Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

CCM Wabadili Siku Ya Uzinduzi Wa Kampeni Zao Arumeru Mashariki.

Chanzo: Mwananchi

AWALI ratiba ilikuwa ikionyesha kwamba CCM ilipaswa kuzindua kampeni zake leo, baadae ikaelezwa kuwa uzinduzi ungefanyika siku moja na CHADEMA, siku ya Jumamosi Machi 10, lakini ghafla ratiba hiyo ikabadilishwa na sasa uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika, Jumatatu Machi 12.

Habari za uhakika kutoka ndani ya chama hicho zilisema mabadiliko ya ratiba ya uzinduzi wa kampeni za CCM, yanatokana na sharti la Mkapa ambaye ametaka kwanza makundi ambayo yalitofautiana kutokana na kura za maoni yakutanishwe ili kuondoa tofauti zao.

Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu wa awamu wa tatu, ambaye anatarajiwa kuzindua kampeni za Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki, anadaiwa kutoa sharti la kumalizwa kwanza kwa tofauti za kimakundi ndani ya chama hicho, kabla ya yeye kufanya uzinduzi wa kampeni za uchaguzi huo.

Mkapa alipendekezwa na Kamati Kuu ya Halmashauri kuu (CC) ya CCM kuzindua kampeni hizo, katika kikao chake cha Machi mosi ambacho pia kilifanya uteuzi wa mwisho wa mgombea ubunge wa jimbo hilo ambaye ni Siyoi Sumari baada ya kufanyika duru ya pili ya kura za maoni kati ya mgombea huyo na aliyekuwa mpinzani wake, William Sarakikya.

Mpasuko ndani ya Chama Cha Mapinduzi katika kura za maoni jimboni Arumeru Mashariki, ni zao la msuguano wa makundi ya urais ndani ya chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015 ambayo kila moja lilitaka kumweka mgombea wake.

Hata hivyo, Mkuu wa Kitengo cha Uchaguzi wa CCM Makao makuu, Matson Chizi, licha ya kukiri kampeni za CCM zitazinduliwa Machi 12 lakini, hakuwa tayari jana kueleza kama Rais mstaafu Mkapa atahudhuria au la.

Chizzi pia alizungumzia tuhuma kwamba wapo watu wanaonunua shahada za kupigia kura na kusema kuwa chama hicho kinapinga utaratibu huo, bila kujali anayenunua ni wa chama gani.

Chizzi alisema kununua shahada ni kutaka kupora haki ya mtu kupiga kura hivyo tayari wametoa taarifa kwa msimamizi wa uchaguzi na polisi kushughulikia suala hilo.

Mkuu huyo wa Kitengo cha uchaguzi akizungumzia makundi yaliyotokana na kura za maoni, alisema kwa sasa yamekwisha na wanaCCM wote wameungana kukihakikisha chama hicho kinapata ushindi.

Mapema wiki hii, Meneja wa Kampeni wa CCM, Mwigulu Nchemba ambaye pia ni Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM, alisema chama hicho kinajipanga kukutanisha waliokuwa wagombea wa kura za maoni na wapambe wao.

Meneja huyo, ambaye yuko jijini Arusha kwa takriban wiki moja sasa, amekuwa pia akikutana na mabalozi na viongozi wa chama hicho katika jimbo la Arumeru Mashariki.

Wakati huohuo, inaelezwa kuwa CHADEMA watazindua kampeni zao kesho Jumamosi Machi 10 eneo la Usa River na zitarushwa live kupitia Star Tv. Baadhi ya viongozi wa hicho akiwemo Mwenyekiti wake, Mh Mbowe, wabunge mbalimbali pamoja na madiwani wawakilishi wa maeneo tofauti ya nchi watakuwepo siku ya uzinduzi! Mwenyekiti wa CHADEMA alitangaza chama hicho kufanya kampeni za kistaarabu kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa kampeni.
Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO