MGOMO wa madaktari jana ulianza katika baadhi ya hospitali za wilaya mkoani Dar es Salaam na Hospitali ya Rufaa Bugando, huku katika mikoa mingine hali ikiwa shwari na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili huduma zikitolewa kwa kusuasua.
Hata hivyo, madaktari wamedai mgomo huo utaendelea nchi nzima hadi Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda na Naibu wake, Dk. Lucy Nkya watakapojiuzulu.
Utafiti uliofanywa na gazeti hili Muhimbili, Amana, Temeke na Mwananyamala, ulionesha katika baadhi ya hospitali wagonjwa walitakiwa kusikiliza vyombo vya habari kisha warejee watakaposikia kuwa mgomo umekwisha.
Amana, Katibu wa Madaktari wa Hospitali hiyo, Dk. Shani Mwaluka, alithibitisha kuwapo kwa mgomo na kusema hali ni mbaya, kwani wamegoma madaktari wengi walioajiriwa na walioko katika mafunzo kwa vitendo.
Alisema wameamua kuwarudisha nyumbani wagonjwa ambao hawako katika hali mbaya na madaktari waliobaki wanawahudumia walio katika hali mbaya zaidi.
“Mgomo huu ni tofauti na wa awali kwani sasa wamegoma madaktari wengi hata wale walioajiriwa, kwani asubuhi walifika na kusaini lakini wakaondoka,” alisema.
Alisisitiza kuwa wanaendelea kujipanga kuhakikisha huduma zinaendelea kwa waliopo kwa madhumuni ya kuhudumia walio katika hali mbaya zaidi.
Katika hospitali hiyo, wagonjwa walikuwa wakifika katika dirisha la Mapokezi na kuelezwa kuwa madaktari wamegoma, hivyo waende katika vituo vya afya vingine vilivyo karibu na kwao.
Temeke, wagonjwa walitakiwa kurudi majumbani hadi watakaposikia kwenye vyombo vya habari kuwa mgomo umemalizika.
Mmoja wa wauguzi katika hospitali hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema ni historia katika hospitali hiyo, kwani haijawahi kuwa na mgomo lakini huo ulioanza jana walishangaa kutoona madaktari.
Muhimbili Muhimbili, hali ilikuwa ya kusuasua kwa baadhi ya sehemu kutoa huduma huku wengi wa wagonjwa wakiandikiwa tarehe za kurudi kuona madakatri bila kuhudumiwa. Neema Silayo, mmoja wa wagonjwa alisema alitakiwa kuonana na daktari wake kwani husumbuliwa na mguu, lakini alipangiwa Machi 19 arudi.
Alielezwa kuwa madaktari ni wachache kutokana na wengi wao kuwa kwenye mkutano hivyo mpaka tarehe hiyo watakuwa wamerejea. Katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa ya Muhimbili (MOI) wagonjwa wengi walionekana wakisubiri matibabu bila mafanikio huku baadhi yao wakilalamika kufika tangu saa moja asubuhi hadi mchana bila kuona daktari.
Lakini baadaye, Ofisa Uhusiano wa MOI, Almas Jumaa, alisema hakukuwa na mgomo kutokana na wote wenye kliniki kuonwa na madaktari. Alisema msongamano huo wa wagonjwa unatokana na baadhi ya madaktari kuomba ruhusa ya kuhudhuria kikao cha madaktari, jambo lililosababisha wengine kupangiwa tarehe za kurudi ili waliopo wahudumie wagonjwa wa dharura.
Ocean Road, huduma ziliendelea kama kawaida kwani kati ya madaktari 11 waliopo wawili ndio hawakuripoti bila taarifa. Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa Ocean Road, Ester Kazenga alisema wanafuatilia madaktari hao kujua sababu za kutofika kazini lakini hakuna mgomo katika hospitali hiyo.
Chanzo: HabariLeo
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 maoni:
Post a Comment