CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kile cha CUF viko mbioni kuungana na kuendesha maandamano makubwa ya pamoja kuishinikiza serikali kuwajibika kwa kushindwa kuongoza nchi.
Wakati CUF kupitia kwa Mwenyekiti wake, Prof. Ibrahim Lipumba, kikiwa kimeweka wazi utayari wake wa kushirikiana na vyama vingine kufanya maandamano ya nchi nzima kutaka viongozi waliotuhumiwa kwa matumizi mabaya ya fedha za umma wawajibishwe, CHADEMA jana kilisema nacho kipo tayari kuungana na chama hicho kufanikisha jambo hilo.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, alisema wapo tayari kuungana si na CUF tu, bali chama chochote chenye dhamira ya kurudisha mamlaka ya nchi kwa Watanzania.
Mnyika alisema tayari Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe, alishatangaza wiki iliyopita akiwa bungeni kuwa watarudi kwa wananchi kuunganisha nguvu za pamoja na kufanya maandamano makubwa kupinga vitendo vya kifisadi baada ya kuona viongozi wa juu wa serikali wakishindwa kuchukua maamuzi magumu.
Aliongeza kuwa hivi sasa umma unapaswa kuungana kuiwajibisha serikali na kumtaka Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, asirudi nyuma katika dhamira ya kuwatetea wananchi.
“Si kuunganisha upinzani tu bali CHADEMA iko tayari kuendelea kuunganisha Watanzania wote wenye kutaka uwajibikaji wa serikali ya Kikwete kwa kuwa madaraka na mamlaka yote ni ya umma, serikali inafanya kazi kwa niaba ya wananchi,” alisema Mnyika.
Alibainisha serikali iliyopewa ridhaa na wananchi ya kuwaongoza inaposhindwa kusimamia masilahi ya wananchi na kuwalinda mafisadi inapaswa iwajibishwe na wananchi na kubainisha hatua hiyo itakuwa ni muendelezo wa harakati za ukombozi wa kweli wa Watanzania.
Hata hivyo, Mnyika alisema maamuzi kamili ya namna ya kuunganisha nguvu hizo na kufanya maandamano makubwa yatakayotikisa nchi, yatatolewa Jumapili wiki hii baada ya kikao cha Baraza Kuu la CHADEMA kukutana
CHANZO: TANZANIA DAIMA, 27 Aprili 2012
0 maoni:
Post a Comment