Orodha ya majina ya wapigakura katika uchaguzi mdogo wa ubunge Arumeru Mashariki ilibandikwa jana asubuhi zikiwa zimebaki siku nane kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo.
Wananchi walianza kujitokeza mara tu baada ya orodha kubandikwa ili kuhakiki majina yao na pia kutambua vituo ambavyo wamepangwa kwa ajili ya kupigia kura.
Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Trasias Kagenzi, alisema jana kuwa katika muda huo wa siku nane, ofisi yake itakuwa wazi kwa ajili ya kushughulikia matatizo madogomadogo yatakayojitokeza.
Msimamizi huyo alisema watashughulikia wale wenye vitambulisho tu, na wale wasiokuwa navyo wasubirimaboresho ya daftari la kudumu la wapiga kura. “Ndiyo maana tumeweka muda wa siku nane, ni muda wa kutosha kwamba hata tatizo likijitokeza na kuhitaji msaada wa makao Makuu ya Tume ya Uchaguzi (NEC), basi ni rahisi kuwasiliana nao na kupata msaada. Watumie fursa hiyo wasisubiri siku ya kupiga kura” aliongeza Kagenzi
Katika hatua nyingine, Kagenzi alisema orodha ya vituo vya kupigia kura imefanyiwa marekebisho na kuondoa kasoro ambazo zilizua malalmiko kutoka kwa CHADEMA kwamba kuna vituo hewa 55.
Alisema tayari orodha sahihi yenye vituo 327 vya kupigia kura imetolewa rasmi kwa vyama vyote vya siasa, ili kuondoa malalmiko ambayo yamekuwa yakijitokeza kutoka kwa vyama vya siasa.
“Vyama vyote nimevitumia orodha hiyo, hiyo ni taarifa rasmi na wala siyo siri..” alisema kagenzi kwa simu
Mkuu wa operesheni wa Kampeni wa CHADEMA Jimboni Arumeru Mashariki, John Mrema, alikiri chama chake kupokea orodha hiyo ya vituo vya kupigia kura.
Dondoo za Uchaguzi Mdogo Arumeru Mashariki
1. | Idadi ya wapigakura | |
Kabla ya marekebisho | 127,249 | |
Baada ya Marekebisho ya NEC | 127,455 | |
Majina yaliyoondolewa | 28 | |
Majina yaliyoongezwa | 54 | |
2. | Idadi ya Kata | 17 |
3. | Idadi ya Vijiji | 74 |
4. | Idadi ya Vituo vya kupigia kura | 327 |
5. | Idadi ya wagombea | 8 |
6. | Idadi ya watakaopiga kura | 127,455 |
Chanzo: Mwananchi Habari, Machi 24 2012
0 maoni:
Post a Comment