Wiki hii imekuwa ya majonzi kwa baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki wa familia mbili za wanachadema Moshi na Arusha baada ya kutokea misiba miwili tofauti, msiba mmoja ukihusisha familia ya ndugu wa muasisi wa CHADEMA, Mzee Edwin Mtei na mwingine kwa familia ya mgombea wa CHADEMA Arumeru Mashariki, Joshua Nassari.
Taarifa zinaeleza kuwa mtoto wa mdogo wake na Mzee Mtei alifariki dunia Machi 14 kwa jali ya gari maeneo jirani na Karanga Moshi, na kaka yake alietambulika kwa jina moja la Aaron alikimbizwa Nairobi kwa matibabu baada ya kuvunjika vibaya miguu yote miwili. Inaelezwa kuwa Aaron ndie alikuwa dereva wa gari hiyo na walikuwa wakielekea KCMC kushughulikia maiti ya jamaa yao mwingine.
Nako Jimboni Arumeru Mashariki ambako kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge zinaendelea, Mgombea wa CHADEMA, Joshua Nassari alifiwa na Baba yake Mdogo, Elisa Nassari.
Maziko ya Elisa yalifanyika Machi 15 na kupelekea chama hicho kuamua kuahirisha mikutano yake ya kampeni kwa siku hiyo iliyopaswa kufanyika katika maeneo ya King’ori, Maroroni na Makiba.
Mapema kabla ya kwenda kwenye mazishi hayo, mgombea huyo na timu zima ya kampeni walikwenda Hospitali ya Nkoaranga ambako walitembelea wagonjwa katika wodi mbalimbali kuwatakia uponaji wa haraka na afya njema. Katika ziara hiyo pia waliweza kufika katika kituo cha watoto yatima cha Nkoaranga kinachohudumiwa na hospitali hiyo na kujumuika nao kwa muda.
Blog ya jamii, “Arusha Yetu” inawapa pole wafiwa wote na kuwatakia majeruhi wote nafuu na kupona haraka ili waweze kendelea na shughuli zao za kila siku! Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali pema peponi.
0 maoni:
Post a Comment