Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

CHADEMA yanasa wasaliti, Shonza, Mchange, Mwampamba watimuliwa BAVICHA

Pichani ya Maktaba kwa hisani ya Jamii Forum: Mbunge wa Maswa Mgaharibi (CHADEMA) Mh John Shibuda pamoja na Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM Ndg Nape Nnauye wakinong’onezana  jambo

na Mwandishi wa Gazeti la Tanzania Daima

MBUNGE wa Maswa Magharibi, John Shibuda (CHADEMA), amekalia kuti kavu kutokana na kutajwa kuwa anafadhili baadhi ya viongozi wa Baraza la Vijana Taifa la CHADEMA (BAVICHA) kuleta mgogoro ndani ya chama hicho.

Siri hiyo ilifichuliwa juzi na baadhi ya vijana hao walipokuwa wakijitetea mbele ya kikao cha BAVICHA ili kuthibitisha tuhuma zilizokuwa zikiwakabili za kutumika kuwachafua viongozi wakuu wa CHADEMA.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya kikao hicho zilisema kuwa mmoja wa vijana hao, Fred Hatari, ambaye ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Wanachama wa CHADEMA Vyuo Vikuu (Chaso), alitoa ushuhuda mbele ya Kamati Tendaji ya BAVICHA kuwa Shibuda amewahi kumwita mara kadhaa na kumpa fedha ili atoe matamko ya kuchafua viongozi wa chama.

Huku akionesha ujumbe kadhaa wa simu yake ya mkononi (sms) aliyodai kutumiwa na Shibuda, mwenyekiti huyo aliiambia kamati kuwa amekutana zaidi ya mara mbili na mbunge huyo na kupewa fedha ili akatoe matamko sehemu tofauti ya kumpinga Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, na kusema kuwa ana kadi ya CCM.

“Fred aliamua kusema ukweli mbele ya kamati yetu, akaomba asamehewe kwa maelezo kuwa alifukuzwa Chuo Kikuu kwa kutetea haki, na kwamba alikuwa akiishi kwa kutangatanga, ndiyo maana alikubali kupokea fedha ya Shibuda, lakini alikataa kumkashifu Katibu Mkuu,” kilisema chanzo chetu.

Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa, John Heche, alipoulizwa jana kuhusu sakata hili, alikataa kusema chochote kuhusiana na kikao chao, akisisitiza kuwa anapanga mkutano na waandishi wa habari ambao atautumia kuweka wazi ukweli na ushahidi wote alionao.

BAVICHA iliunda kamati ndogo ya kuchunguza mgongano uliokuwepo baina ya viongozi wake na hivyo kumteua Mwenyekiti wa baraza hilo Mkoa wa Singida, Josephat Isango, kuwa mwenyekiti.

Baada ya kamati hiyo kuwasilisha ripoti yake juzi, baraza hilo lilifanya uamuzi mgumu wa kuwafukuza baadhi ya viongozi wake akiwemo Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa, Juliana Shonza na kuwasimamisha baadhi ya wanachama.

Katika kikao hicho ambacho kilijumuisha wenyeviti wa mikoa yote ya kichama nchi nzima, Shonza hakuhudhuria badala yake alituma barua akidai kuwa nje ya Dar es Salaam kwa shughuli za kifamilia.

Makamu mwenyekiti huyo amekuwa akidaiwa kusigana kimaamuzi na viongozi wenzake, na hivyo kutoa matamko ambayo wakati mwingine yalikuwa yakikinzana na msimamo wa chama.

Chanzo chetu kilifafanua kuwa, baada ya ripoti ya kamati ya uchunguzi kusomwa, sekretariati ya BAVICHA ilitoa mapendekezo yake kuunga mkono mapendekezo ya kamati na kisha wakaletwa mashahidi wengine waliokuwa nje ya kikao ili kuthibitisha kama yaliyosemwa ni ya kweli au la.

Katika ushahidi uliotolewa, Shonza alibainika kuwa huwa anatumiwa na Shibuda kutafuta vijana wengine wapokee fedha ili watoe matamko ya kukifedhehesha chama.

Baada ya tuhuma hizo kuthibitishwa na kujadiliwa na wajumbe, kura zote ziliazimia kuwa aondolewe uongozi na kusimamishwa uanachama wa BAVICHA.

Wengine waliotuhumiwa kushirikiana na Shonza ni waliokuwa wagombea ubunge mwaka 2010 katika majimbo ya Kibaha Mjini (Habib Mchange) na Mbozi Mashariki (Mtera Mwampamba) ambao pia wamefukuzwa uanachama wa BAVICHA.

Kikao hicho pia kilichukua uamuzi mgumu wa kuwasimamisha uanachama kwa muda wa mwaka mmoja, Gwakisa Mwakisando (Mbeya), Wilson Makala (Babati) na Joseph Kasambala (Mbeya).

Alipotafutwa na gazeti hili jana jioni kwa simu, Shibuda alikanusha kuhusika na tuhuma hizo akisema kuwa hata kijana huyo (Fred) hamfahamu.

“Hivi wewe nikikwambia Shibuda ni baba yako utakubali? Mnapaswa kujiridhisha na uzushi huo, mimi sijui mambo ya BAVICHA maana si mjumbe huko na sikuwahi kutumia fedha kumchafua Dk. Slaa kwani sina ugomvi naye,” alisema.

Aliongeza kuwa hapendi siasa za udaku na chuki, na akaahidi kulifuatilia suala hilo, huku akidai kuwa kuna watu wanataka kumchafua bila sababu.

CHANZO: TANZANIA DAIMA 7 JAN 2013

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO