Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

Dk Kitine, Butiku na Kaduma Wakitabiria kifo CCM

WASEMA WANAMTANDAO NI CHANZO CHA UFISADI

Na Elias Msuya, Mwananchi Habari – Machi 26, 2012
MAKADA watatu wakongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ibrahim Kaduma, Dk Hassy Kitine na Joseph Butiku, wameibuka na kukitabiri anguko chama hicho tawala kwa kile walichosema, kwenda kinyume na misingi ya kuasisiwa kwake.

Kauli za makada hao maarufu, zinakuja kipindi ambacho upepo wa kisiasa umekuwa ukivuma vibaya ndani ya chama hicho kikongwe nchini na barani Afrika, kutokana na vita ya makundi kati ya watuhumiwa wa ufisadi na wale wanaojipambanua kwamba ni wazalendo na wapinga ufisadi.
Wakizungumza juzi usiku katika kipindi cha "Je, tutafika?" Kilichorushwa na kituo cha luninga cha Channel ten, makada hao walitoa kauli hizo nzito huku wakishambulia kundi la wanamtandao ndani ya chama hicho, vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi na vitendo vya ufisadi vinavyolitikisa taifa.

Kaduma
Ibrahim Kaduna Kaduma ambaye aliwahi kuwa Waziri katika Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Mwalimu Julius Nyerere, alisema hali ndani ya CCM sasa ni mbaya na imefika hapo kwa sababu ya kuacha misingi ya TANU iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere.

“Kwa hali ilivyo, CCM kinaweza kusambaratika wakati wowote. Sisi tuliingia kwenye TANU kutokana na misingi ambayo Mwalimu Nyerere aliiweka,” alionya Kaduma.

Kaduma aliitaja misingi hiyo kuwa ni pamoja na imani kuwa binadamu wote ni ndugu, kuwatumikia watu kwa moyo wote, kujitolea nafsi kuondoa umasikini ujinga na maradhi, rushwa ni adui wa haki hivyo ni kosa kutoa au kupokea rushwa, kutotumia cheo cha umma  kwa maslahi binafsi, kusema kweli daima na kuacha fitina, kujielimisha kadiri ya uwezo na kutumia elimu hiyo kwa manufaa ya umma.

Alisisitiza, “Mwalimu hakuwa akiongea nadharia, ndiyo maana mwaka 1955 aliacha kazi aliyokuwa nayo ya ualimu iliyokuwa na mshahara mzuri na kwenda kuimarisha chama cha TANU ilikuwa ni ku-risk (kujiweka kwenye hatari).’’

Dk Kitine
000001dkkitibe Dk Kitine akizungumzia barua zilizowahi kuandikwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku kwa wenyeviti wa CCM (Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete), na kutojibiwa na viongozi hao, alisema hata angekuwa yeye asingezijibu kwa sababu ndiyo mfumo wa chama hicho kutotatua na kuficha matatizo.

“Barua ya Butiku kwenda kwa Mwenyekiti wa zamani na wa sasa haikujibiwa..., hata ningekuwa mimi nimeandikiwa barua na mambo ninayofanya ni wazi, nisingeijibu. Mimi siwalaumu. Hiyo ni moja ya matatizo na utamaduni wa chama tawala kutokuwa na utamaduni wa kutatua matatizo,” alisema Dk Kitine.

Akizungumzia chanzo cha kuporomoka kwa maadili ndani ya CCM, Dk Kitine ambaye pia aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa, alisema  yalitokana na kuanzishwa kwa makundi na mitandao ya kusaka madaraka kwenye chama.

“Mitandao na makundi ndani ya CCM, hakikuandikishwa mahali popote. Mtandao ulianzishwa mwaka 1995 na ulikuwa wa vijana. Mwaka huo mtandao huo ulifanya mgomo mbele ya Mwenyekiti Ali Hassan Mwinyi na mbele ya Mwalimu Nyerere wakati huo tunatafuta viongozi,” alisema Dk Kitine na kuongeza:

“Wakati Mzee Mwinyi anatuongoza kama mwenyekiti na amekuja kutueleza maazimio ya Kamati Kuu kwamba kwanini baadhi ya wagombea hawakuwa na sifa, wanamtandao wakasema jambo hilo halikubaliki.”

