Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

CHADEMA wapinga mchakato wa ubunge Afrika Mashariki

Na Tamali Vullu, Dodoma

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepinga uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Jumuia ya Afrika Mashariki kutokana na mchakato unaoendelea kutokuwa huru na wa haki.

Kutokana na hali hiyo, chama hicho kimemtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah na serikali kuchukua hatua za haraka kurekebisha kasoro zilizojitokeza, ili kuhakikisha uchaguzi huo unawezesha wabunge kupatikana kidemokrasia na kwa kuzingatia masilahi ya umma.

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alizungumza na vyombo vya habari jana akisema kutokana na hali hiyo chama chake kimemwandikia Spika na Katibu wa Bunge kusitisha uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Jumanne ijayo.

Katika uchaguzi huo, CCM ina nafasi ya wagombea wanane na vyama vya upinzani mgombea mmoja.

Alisema uteuzi wa wagombea katika uchaguzi huo haukufanywa kwa kuzingatia uwiano wa vyama vyenye wabunge.

Alisema kulingana na idadi ya wabunge wa CCM (258), chama hicho kilistahili kupata viti visivyozidi saba, lakini wamepewa vinane na vyama vya upinzani kwa ujumla wake vinagombea kiti kimoja.

“Kwa kuzingatia ibara ya 50 ya mkataba wa Afrika Mashariki na uwakilishi wa vyama vyenye wabunge, CCM ilistahili kupata viti visivyoziti saba, CHADEMA chenye wabunge 48, kilistahili kupata kiti kimoja na chama cha CUF chenye wabunge 36 kilistahili kupata kiti kimoja,” alisema Mnyika.

Alisema mchakato wa uchaguzi huo unaoendelea si wa haki, hivyo kasoro zilizopo zinapaswa kurekebishwa ili wabunge hao wapatikane kidemokrasia na kwa kuzingatia masilahi ya umma.

Aidha, alisema kanuni za uchaguzi huo zinakinzana na mkataba wa Afrika Mashariki, hivyo kanuni zinazotumika katika uchaguzi huo ni batili.

Pamoja na hayo, aliwashauri wadau wote kufuatilia kwa karibu uchaguzi huo, kwani ni muhimu kwa taifa kwa kuwa unahusu uwakilishi wa nchi katika chombo muhimu cha kuwakilisha wananchi.

Alisema kutokana na hali hiyo, wameiomba kamati ya kanuni kuitishwa kwa dharura kwa lengo la kurekebisha kanuni za uchaguzi kabla ya kuitishwa kwa uchaguzi huo.

Aidha, alisema kwa mujibu wa Katibu wa Bunge ambaye ni msimamizi wa uchaguzi, uteuzi wa wagombea ulipaswa kufanyika Aprili 10, lakini uteuzi wa wagombea hao umetangazwa jana.

Katika hatua nyingine, Ofisi ya Bunge imeteua wagombea ubunge 33 wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki huku ikimuengua mgombea mmoja baada ya kushindwa kutimiza masharti ya uchaguzi huo.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Katibu wa Bunge, Thomas Kashilillah, ilieleza mgombea aliyeenguliwa ni Mohamed Dedes, baada ya kushindwa kutimiza masharti ya uchaguzi huo – kuthibitisha uraia wake pamoja na kulipa ada ya uchaguzi.

Aliwataja wagombea waliopitishwa katika kundi la wagombea wanawake kuwa ni Angela Kizigha, Fancy Nkuhi, Dk. Godbertha Kinyondo, Janet Mmari, Janet Mbene, Maryam Yahya, Sebtuu Nassor, Shy-Rose Bhanji na Sofia Rijaal wote kutoka CCM na Rose Mwalusamba kutoka CUF.

Alisema wagombea kutoka Zanzibar walioteuliwa ni Abdullah Ali Hassan Mwinyi, Dk. Ahmada Hamad Khatib, Dk. Haji Mwita Haji, Khamis Jabir Makame, Dk. Said Gharib Bilal na Zubeir Ali Maulid, wote akutoka CCM.

Wagombea wa vyama vya upinzani walioteuliwa ni Anthony Komu (CHADEMA), Dk. Fortunatus Lwanyantika Masha (UDP), Micah Mrindoko (TLP), Twaha Taslima (CUF) na Juju Danda, Mwaiseje Polisya na Nderakindo Kessy, wote kutoka NCCR-Mageuzi.

Wagombea wa Tanzania Bara ni Adam Kimbisa, Bernard Murunya, Charles Nyerere, Dk. Edmond Mndolwa, Elibariki Kingu, Dk. Evans Rweikiza, Mrisho Gambo, Siraju Kaboyonga na William Malecela, wote kutoka CCM na John Chipaka (TADEA).

Chanzo: Tanzania Daima

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO