MENEJA WA REDIO YA MTOTO WA LOWASSA ATIWA MBARONI NA TAKUKURU KWA TUHUMA ZA RUSHWA KURA ZA MAONI ARUMERU
SIKU moja baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani hapa kumkamata mfanyabiashara maarufu wa madini, Thomas Mollel 'Askofu’ kwa tuhuma za kutoa rushwa kwa madiwani wakati wa kura za maoni ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki, taasisi hiyo imezidi kutoa meno kwa kumnasa pia Meneja wa Kituo cha Radio 5 cha mjini Arusha.
Meneja huyo, Jimmy Mtemu, ingawa si mwanasiasa, naye amekamatwa akihusishwa na matukio ya rushwa wakati wa kura hizo zilizopigwa juzi na kumpa Siyoi Sumari ushindi wa kura 761 dhidi ya William Sarakikya (361) walioingia katika mzunguko wa pili wa kumpata mgombea wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM.
Kukamatwa kwa Mtemu kulithibitishwa jana na Kamanda wa Takukuru wa Mkoa wa Arusha, Mbengwa Kasomambuto.
Alisema hayo baada ya kuulizwa juu ya taarifa za kukamatwa kwa Meneja huyo, na kukiri, lakini akasema si lazima kila kinachofanywa kitangazwe wakati huo huo.
Alisema: “Kuna watu tuliwakamata jana katika mkutano wa kupiga kura za maoni na mwingine leo na hata huyo (Mtemu) naye tumemkamata, lakini kwa sasa fanya subira muda ukifika tutaweka mambo hadharani.”
Vyanzo vya habari hizi vinasema kukamatwa kwa Meneja huyo kulitokana na kushindwa kutoa ushirikiano kwa maofisa wa Takukuru waliokuwa wanamtafuta mfanyakazi wa kituo hicho aliyetambuliwa kwa jina la Pili Sirikwa.
Kamatakamata hiyo sasa inafanya idadi ya waliokamatwa kwa taasisi hiyo kufikia sita, wanne wakitambuliwa kwa majina huku wengine wakiendelea kuwa siri.
Kamanda Kasomambuto alitaja wengine waliokamatwa kuwa ni ‘Askofu’ ambaye pia ni Diwani wa Mbuguni, Arumeru na Elirehema Kaaya ambaye aligombea katika mzunguko wa kwanza lakini akashindwa kwa kupata kura 205. Mwingine ni Ezekiel Mollel, ambaye ni Katibu wa Jumuiya ya Vijana ya CCM Wilaya ya Monduli.
“Wote tunawashikilia na wako kwa uchunguzi zaidi na ukikamilika, wote watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya rushwa,” alisema Kamanda huyo.
Pia Takukuru inashikilia pikipiki mbili zilizokutwa eneo hilo; moja ikidaiwa kuwa ya Katibu Hamasa wa UVCCM Arumeru, John Nyiti.
Source: HabariLeo
N.O.I.S.E.O.F.S.I.L.E.N.C.E
0 maoni:
Post a Comment