Aliongeza kwamba, mtandao huo ndiyo umekuwa chanzo cha ufisadi ndani ya chama na kufafanua; “Kundi hilo ndilo sasa linaendesha rushwa, linafanya wanachama wa CCM kuwa hawana maana, linakusanya kadi. Kama wanabisha waje kwenye kikao kama hiki wajieleze.”

Dk Kitine alitaja kashfa za ufisadi zilizovuma kuwa ni pamoja na Deep Green, Kagoda, Meremeta, EPA na kubainisha kwamba zote zina mkono wa kundi hilo la mtandao.

“Lakini yote yanatokana na kuficha matatizo, kwa mfano unapowakataza watu kujadili suala la Muungano, unaficha nini? Sasa haya ya kuficha pia masuala ya Kagoda na mengineyo, ipo siku watu watataka majibu yao tu hata miaka 100 ijayo. Matokeo yake watakichukia chama,” alisema.


Kauli ya Butiku
butiku Katika mjadala huo, Butiku ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya  Mwalimu Nyerere, alisema CCM kimebadilika kutoka kuwa chama cha wakulima na wafanyakazi na kuwa chama cha wafanyabiashara na  maslahi binafsi.

“Mnapofanya kazi katika Serikali au chama, wajibu wenu siyo kukiua chama mlichokianzisha kama ni chama chochote au CCM kinachojiita kuwa chama cha wakulima na wafanyakazi. Kwa bahati mbaya sana wafanyabiashara wengi waliojiingiza katika Chama Cha Mapinduzi, wamegeuka, kazi yao na madhumuni ndiyo yamekuwa malengo mbadala ya chama,” alisema Butiku na kuongeza:

“Mimi naamini biashara ni kazi, lakini kama unachukua malengo ya biashara na kuyafanya kuwa malengo mbadala ya Chama Cha Mapinduzi, chama hicho bado kipo?,” Alihoji.

Butiku ambaye aliwahi kuwaandikia barua Mwenyekiti mstaafu wa CCM Mkapa na Mwenyekiti wa sasa Rais Kikwete akitoa angalizo kuhusu mweleko wa chama hicho, alisema hali ya sasa chama ni mbaya.

“Kwa hiyo wakati ule nilisema chama kimeanza safari ya kifo. Leo ukitazama, ukisikiliza viongozi wanavyosema, ukisiliza matendo yao, uwepo wao wote ni wa kibiashara na si kuimarisha chama hicho, ni kuimarisha malengo yao ya kibiashara na kibinafsi,” alisema Butiku.

Aliongeza kuwa chama hicho kimepoteza maadili kiasi kwamba imekuwa kawaida kwa viongozi kununua kura na kwamba siku hizi, uongozi wa chama unanunuliwa.

"Nani anabisha kwamba CCM hatununui uongozi? CCM viongozi wote wa ngazi mbalimbali, mmoja mmoja anieleze kama siyo kweli kwamba CCM kimekuwa chama cha kukumbatia rushwa na kununua uongozi?,” Alihoji na kuongeza:

“Chama kimefikia wakati mtu anaweza kununua kadi 1,000 na kuweka kwenye mkoba wake wakati ndugu Kitine anazo 200, wewe ndiyo mshindi. Mkisha vunja maadili kwa kiwango hicho, bado mpo?”

Hata hivyo, alisema Katiba ya CCM bado inajieleza vizuri na kwamba hiyo ndiyo inamfanya aendelee kuwa mwanachama wa chama hicho japo viongozi wake hawaifuati.

“Katiba inasema chama hiki ni cha wakulima na wafanyakazi, waliokubali madhumuni hayo. Kama hatutaki basi tukibadili, lakini hatuwezi kukibadili kinyemela. Siku hizi naambiwa ukisikika unakikosoa chama, sauti hizo zimekuwa za watu wa Nyerere, hivi katika nchi hii nani asiyekuwa wa Nyerere? Alihoji Butiku.

CCM imetimiza miaka 35 tangu kuasisiwa kwake kwa kuunganishwa vyama vya ASP na TANU mnamo Februari 5, mwaka 1977 lakini, chama hicho katika siku za karibuni kimeshuhudia ukosoaji mkubwa kutoka kwa makada wake wenye mrengo tofauti na mwenendo wa chama hicho kwa sasa, kutokana na kile wanachosema ni chama kukiuka misingi ya waasisi.

Nape
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Nape Nnauye alipotakiwa kuzungumzia hoja za makada hao alijibu kwa kifupi," No comment." (sina cha kusema)

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO