Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

HOJA YA KUTOKUWA NA IMANI NA WAZIRI MKUU BUNGENI KWA MUJIBU WA KATIBA IBARA YA 53A NA KANUNI YA BUNGE, KIFUNGU CHA 133 KUWASILISHWA KWA SPIKA KESHO TAREHE 23/04/2012

HOJA YA KUTOKUWA NA IMANI NA WAZIRI MKUU BUNGENI KWA MUJIBU WA KATIBA IBARA YA 53A NA KANUNI YA BUNGE, KIFUNGU CHA 133 KUWASILISHWA KWA SPIKA KESHO TAREHE 23/04/2012

•    Masharti yametimizwa; wabunge 73 wazalendo wamesaini
•    Ni mwendelezo wa ‘Operesheni Uwajibikaji’

Mnamo tarehe 19/04/2012 wakati nahitimisha hoja ya Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma nilieleza kusudio langu la kuwaomba waheshimiwa wabunge waniunge mkono katika kutia saini zisizopungua asilimia 20 yawabunge wote ili kuweza kutimiza matakwa ya Katiba ibara ya 53A kwa ajili ya kuwasilisha Bungeni hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu.

Mnamo tarehe 20/04/2012 niliandaa orodha ya waheshimiwa wabunge wote na kuisambaza ndani na nje ya ukumbi wa Bunge ili waheshimiwa wabunge wote waweze kutia saini hizo, na mpaka leo tarehe 22/04/2012 orodha hiyo imetimiza idadi ya wabunge wazalendo wanaopigania uwajibikaji 73 kutoka vyama vyote vyenye uwakilishi Bungeni, isipokuwa chama cha UDP ambacho kina Mbunge 1 na hajatia saini waraka huo mpaka sasa. 

Kwa mujibu wa kanuni za Bunge kifungu cha 133 (1) kinasomeka “Mbunge yeyote anaweza kutoa taarifa ya maandishi kwa Spika ya kutaka kuleta hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu kwa mujibu wa ibara ya 53A ya Katiba” na kwa mujibu wa kifungu kidogo cha (3) kinasomeka “hoja ya kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu haitajadiliwa na Bunge
isipokuwa tu kama;

(a)    “taarifa ya maandishi iliyowekwa saini na kuungwa mkono na Wabunge wasiopungua asilimia 20 ya wabunge wote itatolewa kwa Spika, siku zisizopungua kumi na nne kabla ya siku inayokusudiwa kuwasilishwa Bungeni;”

Hali kadhalika kanuni za Bunge Kifungu cha 133 (4) kinasomeka kuwa “hoja inayotolewa chini ya Kanuni hii na iliyotimiza masharti ya Katiba,itawasilishwa Bungeni mapema iwezekanavyo na itaamuliwa kwa kura za siri”.

Hivyo basi baada ya kutimiza matakwa ya kikatiba na kanuni za Bunge kesho tarehe 23/04/2012 tutawasilisha rasmi kwa Spika Taarifa ya Maandishi kwa mujibu wa kanuni 133 (1) na (3) ya hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu kwa kushindwa kusimamia uwajibikaji wa Serikali Bungeni kwa mujibu wa ibara ya 52 na hivyo kulinda Mawaziri wenye kusababisha matumizi mabaya ya fedha za umma na kulisababishia hasara taifa.

Tunatarajia kwamba siku kumi na nne baada ya kuwasilisha hoja hiyo Bunge litakutana kwa  haraka kujadili hoja hiyo ili kuwezesha uwajibikaji na hatua kuchukuliwa za kuhakikisha mapendekezo ya ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na maazimio ya Bunge
yanatekelezwa. Hoja hii ni mwendelezo wa ‘Operesheni Uwajibikaji’ hivyo tunaomba wabunge wazalendo na watanzania wote waiunge mkono ili kuimarisha Uwajibikaji wa Viongozi, kupambana na ubadhirifu na kunusuru uchumi wa nchi na kuchangia katika ustawi wa wananchi.

Kwa niaba ya wabunge wazalendo waliotia saini kuunga mkono taarifa ya
hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu ni;

  …………………………….
Kabwe Zuber Zitto.
Mbunge Jimbo la Kigoma Kaskazini.
22/04/2012

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO