Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

“Uchaguzi EALA usogezwe mbele, uteuzi umekiuka Mkataba wa Afrika Mashariki”

Mchakato wa uchaguzi wa Afrika Mashariki unaoendelea hivi sasa sio huru na wa haki hivyo Spika, Katibu wa Bunge na serikali wanapaswa kuchukua hatua za haraka kurekebisha kasoro zilizojitokeza ili kuhakikisha uchaguzi huo unawezesha wabunge kupatikana kidemokrasia na kwa kuzingatia maslahi ya umma. Aidha, natoa mwito kwa wananchi na wadau wote kufuatilia kwa karibu uchaguzi huu muhimu kwa taifa kwa kuwa unahusu uwakilishi wa nchi katika chombo muhimu cha kuwakilisha wananchi, kuvisimamia vyombo vya kiutendaji vya Jumuia ya Afrika Mashariki na kutunga sheria za kufanikisha utekelezaji wa mkataba wa Jumuia ya Afrika Mashariki na mipango muhimu ya maendeleo katika masuala ya ushirikiano.

Baadhi ya hatua za haraka zinazopaswa kuchukuliwa ni: Msimamizi wa kuzingatia kuwa amefanya uteuzi bila kuzingatia ibara ya 50 ya Mkataba wa Jumuia ya Afrika Mashariki; kusogeza mbele tarehe ya uchaguzi ili kutoa fursa kwa wagombea walioteuliwa kufanya kampeni rasmi na pia kutoa nafasi kwa mapingamizi kuwekwa kwa wagombea wasiokuwa na sifa kwa mujibu wa Mkataba wa Jumuia ya Afrika Mashariki na kanuni husika; kueleza wazi kwa vyama, wabunge na wananchi ni mfumo uliotumika kugawanya idadi ya nafasi tisa zinazogombewa kwa kuzingatia matakwa ya ibara ya 50 ya Mkataba wa Jumuia ya Afrika Mashariki; kufanya marekebisho ya Kanuni za Kudumu za Bunge zinazosimamia uchaguzi wa Afrika Mashariki.Izingatiwe kwamba kwa mujibu wa Katibu wa Bunge ambaye ni Msimamizi wa Uchaguzi husika uteuzi wa wagombea ulipaswa kufanyika tarehe 10 Aprili 2012; hata hivyo uteuuzi wa wagombea umetangazwa tarehe 14 Aprili 2012.

Aidha, vyombo mbalimbali vya habari vimenukuu kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeteua wagombea 24, kwa msingi wa majina matatu ya wagombea kwa kila kundi hali ambayo inaonyesha kwamba kwa mujibu wa maelekezo yaliyotolewa na Msimamizi wa Uchaguzi, chama hicho kimoja kinatarajia kuwa na nafasi nane miongoni mwa nafasi tisa za wabunge wa Afrika Mashariki.Tafsiri ya suala hili ni kwamba inatarajiwa kuwa vyama vya upinzani vitapata nafasi moja tu hali ambayo ni kinyume kabisa na ridhaa ya wananchi ambayo waliionyesha kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na pia ni kinyume na Ibara ya 50 ya Mkataba wa Jumuia ya Afrika Mashariki ambao unataka uwakilishi mpana.

Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi uliopita ambayo yanapaswa kuwa msingi mmojawapo muhimu katika maamuzi kuhusu mgawanyo wa viti CCM (asilimia 74 ya uwakilishi bungeni hata kama ikichukua zote na kuacha kutoa kwa vyama vingine inastahili nafasi zisizozidi 7), CHADEMA (Asilimia 13.7 sawa na nafasi 1) na CUF (Asilimia 10.3 sawa na nafasi 1).

Izingatiwe kwamba ibara ya 50 (1) ya Mkataba wa Afrika Mashariki inatamka bayana kwamba “The National Assembly of each member Partner State shall elect, not from among its members, nine members of the assembly, who shall represent as much as it is feasible, the various political parties represented in the National Assembly, shades of opinion, gender and other special interest groups in the partner state, in accordance with such procedure as the National Assembly of each Partner State may determine”.

Hivyo, Kanuni ya 12 na Nyongeza ya Tatu ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la 2007 inakinzana na kugongana na Ibara ya 50 ya Mkataba wa Afrika ya Mashariki hali ambayo inadhihirisha umuhimu wa Kanuni husika za Bunge kufanyiwa marekebisho au mabadiliko kwa mapendekezo yangu au ya Kamati ya Kanuni kama nilivyoomba kwenye barua yangu kwa Katibu wa Bunge ya tarehe 8 Februari 2012.Kutokana na upungufu huo, ili kuhakikisha uteuzi na uchaguzi unafanyika kwa mchakato huru na wa haki niliwasilisha mapendekezo ya ziada ya marekebisho yenye kulenga kanuni husika zibadilishwe kabla ya uchaguzi kufanyika tarehe 17 Aprili 2012.

Kwa mujibu wa Kanuni ya 115 Nyongeza ya Nane 3 (3) (b) na Kanuni ya 152 (1); nimependekeza marekebisho yafanyike katika Kanuni ya 12 kwa: kuondoa maneno “uwiano wa idadi ya wabunge wa vyama mbalimbali vinavyowakilishwa bungeni’ na kuingiza maneno “vyama vya siasa vyenye uwakilishi bungeni”; kuongeza maneo “maoni mbalimbali (shades of opinion) na makundi maalum ya kijamii” mara baada ya neno ‘jinsia’ na kabla ya maneno ‘uwakilishi wa pande zote mbili za Muungano”

Pia, kwa mujibu wa Kanuni ya 115 Nyongeza ya Nane 3 (3) (d) nimependekeza kufanyike mabadiliko katika Nyongeza ya Tatu ya Kanuni kwa: kufuta kifungu cha 5 (5); kufuta kifungu cha 11 (3) na kubadili mpangilio wa namba kuanzia kifungu kidogo cha (4); Kufanya marekebisho kwenye vifungu vya 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12 na 13 kama nilivyopendekeza kwa barua yangu ya tarehe 4 Aprili 2012.Aidha, nimewaandikia rasmi barua Spika na Katibu wa Bunge kuwaomba wachukue hatua za haraka kurekebisha mchakato wa uchaguzi husika ikiwemo kuitisha kikao cha dharura cha Kamati ya Kanuni kwa ajili ya kuchukua hatua zinazostahili ili kuhakikisha uteuzi na uchaguzi unakuwa huru na haki kuepusha kasoro zilizojitokeza mwaka 2006 wakati wa Bunge la tisa kujirudia mwaka 2012 katika Bunge la kumi.


John Mnyika (Mb)
Bungeni-Dodoma
14/04/2012

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO