Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Dr Slaa Kuunguruma Leo Arumeru

Reg9 Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa leo anatarajia kuunguruma katika kampeni za chama hicho, ili kuongeza nguvu za kumnadi mgombea wa chama hicho Joshua Nassari.

Ofisa habari wa Chadema, Tumaini Makene, alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Arumeru Mashariki mkoani Arusha jana.

Alisema Dk Slaa ataongeza nguvu kwa kampeni hizo ambazo Chadema inaamini kuwa CCM wanatumia lugha za kashfa na matusi dhidi ya Nassari badala ya kutangaza sera na ilani ya chama chao.

Makene alisema nguvu za Dk Slaa zitaelekea katika kuuelimisha umma kuhusu manufaa ya kumchagua Nassari wa Chadema na hasara watakazozipata ikiwa mgombea kupitia CCM, Sioi Sumari, atachaguliwa.

“Hawa watu wa CCM wanamtukana mgombea wetu, wanasema yeye ni gunzi na hilo ni tusi kubwa sana kueleza mgombea huyo gunzi. Ina maana wanawake wa Arumeru wanazaa magunzi badala ya watoto,” alihoji.

Aliongeza, “kuchaguliwa kwa Nassari kutakuwa ishara kuwa Wameru wanazaa watoto na magunzi kama inavyoenezwa na chama tawala.”

Naye Meneja Kampeni wa Chadema, Mchungaji Israel Natse, alilalamikia kitendo kinachodaiwa kufanywa na Meneja Kampeni wa CCM, Mwigulu Nchemba, kusimama jukwaani na kumuita Nassari kuwa ni gunzi.

“Huyu kama Meneja kampeni wa kweli (Nchemba) badala ya kunadi sera ananadi matusi, sisi tunayakataa sana na tunahubiri siasa safi zitakazoleta maendeleo katika Jimbo la Meru,” alisema Mchungaji Natse.

Pia alipinga kile alichokiita kuwa ni propaganda inayofanywa na CCM kupitia kwa Nchemba, kudai kuwa Chadema inajihusisha na ununuzi wa shahada za kupigia kura.

Alisema Chadema ni chama kisichokuwa na uwezo wa kifedha na rasilimali wa kufanya vitendo hivyo viovu, isipokuwa historia inaihukumu CCM kwa kuwa wahusika wakuu.

“Sisi tutanunua shahada wakati hatuna fedha na kila mkutano wafuasi wetu wanatuchangia ili tuweze kununua mafuta ya magari kwa ajili ya kutuwezesha kufika maeneo yote ya Meru, huo ni uongo wa mchana kweupe,” alisema Mchungaji Natse.

Alidai kuwa CCM wamebuni njia mpya baada ya kuona maji yamewafika shingoni na kuamua kununua shahada na kuandika namba za kila kadi na hiyo maana yake wanakwenda kutengeneza daftari hewa la wapiga kura.

Kwa Upande wa mgombea wa Chadema, Joshua Nassari, akijinadi kwa wapiga kura vijiji vya Maloloni, Makiba na kijiji cha Mareu, alilalamikia serikali ya CCM kuleta magari ya maji ya kuwasha, badala ya kuboresha shule ambazo hazina vitabu wala walimu.

“Huu ni wakati wa wananchi kutuma salamu kwa CCM na tutawaonyesha kupitia sanduku la kura kuwa tumewachoka, ” alisema Nassari.

Nassari alisema kuwa kila mwananchi afahamu kuichagua CCM ni kukubaliana na kila aina ya ufisadi unaosababisha watoto kukosa elimu bora na jamii kushindwa kukubaliana na ugumu wa maisha.

“Jimbo letu limekosa Mbunge wa kuwasemea na ndio sababu lilikuwa katika hali mbaya ya miundombinu na kila aina ya ufisadi na mfano upo. Kule Karatu Dk.Slaa alipiga mdomo na serikali ikaleta barabara nzuri na kila kitu, na mimi nitaingia bungeni nikapige mdomo ili watu wasikilize walete maendeleo” alisema Nassari.

Aliongeza kuwa kumchagua Nassari ni kutuma salamu kwa serikali kuwa wana Arumeru wanahitaji maendeleo kwa sababu wamesahaulika.

Wakati huo huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Steven Wassira aliwataka wapiga kura wa jimbo hilo kutoipa kura Chadema kwa sababu chama hicho kinaendesha maandamano badala ya kufanya shughuli za maendeleo.

Wassira alisema hayo wakati akimnadi mgombea kupitia CCM, Sioi Sumari katika kampeni za chama hicho zilizofanyika kwenye vijiji vya kata ya Kikwe.

“CCM ndio chama chenye serikali na chenye nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo,” alisema Wassira ambaye pia ni Mbunge wa Bunda.

Alisema mgombea kupitia CCM, Sioi Sumari ndiye anayefaa kuchaguliwa Mbunge ili atekeleze ahadi zilizowahi kutolewa na mbunge wa jimbo hilo, marehemu Jeremiah Sumari aliyekuwa baba yake mzazi.

Naye Sumari alisema, “serikali ya CCM ina nia ya dhati kabisa ya kuleta maendeleo, nichagueni mimi mwakilishi wa CCM tupunguze kero na kuanzisha miradi ya maendeleo hapa.”

Alisema akipata nafasi hiyo atahakikisha kuwa vijana wanawezeshwa katika miradi ya kiuchumi na hatimaye kupunguza makali ya maisha

Imeandikwa na Cynthia Mwilolezi na Charles Ole Ngereza, Arusha

Chanzo: Nipashe Jumapili

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO