Mh Highness Samson Kiwia (katikati) akisalimiana na mwananchi wakati akitoka nje ya Ukumbi wa Mahakama sambamba na Wakili wake Mh Tundu Lisu (kushoto) aliyesimamia kidete kesi hiyo na kuibuka washindi.
HATIMAYE Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, imetoa hukumu katika kesi ya kupinga matokeo ya ushindi wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela Jijini Mwanza, Highness Samson Kiwia (Chadema), iliyofunguliwa na walalamikaji watatu, ambapo mbunge huyo ameibuka kidedea kwa kushinda kesi hiyo ya madai.
Mbali na Mbunge Kiwia kushinda kesi hiyo namba 12/2010 iliyofunguliwa na walalamikaji, Yusuph Masengeja Lupilya, Nuru Ramadhani Nsubuga na Beatus Martin Madenge, Mahakama hiyo imewaamuru walalamikaji hao watatu kulipa gharama zote za kuendeshea kesi zilizotumiwa na mbunge huyo wa Chadema.
Hukumu hiyo imetolewa leo na Jaji Gadi Mjemas kutoka Mahakama ya Bukoba Mkoani Kagera, ambapo mamia ya watu walifurika mahakamani hapo kusikiliza hukumu hiyo iliyoanza kusomwa na Jaji majira ya saa 3:30 asubuhi hadi saa 4:58.
Akisoma kwa umakini na utulivu mkubwa hukumu hiyo iliyoonekana kuwa na zaidi ya kurasa 15 hivi, Jaji Mjemas aliyekuwa amevalia joho lenye michirizi nyekundu na nyeupe, alikuwa akisoma madai na ushahidi uliotolewa mahakamani dhidi ya walalamikaji pamoja na utetezi uliotolewa mahakamani hapo na Mbunge Kiwia kupitia wakili wake maarufu nchini, Tundu Lisu.
Kwa mujibu wa Jaji Mjemas, kesi iliyofunguliwa na walalamikaji hao watatu ni halali na hatua zote za kisheria zimechukuliwa na mahakama hiyo kama zinazochukuliwa katika kesi nyingine zozote zile.
Walalamikaji hao watatu walikuwa wakiiomba mahakama hiyo itengue ushindi wa mbunge huyo wa Ilemela, Kiwia, kwa madai kwamba alishinda pasipo halali, kwani wapiga kura 114,085 wakiwemo wana CCM walizuiliwa na wafuasia wa Chadema kwenda kupiga kura katika vituo halali vilivyotengwa na Tume ya Uchaguzi nchini (NEC), hivyo kusababisha aliyekuwa mgombea wa CCM Jimbo hilo la Ilemela, Anthony Mwandu Diallo kushindwa katika uchaguzi huo.
Pia walalamikaji hao walikuwa wakidai kwamba watu ambao hawakupiga kura Jimbo la Ilemela siku hiyo ya Uchaguzi ni 114,085, kati ya watu 175,978 waliojiandikisha kupiga kura ambapo waliopiga kura halali ni 61,893 pekee, na kwamba anaamini idadi ya watu ambao hawakupiga kura ilitokana na kuzuiwa na vijana 200 anaoamini ni wafuasi wa Chadema.
“Katika hati ya mashtaka ya walalamikaji, akiwemo shahidi wa kwanza wa upande wa wadai, Beatus walisema siku ya uchaguzi wao walipiga kura kwa halali. Hati hiyo waliiandika wao na kuisaini…lakini baadaye shahidi huyu Beatus aliikana hati hiyo mbele ya mahakama akidai eti hakupiga kura halali siku hiyo.
“Shahidi huyu Beatus aliiambia mahakama kwamba wapiga kura 114,085 walitishwa na kuzuiliwa kupiga kura. Lakini wakili Tundu Lisu alimuomba shahidi huyo atoe ushahidi lakini Beatus akashindwa kuithibitishia mahakama hii.
“Pia Tundu Lisu alipomuuliza shahidi huyo wa kwanza kuieleza mahakama hii iwapo kuna sheria yoyote inayowalazimu Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ilemela kueleza sababu za watu ambao hawakwenda kupiga kura siku ya uchaguzi, shahidi alishindwa kuthibitisha. Kwa maana hiyo mahakama imeona walalamikaji hawakuwa na ushahidi unaojitoshereza”, alisema Jaji Mjemas.
Hata hivyo, Jaji huyo alibainisha kwamba, mahakama yoyote ile haitoi maamuzi kwa ushahidi usiojitoshereza, bali maamuzi sahihi huwa yanatolewa pale ushahidi unapothibitika kwamba ni kweli ama si kweli, na kwamba, iwapo walalamikaji wangewasilisha ushahidi wao unaothibitisha ukweli wa madai yao, mahakama hiyo ingeweza kusema wameshinda, lakini kwa sasa ushahidi wao hauiridhishi mahakama hiyo.
Kufuatia maelezo marefu yaliyosomwa mbele ya mahakama hiyo, Jaji Mjemas alihitimisha kusoma hukumu hiyo kwa kusema kwamba: “Kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa na walalamikaji pamoja na upande na maelezo ya wa wadaiwa, mahakama hii inatupilia mbali mashtaka haya, na walalamikaji wanapaswa kulipa gharama zote za kesi hii”.
Akizungumzia ushindi wake huo, Mbunge Kiwia alieleza kufurahishwa na maamuzi ya kweli yaliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, na kusema huo ni ushindi wa kihistoria katika Taifa hili, na aliahidi kuwafungulia kesi ya kuwadai gharama zote waliokuwa walalamikaji wa kesi hiyo, ambao ni Lupilya, Nsubuga pamoja na Madenge.
“Kwa kweli huu ni ushindi wa kihistoria kwa nchi hii ya Tanzania. Lakini naamini kesi ni gharama na nitawafungulia kesi hawa watu ili walipe gharama zote nilizotumia. Nitakaa na mwanasheria wangu Tundu Lisu tuone ni gharama kiasi ghani tumetumia”, alisema Mbunge Kiwia huku akishangiliwa na mamia ya wafuasi wake.
Chanzo: website ya fikarapevu
0 maoni:
Post a Comment