90 inapaswa awe amepatikana Mbunge mwingine.

Wakati akitamka haki hizo zilizopo wazi, mamai ya watu hao walipika kelele kiasi cha Mbowe kushindwa kuongea wakitaka CHADEMA isihangaike na rufaa kwasababu Lema walimchagua kwa kura nyingi, na haku chaguliwa na Mahakama na hivyo kama ni rufaa ikatwe kwa wananchi waamue.

Akijibu ombi hilo baada ya utulivu kurejea ili kuweza kusikilizana, Mbowe alieleza kuwa kosa alilopatikana na hatia Lema, linaangukia katika kifungu  cha sheria za uchaguzi cha “Kufanya Matendo Kinyume na Maadili” ambacho adhabu zake zinaweza kumtoa mgombea kwenye haki ya kugombea tena kwa miaka 5, na akatolea mfano wa Steven Wassira aliewahi kufungiwa kwa miaka 5 kwa kupatikana na hatia ya kutumia rushwa katika uchaguzi.

“CHADEMA sio chama cha wahuni, ni chama cha watu makini, tunazungumza mambo makini kwa maslahi ya taifa. Kila linalotokea ni mpango wa Mungu, nasi CHADEMA tunamtanguliza Mungu. Tunajadili mustakabali wa taifa katika kipindi kigumu cha mapito. Hekima, busara na subira ya kila mtu inahitajika ili tuioneshe dunia ukiukwaji mkubwa wa haki uliopo Tanzania… Katika hatua ya sasa, tutawanyike kwa amani natutazungumza zaidi Jumamosi NMC” alimaliza na wananchi wakatawanyika kwa ustaarabu wa hali ya juu.

Mara baada ya mkutano na wananchi, ulifuatia mkutano wa ndani na wanahabari ambapo Mh Mbowe alikanusha tetesi zilizoibuliwa na swali la mwandishi kuwa CHADEMA walikuwa na makubaliano na Serikali ya CCM kugawana majimbo ya Arusha Mjini na Arumeru Mashariki.

“Hatuna mazungumzo yeyote na Serikali. Nchi inaweza kuingia kwenye machafuko pindi haki inaponyimwa na Mahakama”, alieleza Mbowe

Akifafanua zaidi kuhusu kutowakubalia wananchi ombi lao la kutaka uchaguzi urudiwe kwasababu wanaimani na mtu wao, Mbowe alisema “Hukumu imesomwa, hatujapata nakala ya hukumu. Kama kuna makosa katika mtiririko wa hukumu, tunaomba watu wawe na subira ili tusiingine kwenye machafuko”

“Watawala wasome alama za nyakati. Nchini Tunisia ni mtu mmoja tu alifanya tukio ambalo liliamsha hasira za wananchi kudai mabadiliko kwa nchi nyingine (za kiarabu). Nisingependa kuona nchi yetu inaingia huko” alisema Mbowe.

Lema azungumzia hukumu yake

IMGP0816 Lema aliwaeleza wananchi kuwa kilichohukumiwa kwa upande wake anaona ni mazingaombwe tu na kuwa sio sheria imehukumu, bali ni maelekezo hukumu iwe hivyo.

Aliwatoa woga wananchi wake na kuwataka wasiumizwe na hukumu hiyo na kwamba bado yuko nao na wawe wajasiri ili waendelee kupambana kwa pamoja kudai haki zao na kwamba hawawaacha.

“Naweza kuhisisi uchungu mlio nao mioyoni mwenu, msiogope. Mkiogopa ninyi mko wengi mimi mmoja nitaogopa zaidi. Mlipiga kura mkazilinda. Leo wametengua ubunge wangu, wana Jaji wa Mahakama sisi tuna jaji wa Mbinguni” alisema Lema.

“Safari ya ukomboziilianza zamani, watu walikufa, watu walivunjika miguu, watu walifilisika, watu walinyanyasika..safari bado inaendelea, msiogope” alieleza Lema.

Alitahadharisha taifa kuwa kama mtindo wa vyombo vilivyoaminiwa kutoa ufafanuzi wa sheria vitaendelea kufanya kazi kwa maelekezo ya kupendelea upande fulani, ipo siku demokrasia yetu itahamia msituni.

Aidha katika hotuba yake na vyombo vya habari Mahakamani asubuhi mara baada ya hukumu kutolewa, Mh Lema aliwaambia wafuasi wake kuwa alikuwa anajua jinsi hukumu ile ingekuwa vile kwa vile alishapata taarifa za maagizo toka Ikulu Dar es Salaam kuwa Mhakama ihakikishe anavuliwa ubunge.

Baadae mchana wa jana, Ikulu ya Dar es Salaam ikatoa taarifa ya kukanusha kuhusika kwake na maamuzi hayo ya kutengua Ubunge wa Lema kama mwenyewe alivyodai.

DSC07407 Akirudia tuhuma dhidi ya njama alizodai kuzigundua mapema za kutengua ushindi wake (wa zaidi ya kura 19,000) bila kuzingatia haki za kisheria kwa kusikiliza mashitaka na utetezi ili mtu atiwe hatiani kwa ushahidi usiotia shaka, aliorodhesha matukio mengine yaliyoashiria kuwa hukumu ile ilepangwa na ilishavuja muda mrefu kwa watu wa upande mmoja wa kesi husika.

Mh Lema alisema, juzi usiku Mbunge mteule wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari alikutana naafisa msaidizi wa Polisi akamwambia “mmetupiga Meru, mtalia Arusha”

Akifafanua zaidi Lema alisema kwamba, siku ya jana mapema sana asubuhi Polisi walijazana ofisini kwake kuweka ulinzi, alipofika Mhakamani nako akauta tayari kuna red tapes zimefungwa watu wasiiingie, na askari wengi wamesambazwa kila kona na wengine kujificha na magari ya maji ya kuwasha.

Alisema hali hiyo ilimpa tafsiri nyingi na kujiuliza ni nani aliwaambia ubunge umetenguliwa kabla haujatenguliwa kiasi cha kujihami namna hiyo.

Lema akasema pia kuwa alikuwa anazotaarifa siku tatu kabla ya Uchaguzi wa Arumeru Mashariki, Mwigulu Nchemba alimwagiza kijana mmoja wa CCM, Mtui kuwa akajipange kuna uchaguzi Arusha Mjini.

Akihitimisha hotuba yake, Lema alikumbushia nadhiri aliyoweka mwanzo wa kesi yake hiyo kuwa endapo akishinda atajenga sehemu maalumu kwa watu kukutana, kuzungumza na kufanya maombi. Akaahidi bado nia hiyo anayo na ndani ya miezi sita atakuwa amekamilisha kazi hiyo.

Na mwisho kabisa akawashukuru na kuwataka wananchi wasihofu kutokuwepo kwake Bungeni  na kwamba katika kipindi hicho ambacho hatakuwa Bungeni, Joshua Nassari atawatetea Bungeni.

TBC wakataliwa mkutanoni

Aidha, katika hali isiyokuwa ya kawaida wananchi waliofurika mbele ya ofisi za chama jana walikataa kabisa kuruhusu wanahabari kutoka Shirika la TBC kufika eneo lile kuchukua taarifa kwa madai kwamba TBC hupotosha umma kuhusu matukio yanayoihusu CHADEMA.

Kwa ujumla siku ya jana, pamoja na watu wengi kuonekana kuwa na hasira kwa kilichoamuliwa, hakukuwa na matukio yeyote ya ghasia, vurugu, ugomvi n.k. Watu walitawanyika kwa utulivu na amani.

Hata hivyo, viongozi wa CHADEMA wanastahili pongezi kwa kuweza kutumia busara kuwatuliza mamia ya wananchi waliokuwa na hasira dhidi ya CCM wasiweze kumdhuru mtu au kitu chochote mjini hapa, na kuwataka wapokee maamuzi hayo kwa amani na ujasiri kama changamoto katika kupigania haki yao.

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO