Published by Fikra Pevu – yesterday, March 30, 2012
Aliyekuwa Waziri Mkuu Bw. Edward Lowassa leo amejikuta katika wakati mgumu baada ya msafara wake kuzomewa na mamia ya wananchi wa Arumeru wakati akitoka kuhutubia mkutano wa kampeni kumnadi Bw. Siyoi Sumari kama mgombea wa Ubunge katika uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki.
Akihutubia mkutano huo uliofanyika kwenye uwanja wa Patandi Bw. Lowassa alitangaza “kufungwa” kwa ajenda mbalimbali ikiwemo ile ya tatizo la ardhi, maji na umeme. Lowassa alikiri kuwa serikali ya chama chake haijaitikia vizuri na kushughulikia matatizo ya wana Arumeru na kuwa uchaguzi huu mdogo umewapatia CCM nafasi ya kujua kwa undani kero za Arumeru Mashariki.
“Lazima tukiri (tatizo la ardhi) hatukulishughulikia vya kutosha” amesema Bw. Lowassa akielezea kuwa tatizo hilo ambalo limedumu tangu 1951 hadi 1961 tulipopata uhuru na limeendelea kudumu kuanzia wakati huo hadi leo hii. “Kwa uchaguzi huu tunafunga ajenda ya matatizo ya mashamba ya Arumeru” amesema Bw. Lowassa ambaye licha ya kuwahi kuwa Waziri Mkuu aliwahi kuwa Waziri wa Ardhi, na Maendeleo ya Makazi. katika serikali ya Rais Ally Hassan Mwinyi kati ya mwaka 1993 hadi 1995.
Akizungumzia tatizo la maji Bw. Lowassa amesema kuwa ni kweli watu wa Monduli wanapata maji kutoka Arumeru na hilo lilifanyika wakati wa Sokoine. Ameelezea pia kuwa wakati wake wamechimba visima Monduli kwani aliogopa kuja Arumeru kuchukua maji. Hata hivyo, Lowassa hakuwaambia wananchi wa Arumeru Mashariki yeye alifanya nini wakati akiwa Waziri wa Maji kwa miaka mitano chini ya serikali ya Rais Mkapa kati ya 2000 na 2005.
Akionesha usahaulifu kuwa serikali ya Chama chake ndio imekuwa madarakani kwa miaka hamsini huko Arumeru Mashariki Bw. Lowassa alidai kuwa uchaguzi huu mdogo ndio umewapatia CCM na serikali nafasi ya kujua kero za wananchi kana kwamba chama chake kilipowasimamisha wabunge katika chaguzi kumi zilizopita hawakujua kero hizo.
Lowassa akishangiliwa na watu wachache waliofika kwenye mkutano huo aliahidi kuwa endapo wananchi wa Arumeru Mashariki watamchagua Siyoi basi tarehe 10 Aprili, 2012 yeye na wabunge wengine wa Arusha (akiwemo Siyoi –kama atachaguliwa) wataenda kukutana na Waziri wa Ardhi Prof. Anna Tibaijuka kuhusiana na matatizo hayo ya ardhi.
Pamoja na majaribio ya hapa na pale ya kuwahamasisha wahudhuriaji wake mkutano wa Lowassa haukuwa na msisimko mkubwa kama ilivyotarajiwa hasa baada ya kuwa na wasiwasi endapo angepanda jukwaani au la. Mkutano wake ulihudhuriwa na wabunge wengine wa CCM pamoja na viongozi mbalimbali wakiwemo Wilson Mukama, Nape Nnauye na viongozi wa kampeni ya CCM jimboni humo.
Hata hivyo kimbembe cha Lowassa leo ni zomea zomea ya mamia ya wananchi waliokuwa wamejipanga kwenye barabara mbalimbali wakionesha alama ya vidole viwili ambavyo hutumiwa na Chama Kikuu cha Upinzani nchini –CHADEMA – ambacho nacho kinagombania jimbo hilo kwa kumsimamisha aliyekuwa mgombea wao mwaka 2010 Bw. Joshua Sumari.
Mamia ya watu walijipanga kuanzia maeneo ya Sanawari mjini Arusha ambapo kote kote walikuwa wamevaa mavazi ya rangi za CDM huku wakipunga alama “V” kwa vidole vyao kuuelekezea msafara wa viongozi wa CCM akiwemo Bw. Lowassa. Hata hivyo baadhi ya wachunguzi wamesema kuwa zomea zomea hiyo haina maana yoyote hasa kama wazomeaji hawatojitokeza kupiga kura kwani kinachoangaliwa siku ya Jumapili ni “nani amepata kura nyingi siyo nani alizomewa zaidi”.
Kwa maoni ya baadhi ya viongozi wa CHADEMA kuhusiana na kushindwa kwa Bw. Lowassa kuelezea jitihada zake kama Waziri wa sekta hizo muhimu kumeonesha ni jinsi gani ahadi zake leo chama cha mapinduzi hakina mikakati ya kweli ya kutatua kero hizo. “Lowassa leo anazungumzia matatizo ya ardhi na maji Arumeru wakati amewahi kushika nafasi zote muhimu kuhusiana na suala hili ni kichekesho na kejeli ya mwaka” amesema Dr. Slaa akizungumza kufuatia kuhitimishwa kwa mkutano wa Lowassa.
“Wananchi wa Arumeru hawadaganganyiki tena; kama mtu aliyewahi kuwa Waziri wa sekta hizo tena na baadaye waziri mkuu hakufanya lolote iweje leo waweke tumaini lao kwa kijana ambaye hana cheo au uongozi wowote kuwa ati matatizo yataondolewa?” alihoji Dr. Slaa.
Vyama vyote vya siasa vinahitimisha kampeni zao kesho Jumamosi katika maeneo mbalimbali ambapo mkutano wa kufunga Kampeni wa CCM utaongozwa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Bw. Benjamin Mkapa wakati ule wa CDM unatarajiwa kufungwa na Dr. Slaa. Huko Mwanza – Kata ya Kirumba Zitto Kabwe anatarajiwa kufunga kampeni wakati Dar-es-Salaam Bw. Mnyika anatarajiwa kufanya hivyo hivyo.
NOTISI YA MHARIRI:
Kwa wananchi wa Arumeru Mashariki – tuma MATOKEO YA UCHAGUZI kwa kadiri utakavyoweza kupata kutoka vituo mbalimbali kwenda support@jamiiforums.com au kwa kuingia kwenye mtandao wa Facebook wa “Jamiiforums” ambapo tutayarusha matokeo hayo moja kwa moja.
Na. M. M. Mwanakijiji na Waandishi wa Fikra Pevu Arumeru
0 maoni:
Post a Comment