Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali –CAG Ludovick Utoh amesema deni la taifa limeongezeka kwa asilimia 38 kutoka trilioni 10.5 mwaka 2010 mpaka trilioni 14.4 mwaka 2011 kwa mujibu wa taarifa ya ukaguzi ya mwaka 2010/2011.
Deni hilo limeongezeka kutokana na hatua ya serikali kukopa kwenye mabenki ya ndani na nje ya nchi kwa minajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akisoma taarifa ya mwaka 2010/2011 ya ukaguzi wa hesabu za serikali kuu, serikali za mitaa na mashirika ya umma CAG Utoh alisema, mbali na kuongezeka kwa deni hilo lakini pia serikali imepoteza zaidi ya shilingi trilioni 1.2 kutokana na misamaha isiyo ya lazima ya kodi.
Kwenye ukaguzi wa serikali za mitaa CAG alizitaja halmashari za Arusha, Songea, morogoro, Kilindi na Misungwi kuwa na hati zisizoridhisha.
Kwa upande wa ukaguzi wa mashirika ya umma Bwana Utoh amesema, ofisi yake imegundua usimamizi mbovu kwenye uendeshaji wa chuo kikuu chaDodoma– UDOM na kwamba majengo ya chuo hicho hayana hati miliki.
Wakizungumzia ukaguzi huo wenyeviti wa kamati tatu za bunge zinazosimamia mapato ya serikali na mashirika yake wameelezea kusikitishwa na hali ya matumizi mabovu kwenye taasisi hizo.
Hata hivyo CAG alishindwa kueleza matokeo ya ukaguzi maalumu wa shirika la usafiri Dar es salaam – UDA kutokana na kutopata kibali kutoka kwa waziri mkuu aliyemuagiza kufanya ukaguzi huo.
Published by Radio Free Africa (Habari za Kitaifa)on 13th April 2012
0 maoni:
Post a Comment