HALI ya amani katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki sasa ni tata kutokana na kuibuka vitendo vya utekaji wafuasi wa vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo.
Chadema ndiyo wamelalamikia kutekwa kwa makada wake wawili, Omar Abdul ambaye hadi jana alikuwa hajulikani alipo wakati kada mwingine, Juma Ally (32) amelazwa hospitali baada ya kutekwa na kunyang’anywa gari, kisha kutupwa mtoni baada ya jaribio la kumuua kushindikana.
Kamanda Andengenye amethibitisha matukio yote mawili ambayo yamekuja kipindi ambacho kimegubikwa na vurugu katika mikutano ya kampeni za CCM na Chadema, huku vijana kadhaa wakiripotiwa kujeruhiwa kwa mapanga na wengine kukamatwa na polisi.
Katika tukio la kwanza, Juma ambaye ni mkazi wa Tengeru, juzi alitekwa na watu asiojulikana akiwa na gari lake, kisha kutaka kumuua. Andengenye alisema tukio hilo lilitokea Machi 27 usiku, wakati watu wanane, walikodi gari la Juma katika eneo la Usar River na kutaka kupelekwa Makumira lakini kabla ya kufika mmoja wao, aliomba kushuka na ghafla watu hao, walianza kumshambulia dereva huyo na kumtupa kwenye korongo.
Alisema wakati watu hao, wakimshambulia, kijana huyo alianza kupiga kelele, ndipo walimvua nguo zote na kuchukua simu na fedha kisha kutoweka na gari hilo aina ya Toyota lenye namba za usajili, T563 BTM.
Andengenye aliongeza kuwa kutokana na sauti aliyokua akitoa Juma, mpita njia mmoja aliisikia na kumulika tochi kwenye Korongo hilo ndipo alimwona na kuita watu wengine kusaidiana kumtoa kisha kumkimbiza Hospitali ya Wilaya ya Arumeru iliyopo Tengeru akiwa uchi huku amejeruhiwa vibaya.
Hadi jana Juma alikuwa bado amelazwa. Akizungumza kwa taabu na waandishi wa habari, alisema watu hao kabla ya kumteka na kumpora gari, walimuomba awapeleke eneo la Makumira.
Katika tukio lingine, Omar maarufu kama Omar Matelephone, ambaye amekuwa akivalia kanzu iliyoshonwa kwa rangi za bendera ya Chadema, kwa siku nne hadi jana, alikuwa hajulikani alipo ikiwa ni siku mbili tangu alipokwaruzana na Makamu Mwenyekiti wa UVCCM, Benno Malisa katika klabu ya ‘Triple A’ baada ya kiongozi huyo wa UVCCM, kumtaka avue mavazi yake ya Chadema.
Tangu Machi 25 Omar alipohudhuria mkutano wa Chadema katika kata ya Songoro, hajaonekana na simu zake zote hazipatikani, pia nyumbani kwake hayupo.
Rafiki wa Omar, Christopha Mbajo alisema jana kuwa yangu walipoachana naye jioni ya Machi 25, hawajamuona hadi jana na simu zake zote hazipatikani.
“Hatujui yuko wapi ila tunakumbuka mara ya mwisho aligombana na Malisa na baadaye waliombana msamaha, kisha aliitwa na Ofisa Usalama wa Taifa Mkoa wa Arusha, Suleiman Mombo na kuhojiwa juu ya ugomvi huo,”alisema Mbajo.
Akizungumza na Mwananchi jana kwa simu, Malisa alikana kumfahamu Abdul na kueleza kuwa hajawahi kugombana naye katika ukumbi wa ‘Triple A’ uliopo jijini Arusha kama inavyodaiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Meneja Kampeni wa Chadema, Vincent Nyerere, alidai vitendo hivyo vinafanywa na kundi la vijana wa CCM walioletwa kutoka nje ya Arumeru na kwamba polisi wanapaswa kulaumiwa kwa kushindwa kuwadhibiti
“Tuliwaambia kuna kundi la vijana linakuja na basi la Manko Express toka Musoma na kwamba wawazuie kwani ni vijana wa vurugu, tukawapa na majina yao lakini wameshindwa kuwadhibiti na sasa wanatishia maisha ya watu!”Alilalamika Nyerere.
Published by: Mwananchi Habari – yesterday, Machi 30 2012
0 maoni:
Post a Comment