Mashine maalumu ya kutengeneza matiti
BIASHARA huria imezua mengi. Hali kadhalika Sayansi na Tekenolojia nayo, imeleta mengi. Katika kuwaondolea kero wanawake wenye matiti yaliyosinyaa hapa nchini, wataalamu kutoka China wameanza kutoa huduma ya kunyanyua matiti hayo kwa kutumia mashine maalumu.
Wachina wamejipatia umaarufu katika kuleta bidhaa mbalimbali hapa nchini, zikiwamo za kuongeza nguvu za kiume, kupunguza uzito, kuotesha nywele, kujichubua (kumfanya mtu mweusi awe mweupe), kuongeza makalio nk.
Huduma hiyo ya kusimamisha matiti yaliyolala, imeanza kutolewa katika Saluni ya Blue Palace, iliyopo nyuma ya Shule ya Mapambano, Sinza jijini Dar es Salaam.
Haikuwa rahisi kuweza kuamini kuwa vitu kama hivi vinaweza kupatikana Tanzania. Mwananchi Jumapili lilifunga safari mpaka kwenye saluni hiyo inayomilikiwa na Sarafina Mtweve, kujionea jinsi teknolojia hiyo inavyofanya kazi.
Mbali na meneja wa saluni hiyo, Trust Mwembe, pia alikuwepo mtaalamu kutoka China aitwaye, Ciisy Pang, ni binti wa miaka 23 tu, lakini anasema kwa miaka minne amefanya kazi hiyo na kuwasaidia wanawake mbalimbali waliokuwa wakikerwa na matiti yaliyolegea au kuanguka.
Pang na kundi lake wanatoa huduma hii kwa gharama ya Sh150,000 kwa kuanzia, ingawa wanahisi gharama hizo zitapanda katika siku chache zijazo.
Jinsi matiti yanavyosimamishwa
Mashine hiyo inayoitwa ‘Beauty Machine’ ina uwezo wa kusimamisha matiti ya kila saizi kwa kuwa huambatanishwa na vibakuli (cups) kama unavyoona pichani.
Kazi kubwa ya mashine hiyo ni kuamsha misuli ambayo hushikilia nyama za matiti.
Pang anasema, zoezi la kusimamisha matiti huchukua wiki tatu mpaka sita, inategemea aina ya mteja na wakati mwingine juhudi zake.
Chanzo: Julieth Kulangwa, Mwananchi Habari
0 maoni:
Post a Comment