Mahakama ya kimataifa ya jinai ICC iliyoko the Hague, imempata na hatia ya uhalifu wa kivita mbabe wa zamani wa kivita katika Jamuhuri Ya Kidemokrasia ya Congo Thomas Lubanga (pichani).
Hukumu hiyo ndiyo ya kwanza kutolewa na mahakama ya ICC tangu kubuniwa kwake zaidi ya muongo mmoja uliopita. Hata hivyo mahakama itaamua baadaye hii leo adhabu atakayopata Lubanga.
Lubanga alipatikana na hatia ya kuwasajili watoto walio chini ya umri wa miaka kumi na mitano kama wanajeshi wake wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kaskazini mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya congo.
Lubanga pia alisemekana kuwa kiongozi wa kundi la waasi wakati wa makabiliano ya kikabila katika eneo lenya utajiri wa dhahabu nchini humo.
Upande wa mashtaka ulimtuhumu Lubanga kwa kutumia watoto kama watumwa wa ngono, walinzi wake na wapiganaji wake.
Katika uamuzi uliopitishwa kwa kauli moja, majaji watatu waliokuwa wanasikiliza kesi dhidi ya Lubanga, walisema kuwa ushahidi dhidi ya Lubanga ulithibitisha kuwa kundi la waasi lilioongozwa na Lubanga pia linapaswa kuwajibishwa kwa makosa ya kusajili watoto kama wapiganaji waliopigana kwenye msityari wa mbele.
Lubanga, aliyekamatwa mwaka 2005, huenda akahukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kuwa mahakama hiyo haiwezi kupitisha hukumu ya kunyongwa.
Chanzo: BBC Swahili
0 maoni:
Post a Comment