Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Kamanda wa Polisi Arusha aahidi Sh Mil 10 kwa atakae fanikisha kupatikana kwa wauwaji wa Mwenyekiti wa CHADEMA Usa-River, Arumeru.

DSCN0181

Thobias Andengenye, RPC Arusha akizungumza kwa niaba ya Jeshi la Polisi

KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Arusha, RPC Thobias Andengenye ametoa ahadi ya jumla ya shilingi za kitanzania milioni 10 kwa mwananchi atakaewezesha kupatikana kwa waliohusika na mauaji ya kikatili kwa aliekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kata ya Usa-River aliauwawa juzi Ijumaa.

Andengenye ameyasema hayo wakati alipopewa nafasi ya kuzungumza na wafiwa, viongozi na wananchi wengine katika sherehe za kuaga mwili wa marehemu huyo zilizofanyika katika uwanja wa Ngusero, Usa-River kuanzia saa sita mchana leo.

Akizungumza kwa niaba ya Jeshi la Polisi, Kamanda Andengenye alisema kuwa Jeshi lake lina wajibu wa kulinda maisha na mali za wananchi na hivyo litafanya kila linalowezekana kuhakikisha watuhumiwa wote wanatiwa nguvuni.

Alitoa rai kwa wananchi wema kutoa ushirikiano kwa Jeshi hilo ili kuweza kufanikisha kupatikana kwa wahalifu hao.

Kamanda Andengenye aliambatana na viongozi wengine wa Polisi akiwemo OCD wa Wilaya ya Arumeru, OCD John.

Viongozi wengine wakubwa waliopata nafasi kuzungumza katika shughuli hiyo ya kutoa heshima za mwisho walikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Arumeu Mh Mercy Silla, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Mh Joshua Nassari, na Mbunge wa Musoma Mjini Mh Vicent Nyerere.

Wengine ni mwakilishi wa Kamati Kuu ya CHADEMA na Mbunge wa Zamani Jimbo la Arusha Mjini, Mh Godbless Lema, Mbunge mpya wa CHADEMA viti maalumu, Mh Cecilia Paresso pamoja na mwakilishi wa chama  hicho Mkoa wa Kilimanjaro Mh Basil Lema.

***

DSCN0198

Mbunge wa Arumeru Mashariki, Mh Joshua Nassari akizungumza kwa hisia katika tukio hilo leo. Kwa nyuma anaonekana Kamnada Andengenye akifuatilia kwa karibu

Akizungumza kwa majozi makubwa, Mbunge wa Arumeru Mashariki Mh Joshua Nassari, mbali na kupongeza uamuzi wa Jeshi la Polisi kuwasaka wahusika kwa udi na uvumba, aliwapa muda watekeleze majukumu yao katika kipindi hiki ambacho alidai amewatuliza watu wa Arumeru na kueleza kwamba endapo uchunguzi huo utachelewa sana basi ataawaruhusu watu wa Meru wafanye kinyume chake.

Mh Nassari alikumbushia tukio la askari Polisi alieuwawa siku kadhaa zilizopita Wilayani Arumeu na jeshi la Polisi liliweza kumkamata mhusika, tukio ambalo alidai lilikuwa gumu zaidi kumpata mhusika tofauti na hili la kuchinjwa mwenyekiti, hali inayoashiria kuwa kuwapata wahusika ni rahisi zaidi.

Alisema kama kuna kundi fulani limeamua kuua viongozi wa CHADEMA mmojammoja kwa kudhani labda watawapunguza nguvu, basi watambue kuwa ndio kwanza wamechochea moto.

Nassari aliwataka wananchi kuungana nae katika mfungo wa siku mbili mfululizo kuanzia kesho ili kumuomba Mungu asimamie harakati za ukombozi ambazo zinaonekana kuhujumiwa.

Alitumia nafsi hiyo pia kuwasihi wananchi waguswe na mzigo waliobaki nao familia ya marehemu na kuwaomba watakaokuwa na chochote wachangie katika visanduku vilivyokuwa vinapitishwa.

Miongoni mwa waliotoa michango yao ya rambirambi uwanjani hapo ni pamoja na Kamanda Andengenye.

****

DSCN0216

Aliekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, na Mjumbe wa Kamati Kuu CHADEMA Mh Gobless Lema akizungumza katika shughuli hiyo ya kuaga mwili wa marehemu leo

Aliekuwa Mbunge wa Arusha Mjini ambae aliwakilisha Kamati Kuu ya CHADEMA iliyokutana jana, Mh Godbless Lema alisema Kamati Kuu ilishtushwa sana na taarifa za kifo hicho cha kusikitisha kiasi cha kupelekea kikao husika kuvurugika mara baada ya kupokea picha za mauaji ya kikatili toka kwa Mbunge Nassari.

Lema aliwataka wananchi wasiogope wala kutishika na matukio haya ya mauaji yanayokiandama chama chake na kuadai kwamba kama kikundi hicho cha uchinjaji bado kipo basi yeye yupo tayari kufuata baada ya mwenyekiti huyo kuchinjwa.

Alisema hali imekuwa ya hatari kiasi kwamba watu wanaogopa kuishi na hata kupokea simu.

Lema aliwataka wananchi waliohudhuria viwanjani pale kuwa wasilipize kisasi na badala yake wafanye sana maombi na kumuomba Mungu kisasi hicho kiwarudie wahusika.

