Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Jinamizi La Millya laendelea kuiandama CCM, safari hii Diwani wake mwingine mkoani Mwanza Ajiunga na CHADEMA

UPEPO mbaya unaonekana kukikumba Chama cha Mapinduzi (CCM), kwa viongozi wake kukihama chama hicho, umeingia katika Mkoa wa Mwanza, ambapo Diwani wa Kata ya Nyampulukano Wilayani Sengerema mkoani hapa, Hamis Mwangao Tabasamu ametangaza kuihama CCM na kujiunga na Chadema.

Diwani huyo ambaye amejipambanua kwa kupiga vita ufisadi ndani ya wilaya hiyo, ametangaza azma yake hiyo katika kikao na waandishi wa habari kilichofanyika Ryan's hoteli, na kupokelewa na aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema (Chadema).

Diwani Tabasamu ambaye jumamosi amepanga kuhudhuria na kuhutubia mkutano mkubwa utakaoongozwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa kata ya Nyampulukano, amekuwa ni miongoni mwa viongozi wengine wa CCM kukihama chama hicho na kujiunga na Chadema ndani ya muda wa wiki moja.

Hivi karibuni, aliyekuwa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Mkoa wa Arusha, James Milya alitangaza kujiuzulu nyadhifa zake zote kisha kujiunga rasmi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo.

Mbali na Milya, viongozi wengine kadhaa akiwemo diwani wa Kata ya Sombetini mkoani Arusha, Alphonce Mawazo (CCM), juzi alikihama chama chake hicho kisha kujiunga na Chadema, chama ambacho kinaonekana kuiweka pabaya CCM na Serikali yake kwa ujumla.

Akizungumza mchana huu wa leo, katika kikao chake na waandishi mbele ya Lema ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Taifa, diwani Tabasamu ambaye aliwahi kuibua tuhuma za ufisadi katika halmashauri ya Wilaya ya Sengerema alisema: "Kuanzia leo (jana), natangaza rasmi kukuhama CCM na kujiunga na Chadema".

Alisema, lengo lake la kuhama kutoka ndani ya CCM si la kushawishiwa na mtu ama kiongozi yeyote, bali ni dhamira yake ya kweli kama Mtanzania halisi mwenye uhuru wa mawazo, na kwamba amechoshwa na siasa za 'majitaka' ndani ya CCM.

Kwa mujibu wa diwani huyo wa Nyampulukano wilayani Sengerema, kuondoka kwake CCM inatokana na kushindwa kuafikiana katika maslahi ya wananchi, ambapo alidai wapo baadhi ya viongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo wanakumbatia vitendo vya kifisadi.

"Uamuzi wangu huu wa kuhamia Chadema kutoka CCM unatokana na kushindwa
kuafikiana katika mambo yanayogusa maslahi ya wananchi katika
halmashauri ya wilaya ya Sengerema.

"Mafisadi wameliteka baraza la Madiwani la Sengerema!. Kwa maana hiyo natangaza rasmi leo, najiuzulu nafasi zangu zote ndani ya CCM, na nahamia Chadema", alisema Tabasamu ambaye amewahi kuingia mgogoro na mkuu wa wilaya hiyo, Elinas Palagyo kwa kile kinachodaiwa msimamo wake wa kupiga vita ufisadi.

Alizitaja sababu nne za kuhama ndani ya chama hicho tawala kuwa ni pamoja na kuwepo kwa madiwani wengi wa CCM wasio wazalendo kwa kuruhusu kuhamishwa mnada wa ng'ombe kutoka Kijiji cha Ibondo Nyampulukano kisha kuhamishiwa Kata ya Sima.

Sababu nyingine ni ucheleweshaji wa makusudi kuunda halmashauri ya mji
wa Sengerema kuanzia mwaka 1990 hadi mwaka huu, kupunguzwa kwa mipaka ya mji mdogo bila kufuata vikao halali vya kisheria.

Nyingine ni halmashauri ya wilaya hiyo ya Sengerema, iliyopo chini ya uenyekiti wake, Mathew Lubongeja (CCM), kushindwa kuwachukulia hatua watu aliowaita wezi waliotajwa na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), PPRA, ambapo alidai maelekezo ya CAG kuhusu kuchukuliwa hatua watuhumiwa wa ufisadi kutotekelezwa hadi leo.

Awali, akizungumza katika kikao hicho na waandishi wa habari, Lema alimpongeza diwani huyo wa Nyampulukano kwa kuondoka ndani ya CCM na kujiunga na Chadema, na alisema huo ni uamuzi sahihi na wa kijasiri unaolenga kuikomboa nchi hii kutoka CCM.

"Nakupongeza sana mheshimiwa Tabasamu kwa kuondoka CCM na kuja Chadema chama makini. Nawaomba sana na madiwani, wabunge na viongozi wengine wa CCM wawahi kujiunga na Chadema kabla safina haijafungwa", alisema Lema.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma - FikraPevu.com, Mwanza

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO