JK: Nilisaini Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Kuepuka Hasira za Wabunge wa CCM
RAIS Jakaya Kikwete amesema alisaini Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kukwepa hasira za wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Rais Kikwete alitoboa siri hiyo katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi Februari aliyoitoa juzi kupitia vyombo vya habari.Uamuzi huo wa Rais kutia saini muswada huo ambao tayari ulikuwa umepingwa kila kona ya nchi licha ya kupitishwa na Bunge, ulizidi kuibua hasira za makundi mbalimbali ya kijamii.
Rais wakati akisaini muswada huo, Novemba mwaka jana, alikuwa ameanza mazungumzo na makundi ya kijamii ukiwamo ujumbe wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Lakini, mwenyewe akifafanua ni kwa nini alisaini muswada huo wakati ulikua ukipingwa na wananchi na huku akiwa katika mazungumzo na wadau, ndipo alisema, “Kitendo cha mimi kukataa kutia sahihi kingejenga chuki kwa upande wa wabunge walio wengi ambao waliujadili muswada huo na kuupitisha. Wangeweza kuhisi wamedharauliwa na kuonekana hawana thamani.”
Rais Kikwete alisema vyama vya siasa na asasi za kiraia waliomba asitie saini na badala yake aliagize Bunge liujadili tena muswada huo.
“Sikutaka kuliingiza taifa letu katika mgogoro mkubwa wa kisiasa na kikatiba usiokuwa wa lazima unaoweza kuepukwa kwa kutumia njia nyingine za kisheria na kikatiba,” alisema Kikwete.
Alisema, alipofanya mazungumzo na vikundi hivyo vya kiraia, aliwaeleza kuhusu ugumu huo wa kuacha kutia saini na kuurudisha bungeni kujadiliwa upya.
Soma habari hii zaidi kupitia Gazeti Mwananchi
0 maoni:
Post a Comment