WAZIRI Mkuu, Mh Mizengo Pinda amejikuta katika wakati mgumu katika kipindi cha maswali na majibu ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu Bungeni leo asubuhi pale alipotakiwa kueleza kama ni kweli Serikali yake ina sera za ubaguzi wa maeneo ambayo wananchi wameamua kuchagua upinzani nchini.
Swali hili limebuliwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mh Freeman Mbowe alietaka kujua kauli ya serikali kuhusiana na kauli nyingi ambazo zimekuwa zikitolewa na viongozi wa juu wa Serikali nchini zinazopandikiza ubaguzi na chuki kwa wananchi, kwamba maeneo ambayo upinzani umechaguliwa hawatapata fedha za mgao kwa miradi ya maendeleo.
Akijibu swali hilo kwa mara ya kwanza, Waziri Mkuu Pinda alisema sio kweli kwamba kuna kauli za namna hiyo na kusisitiza kuwa hakuna mahali nchini Serikali haijapeleka fedha za mgao iwe ni kwa Majimbo ya CHADEMA, CUF, CCM au chama chochote kingine.
“Kwanza nioneshe masikitiko yangu. Swahi hili limeulizwa kiujumla kana kwamba ni jambo la kweli wakati hata yeye (Mbowe) anajua si la kweli. Hakuna mahali hatujapeleka fedha… (za mgao)” alisema Pinda.
Baada ya kutoa majibu hayo, Mh Mbowe alisimama na kuuliza swali la nyongeza akitaka kujua Waziri Mkuu atachukua hatua gani kwa mawaziri waliotoa kauli hizo endapo atathibitisha, na kisha akawataja kwa majina na maeneo walipotoa kauli hizo zinazoashiria ubaguzi wakiwa kama viongozi wa Serikali ambayo inawajibika kwa wananchi wote.
Mh Mbowe amemtaja Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwezeshaji, Dk Mary Nagu kuwa wakati akimnadi mgombea wa CCM, Sioi Sumari katika uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Arumeru mkoani Arusha alitoa kauli za ubaguzi.
Mh Nagu katika kampeni hizo zilizohitimishwa na uchaguzi wa Aprili 1, 2012, aliwaambia wananchi kwamba wakimchagua mgombea wa CCM (Sioi Sumari) Serikali itawapa maendeleo, lakini wakimchagua mpinzani yeye (Waziri Nagu) hatampa ushirikiano na atakuwa akimkwepa.
Kwa kifupi ni kwamba Waziri Nagu alisema kupitia wizara yake ya Uwezeshaji na Uwekezaji kama atachaguliwa Sioi, ofisi yake itaharakisha maendeleo katika eneo hilo kwa kujenga Eneo Maalumu la Uzalishaji kwa Mauzo ya nje (EPZ), Kata ya Mbunguni katika jimbo hilo ambalo litasaidia wakulima kuuza mazao yao ya mbogamboga na matunda.
Mbowe amemtaja waziri mwingine, Dr John Pombe Maghufuli na kueleza kuwa akiwa Igunga kwenye kampeni za Uchaguzi Mdogo Jimbo la Igunga uliofanyika mwezi Oktoba mwaka jana nae alitoa kauli za namna hiyo.
Waziri wa Ujenzi Dakta Maghufuli aliwataka wananchi wa Igunga mkoani Tabora kutodanganyika na ahadi uchwara za ujenzi wa Daraja la Mto Mbutu, ahadi ambazo alidai zilikuwa zikitolewa na wagombea wa vyama vya Upinzani na kwamba ni yeye na Serikali yeye pekee kama Waziri mwenye dhamana ndio watakaoamua.
Dakta Maghufuli alitoa kauli hiyo wilayani Igunga katika Viwanja vya Saba saba wakati alipokuwa akimnadi Mgombea wa CCM Dakta Dalaly Kafumu kwa wapiga kura wa Jimbo la Igunga, ambae baadae aliibuka mshindi katika uchaguzi huo.
Waziri mwingine alietajwa na Mh Mbowe kutoa kauli kama hizo Jimboni Arumeru Mashariki ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ambae pia ni Mbunge wa Arumeru Magharibi, Mh Goodlucky Ole Medeye
Safari hii, baada ya kutolewa uthibitisho huo na Mh Mbowe, Waziri Mkuu alilazimika kuwa mpole na kukubaliana Mh Mbowe juu ya kauli hizo za viongozi wa Serikali bila kutamka kama ni kweli au hapana.
Pinda alisema kauli hizo kama zimetokea kwenye kampeni ni mambo ya bahati mbaya tu na kuahidi kuwa Serikali yake itaendelea kufuata sheria katika utekelezajai wa mpango yake.
“Watanzania tujenge demokrasia yetu ambayo bado ni changa. (Serikali) tunasimamia sheria bila upendelao. Kama kuna kauli kwenye kampeni ni mambo unfortutane (hayakukusudiwa)..tutaendelea kufuata utawala wa sheria” alisema Pinda
Kwa rekodi zilizopo nchini, kumekuwepo na kauli hizi za kuwabagua wananchi toka kwa viongozi wa Serikali, kauli hizo sio tu zinaonyesha ubaguzi, bali zinawatisha na kuwafanya wananchi wajihisi kuwa watumwa katika nchi yao wenyewe.
Kwa mfano, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye wakati akiwa waziri Mkuu katika utawala wa awamu ya tatu, aliwahi kukaririwa akisema ukitaka kufanya biashara lazima uingie CCM na ukitaka kuwa masikini ingia vyama vya upinzani.
Baada ya hapo zimekuwepo kauli nyingine nyingi zilizoendelea kutolewa na viongozi wa juu wa Serikali kuhusu vitisho vya kuwatenga au kuwanyima maendeleo endapo wataisaliti CCM ambayo ni chama tawala.
Kauli nyingine iliyowahi kutolewa siku za nyuma na baadhi ya viongozi wa Serikali ni kwamba msiwachague wagombea wa upinzani kwa sababu hawana Serikali, hivyo hahawezi kuwapatia maendeleo.
Baadhi ya wananchi waliotoa maoni yao kuhusiana na kauli hizi wamesema hizi ni dalili kuwa sasa Serikali inaanza kunajisi demokrasia nchini na hata kuvunja Katiba inayosema kila mtu ana haki ya kuchagua au kuchaguliwa kuongoza. Lakini pia kauli hizi ni za kuwafunga minyororo wananchi na kulazimishwa kuchagua mtu anayemtaka kiongozi wa Serikali hata kama wao hawamtaki.
Wanasema, kama utamaduni huu ambao umeanza kuonyeshwa na viongozi na mawaziri wetu ukiendelea ni wazi, sasa Serikali inaelekea kwenye udikteta.
Maelezo ya ziada: Julius Magodi (juliusmagodi@yahoo.com), Mwananchi Jumapili, 25 Machi, 2012
0 maoni:
Post a Comment