Akifafanua zaidi alidai kuwa lipo kusudi kwenye mauaji hayo na kudai kwamba pengine ni juhudi za kumdhoofisha Mbunge Nassari na kuwatisha wananchi wasishiriki harakati za ukombozi zinazoendeshwa na kusimamiwa na chama chake.

“Lipo kusudi kwenye haya mauaji, wacheni hasira zijikusanye taratibu. Mnapigwa risasi kwasababu mnataka ardhi, mnataka watoto wenu wasome vizuri. Pigweni risasi ukombozi unakuja” alisema Mh Lema.

Lema aliwasihi wananchi walisiwahukumu Polisi wote kwa mavazi yao kwasababu miongoni mwao wapo ambao wanaumia na matukio haya.

Kabla ya kueleza kuanza ziara ya kuimarisha chama mikoa ya Iringa kwa wiki hii, Lema aligusia ujumbe aliodai uliwahi kutolewa na marehemu kwa baadhi ya viongozi wake kabla hajafa.

Lema akasema marehemu Msafiri aliwahi kumueleza yeye na Vicent Nyerere kuwa kuna watu walikuwa wanamtishia watamuua.

Akiwasilisha salamu za Kamati Kuu, Lema alisema kuwa Kamati Kuu na chama kwa ujumla kitaangalia namna gani ya kuweza kuwasaidia mke na watoto walioachwa na marehemu.

Awali msemaji wa familia ambae ameachiwa jukumu la kulea familia ya marehemu, aliomba wasamaria wema kuweza kujitkeza kumsadia kuwasomesha watoto hao watatu walioachwa na marehemu.

***

DSCN0211 Mh Vicent Nyerere kwa upande wake alianza kwa kumshukuru RPC Andengenye kwa ahadi ya kuwasaka wahalifu hao hadi wapatikane na kudai kuwa ataifuatilia ahadi hiyo.

Mh Nyerere alilaani mauaji hayo kwasababu yamemnyima marehemu haki yake Kikatiba, haki ya kuishi na pia yamewaudhi wengi na kwamba hata yeye hapendi kuona yakijirudia iwe ni kwa mtu yeyote, alie na itikadi ya siasa na asie nayo.

Alitoa masikitiko yake juu ya mke wa marehemu wa watoto ambao wameachwa wakiwa.

***

DSCN0186

 Mwakilishi wa CHADEMA Kilimanjaro, Mh Basil Lema

Nae mwakilishi wa CHADEMA Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema alisema hana wasiwasi na Jeshi la Polisi na kuwataka majirani watoe ushirikiano kwa Jeshi hilo ili wahusika wapatikane.

Akizungumzia kuchinjwa kwa Msafiri, Basil alisema damu yake itaendelea kuwa chachu ya kudai ukombozi na kwamba lengo la ukombozi si la mwili.

“Mapambano yataendelea hata kwa kufa mmojammoja. Tutakawa mapanga, lakini tutaingia Ikulu na makovu yetu” alisema Basil Lema.

***

Wawakilishi wa CHADEMA Arusha na Arumeru nao walielezea imani yao kwa Jeshi la Polisi na kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Jeshi hilo ili kuhakikisha watu waliohusika na mauaji hayo wanapatikana ili kurudihsa imani ya wananchi kwa jeshi hilo.

Waliwataka wananchi ambao watakuwa waoga kujitokeza Polisi basi waende ofisi ya chama na kutoa taarifa zitakazosaidia kuwapata wahalifu hao.

Wananchi walielezwa wakichukulie kifo cha mpendwa wao kama mbolea ya kupambana na uonevu hadi hatua ya mwisho kwasababu yapo maisha baada ya kifo.

DSCN0182

 Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Arumeru, Ndg Toti Ndonde

Akinukuu maneno ya wanafalsafa wa dunia, Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Arumeru Ndg Toti Ndonde alisema taifa na binadamu vinaweza kuzaliwa na kufa lakini mawazo hayawezi kufa, na hivyo anaamini Msafii bado anaishi kwa namna hiyo kwasbabu alikuwa mwanamapinduzi.

***

Serikali iliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru ambae mbali na kulaani mauaji hayo, aliahidi kuwa Serikali yake itashirikiana na Jeshi la Polisi kuhakikisha matukio kama haya hayajirudii tena katika jamii.

DSCN0223Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mh Mercy Silla

Mwili wa marehemu umesafirishwa leo jioni kwenda Same-Kilimanjaro kwa maziko yanayotarajiwa kufanyika kesho.  Mbunge wa Musoma Mjini ndie atakaewakilisha chama katika maziko hayo.

BLOG hii inawapa pole wafiwa wote na Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema. Amina!

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

1 maoni:

Anonymous said...

BWANA WETU YESU KRISTO ALIKUFA PALE MSALABANI KWA AJILI YA DHAMBI ZETU.


HIVYO MUNGU WA REHEMA WEWE PEKE YAKO NDIO UNAWAJUWA CC HATUWAFAHAMU WAUAJI HAWA. WAPE KUWA NA MOYO WA NYAMA NA UWAPE KUONA HUKUMU HII INAWAHUSU NA KUKURUDIA WEWE. MAANA WANAIJUA DHAMIRA YAO YA KUMUUA BINADAMU MWENZAO KWA KUMCHINJA

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO