CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimezidi kupoteza nguvu zake sehemu mbalimbali nchini, baada ya waliokuwa viongozi na makada wake ngazi za vijiji na wilaya kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Habari kutoka mikoa ya Manyara, Iringa na Kagera zimesema kuwa wimbi la kukimbia kwa wanachama wa CCM na kujiunga na upinzani limeshika kasi kuliko mwaka wowote tangu kuingia kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Huko Babati zaidi ya wanachama 1,500 wa CCM wakiwamo wenyeviti wa vijiji wilayani Babati wamekihama chama hicho na kujiunga na CHADEMA, wakati wa mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Kati ya waliojiunga na CHADEMA ni pamoja na Bi. Zamda ambaye ni kada maarufu wa CCM mjini hapa, Wakili Lumambo na wenyeviti wawili wa vijiji vya Mruki na Hala, ambao walijiunga na wanachama wao zaidi ya 100.
Akihutubia mkutano huo, Lissu amewataka wananchi wa Jimbo la Babati Mjini na wengineo kuiga mifano ya waliokataa kuonewa na kunyanyaswa na serikali ya CCM badala yake wachukue hatua ili kuondoa uvundo, wizi na uozo unaoendelea kufanywa na watawala.
“Hatujaweka mkataba wa kuibiwa na serikali ya CCM kwa kipindi cha miaka mitano mitano, kwa hiyo hatuhitaji kusubiri hii miaka mitatu ya uchaguzi iliyobaki. Wakati umefika sasa wa kuchukua hatua, tukianzia na hili suala la mawaziri wanane, na pamoja na umaskini wetu tukiamua kusema kwa pamoja hakuna mtu atakayeweza kutuzuia,” alisema Lissu.
Huko Iringa, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kihesa Mgagao, Kata ya Ngúruwe, wilayani Kilolo, Isdori Kindole na wazee wawili, Tula Dumba (75) na Japhet Ngoda (88) wamejiunga na CHADEMA kutokana na kile walichodai kuwa wameshindwa kupata haki ya kweli kutoka katika chama hicho kupitia uongozi wao wa kijiji hususan diwani wao kutuhumiwa kuhujumu mali za umma.
Wazee hao wamedai kuwa wao waliingia kwenye TANU wakati Rais akiwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, walipata fursa ya kukaa pamoja na kuzungunza juu ya mambo mbalimbali yakiwamo ya chama pamoja na maendeleo ya Watanzania kwa ujumla.
Akindole alisema sababu kubwa iliyomfanya kuhamia CHADEMA ni kuona uongozi wa CCM wa sasa ukiwanyanyasa wananchi kupita kiasi na kunyamazishwa pindi wanapokuwa na maneno ya kushauriana juu ya maendeleo ya kijiji chao.
“Kwa sababu hiyo mimi nimeamua kutoka kwenye Chama cha CCM na kuhamia CHADEMA ili nijaribu kuona msimamo unakwendaje, maana tunanyanyaswa kupita kiasi na tukitaka kulalamika serikali haitusikilizi, na mbunge akija hapa tukilalamika hata yeye hatusikilizi. Mimi nilikuwa na mambo yangu mengi tu nimelalamika mpaka wilayani lakini sikusikilizwa. Tufanyeje wananchi?’’ alisema Japhet.
Kwa upande wake mzee Tula amesema kuwa, wakati wa uongozi wa Mwalimu Nyerere kulikuwa na viongozi waliokuwa wamepata mafunzo ya uongozi kwa lengo la kuwasaidia wananchi lakini kwa sasa wananchi wakilalamika viongozi hawatoi msaada wowote zaidi ya kukandamizwa kutokana na viongozi wengi kukosa maadili ya uongozi.
“Hapa nilipo nina miaka 75, mzee kama mimi sikuwa na haja ya kuhama hama chama, lakini ninatafuta msaada, kama CCM kungekuwa na msaada viongozi wasio bora wangekuwa wanaonywa na kufuata maadili ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kweli nisingehama,“ alisema Tula.
Aidha, wazee hao wamesema kuwa, licha ya wao kuhamia CHADEMA, lakini bado wanaiomba serikali kumchukulia hatua mwenyekiti huyo wa Kijiji cha Kihesa Mgagao ambaye pia ni diwani wa kata na mwenyekiti wa CCM, kwani hawatendei haki wazee wa kijiji hicho na wananchi kwa ujumla na uongozi wake ni wa kidikteta.
CHADEMA yashinda viti vinane
Huko Chato, katika Mkoa mpya wa Geita, CHADEMA kimepata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mdogo wa wenyeviti wa serikali za vijiji baada ya kuibwaga CCM kwa kupata vijiji vinane kati ya 11 vilivyokuwa vikishindaniwa.
Uchaguzi huo mdogo wa kuziba nafasi zilizoachwa wazi na baadhi ya viongozi waliokuwepo awali jimboni humo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vifo ambao ulifanyika hivi karibuni uliwafanya baadhi ya Wana CCM kujiunga na CHADEMA mara baada ya matokoeo kutangazwa akiwamo aliyekuwa mgombea wa CCM wa Kijiji cha Minkoto.
Nafasi zilizogombewa zilikuwa zikishikiliwa na viongozi wa CCM kabla ya baadhi yao kujiuzulu, kuhamia vyama pinzani na wengine kuhama makazi yao na kwenda maeneo mengine.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, msimamizi msaidizi wa uchaguzi huo, Sodio Nyuga alisema CHADEMA kimefanikiwa kutwaa nafasi 8 za vijiji dhidi ya tatu zilizonyakuliwa na CCM .
Hata hivyo, CCM ilijifariji kwa kutwaa uenyekiti katika vitongoji 28 na CHADEMA kikipata nafasi 10, wakati wajumbe wa serikali za mitaa CCM kilijipatia wajumbe 92 na CHADEMA 46.
Katibu wa CHADEMA wa Wilaya ya Chato, Mange Sai, alisema ushindi uliopatikana ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa wilaya hiyo kwa kuwa baadhi ya vitongoji CHADEMA ilipitisha wagombe pasipo kuwa na upinzani wa chama tawala jambo ambalo linaonyesha wazi kukubalika kwa chama hicho kwa wananchi.
Alisema kuwa CHADEMA kilitegemea kuibuka kidedea katika uchaguzi huo mdogo kutokana na wapiga kura kuchoshwa na ahadi mbalimbali za serikali ya CCM ambazo zimekuwa hazina utekelezaji na badala yake baadhi ya viongozi wamekuwa wakijinufaisha kwa maslahi yao binafsi huku wakiwaacha wananchi wakitaabika.
0 maoni:
Post a Comment