CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetishwa na wimbi la mauaji yanayotishia amani ya nchi kikidai kuwa jumla ya wanachama wake 15 wameuawa katika wilaya ya Igunga peke yake.
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alidai kuwa mauaji hayo yana mkono wa serikali ya CCM, ambayo imeona wazi kuwa upepo wa kisiasa umekiendea vibaya na sasa kinataka kujiimarisha katika utawala kwa kuua watu wanaoipinga.
Akifungua kikao cha Baraza Kuu la chama hicho jijini Dar es Salaam jana, mwenyekiti huyo alifafanua kuwa mbali na kuuawa kwa watu wanne kwa pamoja na juzi kifo cha mwenyekiti wao wa tawi huko Arumeru mkoani Arusha, jumla ya wanachama wake 15 wameuawa katika wilaya ya Igunga peke yake tangu kumalizika kwa uchaguzi mdogo wa jimbo hilo mwaka jana.
“Wapo watu wanadhurika kwa sababu ya kuwa CHADEMA na mfano mzuri ni Mbunge Highnes Kiwia, aliyeshambuliwa na wahuni wa serikali ya CCM. Kule Igunga zaidi ya wanachama wetu 15 waliuawa na lengo la yote haya ni kuwakatisha tamaa wananchi ili wasiiunge mkono CHADEMA,” alisema Mbowe.
Alisema mauaji ya watu wanne yaliyotokea Arusha wiki mbili zilizopita na ya juzi ya mwenyekiti wa tawi wa chama hicho, hayawezi kuepushwa na hujuma za kisiasa kwa kuwaandama watetezi wa haki za wanyonge.
Alisema serikali yoyote inayotumia vyombo vya dola na vijana wake kuua watu, haina uhalali wa kuwa madarakani na kwamba chama hicho kimeamua kwa dhati kupambana na kila aina ya uchafu ndani ya nchi kwa nia ya kuwaokoa Watanzania wanaoangamia.
Mbowe alizidi kuishambulia serikali akisema hatua ya kunyamazia mauaji na kupigwa kwa viongozi na wanachama wa CHADEMA ni kielelezo tosha cha watawala kukata tamaa na ishara ya wazi ya kutapatapa.
Polisi yakanusha, yaunda tume
Kutoka jijini Arusha, Jeshi la Polisi nchini limedai kuwa halina habari juu ya mauaji hayo kuhusishwa na mambo ya kisiasa, lakini limekubali kuunda tume maalumu ya kuchunguza vifo hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Naibu Kamishna wa Polisi, Isaya Mngulu, ilisema kuwa Mkuu wa Jeshi hilo nchini, Inspekta Jenerali, Saidi Mwema, ameunda tume maalumu itakayokuwa chini ya Mngulu na kujumuisha maofisa wa ngazi mbalimbali wa jeshi hilo kwa ajili ya kuongeza nguvu ili kufanikisha uchunguzi wa matukio ya mauaji na vurugu wilayani Arumeru.
Mngulu pasipo kuingia kwa undani kutokana na tuhuma za mauaji hayo kuhusishwa na mambo ya kisiasa, alikiri kuwa matukio hayo yamesababisha hali kuwa tete katika wilaya ya Arumeru, hivyo watalazimika kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na wananchi ili wahusika wote waweze kukamatwa.
Aliwataka wananchi wenye taarifa kuzitoa jeshi hilo na kwa viongozi wa serikali huku akiwahakikishia kuwa hakuna atakayewataja hadharani.
Mchakato wa Katiba, rufaa ya ubunge
Kuhusu mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya, Mbowe alisema wakati Kamati ya Katiba inafanya kazi yake CHADEMA itakuwa njiani kuwaelimisha wananchi ni vitu gani vinapaswa kuwepo na kutokuwepo katika Katiba hiyo.
Alisema wananchi watajadili Katiba kadiri wanavyotaka na siyo kama anavyotaka Rais Jakaya Kikwete na kwamba hata suala la Muungano litajadiliwa.
Akiongelea sababu za kukata rufaa katika jimbo la Arusha mjini Mbowe alisema wamefanya hivyo kwa ajili ya kuweka kumbukumbu ya kusimamia haki, huku akibainisha kwamba hata kama uchaguzi wa jimbo hilo utafanyika leo wana uhakika wa kushinda kwa kiwango kikubwa.
“Tunaamini wapo majaji ambao wana nafasi ya kusimamia haki pasipo kuyumbishwa na wao watafanya kazi hiyo kwa uadilifu kwa ajili ya kuweka kumbukumbu za upatikanaji wa haki sawa; hiyo ndiyo sababu iliyotufanya tukate rufaa katika jimbo la Arusha mjini,” alisema Mbowe.
Akizungumzia mfumko wa bei mbowe alisema hali ni mbaya kwa mfumko kutoka asilimia 19 hadi 24 na kubainisha hali hiyo inachangiwa na watendaji wanaojifikiria wenyewe pasipo kuwaangalia wananchi wanaowatumikia.
“Kama hali itaendelea hivi ni hatari kwa usalama wa nchi kwani matumizi ya serikali peke yake ni shilingi trilioni 12 na ukiangalia kwa umakini wanaochangia hali hii ya matumizi makubwa ni viongozi wanaotumia fursa vibaya,” alisema Mbowe.
Sabodo aishukia serikali
Naye kada maarufu wa CCM na mfanyabiashara maarufu nchini Mustapha Sabodo, aliyealikwa katika mkutano huo, aliishukia serikali ya CCM akidai kuwa viongozi wake hawana shukrani kwa namna alivyojitolea kwa miaka 50 kuisaidia kwa kila njia.
Sabodo alisema hajawahi kupewa hata ‘asante’ na viongozi wa CCM, pamoja na kuipa msaada wa mabilioni ya fedha, hali ambayo imemsikitisha.
“Mimi si mwanasiasa na hata wakati wa uhai wa Baba wa Taifa (Mwalimu Nyerere) nilitaka kupewa uwaziri na baadaye uenyekiti wa benki ya NBC nikakataa kwa sababu mimi ni mfanyabiashara lakini juu ya yote hawajui hata kusema asante kwa niliyowafanyia,” alisema Sabodo.
Sabodo alikiri kuwa CHADEMA imeonyesha kuwa ni chama makini, kinachopigania maslahi ya Watanzania na kuthamini mchango wa kila mtu bila ubaguzi, na kudai kuwa atawafuata marafiki zake akiwemo waziri mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba na kuwaeleza umuhimu wa kuiangalia CHADEMA kama chama kinacholenga kuwakomboa wanyonge. Aliahidi kuzidisha misaada zaidi kwa CHADEMA, na kukumbushia ahadi yake ya kuwapatia jengo la kisasa kwa ajili ya ofisi.
Alisema dhana kuwa chama hicho ni cha kidini ni propaganda za watu walioshindwa kwenda na kasi yake na kutaka kutumia nafasi ya kuwachonganisha wananchi ili wapate kuwatawala milele.
“Wanasema CHADEMA inabagua dini huo ni uongo na ninakuombeni muendelee kupambana CHADEMA hoyeee!” alisema Sabodo huku wajumbe wa baraza kuu wakimshangilia.
Awali katibu mkuu wa CHADEMA Dk. Willibrod Slaa akiuelezea uzalendo wa Mustapha Sabodo, alisema amekuwa muwazi kwa mambo yake licha ya wafanyabiashara wengi kubaki katika mawazo mgando kuwa mtu anayetaka mambo yake yaende sawa ni lazima awe mwanachama waCCM.
Alisema watu wengi wenye uwezo na hata wasomi wamekuwa wakijificha kuzungumzia siasa hususan kwa upande wa upinzani kwa hofu ya kuharibikiwa mambo yao tofauti na Sabodo ambaye ni muwazi kwa kila anachokifanya.
Alisisitiza ufisadi wa Tanzania unatokana na mambo mengi kufanywa gizani kwa kuwa hadharani watu wanaogopa wataumbuliwa.
“Wanatuuliza tunapokea hela za Sabodo tuna uhakika gani kama si za fisadi, sisi tunawaambia huyu hafanyi gizani na kama ana madhambi leo hii kwa namna anavyojitoa kwa CHADEMA asingekuwa na kitu,” alisema Dk. Slaa.
CHANZO: Tanzania Daima, 30th April 2012
0 maoni:
Post a Comment