Tunakusogezea karibu habari na matukio, zaidi habari za kisiasa na utawala, matukio ya Arusha na maeneo jirani, bila kusahau na mambo mengineyo ya kitaifa yanayojiri katika maeneo mbalimbali ya nchi kuhusu maendeleo na kuwa ya maslahi kwa watu wengi. Burudani na michezo pia havijasahaulika. Kizuri zaidi, unaweza kupata link ya Blogu nyingine na website muhimu hapa hapa kwa kuscroll mpaka chini. Karibu tuhabarike!

LEMA AREJEA KIVINGINE ARUSHA, ATANGAZA MKAKATI MPYA WA KUMPINGA MEYA

BAADA ya kuwa nje ya Bunge kwa takriban miezi tisa baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kumvua ubunge Aprili 4 mwaka jana, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), ameingia ofisini kwake rasmi huku akiwa na mikakati mipya ya kuendelea kumpinga meya wa jiji hilo, Gaudence Lyimo.

Lema ambaye alirejeshewa ubunge wake na Mahakama ya Rufaa Tanzania Desemba 22, mwaka jana, amewataka pia Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongela, na Mkuu wa Mkoa huo, Magessa Mulongo, kuacha kutoa matamko ya kisiasa yenye kulenga kukipiga vita chama chake cha CHADEMA.

Alisema kuwa badala yake wajikite kwenye kusimamia shughuli za maendeleo ya wananchi kama Katiba ya nchi inavyowaelekeza na waelewe kuwa wabunge na madiwani toka vyama vyote wana hadhi sawa kwani ni wawakilishi wa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Lema aliahidi kuendelea kupinga unyanyasaji unaofanywa kwa wafanyabiashara wadogo maarufu kama Wamachinga ambao alidai kuwa idadi yao imekuwa ikiongezeka kila kukicha.

Alisema kuwa hali hiyo imetokana na serikali kushindwa kuzalisha ajira kupitia viwanda na mashamba huku ikishindwa kutoa elimu ya ujasiriamali hatua aliyodai inaongeza idadi ya Machinga hao ambao wanatafuta fedha za kujikimu.

Lema ambaye alisindikizwa na kundi kubwa la wananchi wa jiji la Arusha wakiwemo viongozi mbalimbali na madiwani wa CHADEMA toka halmashauri hiyo, aliweka bayana kuwa msimamo wake wa kuendelea kutomtambua Meya Lyimo bado uko palepale.

Alifafanua kuwa sasa amekuja na staili mpya ya kumpinga kwa hoja kwenye vikao anavyoviongoza badala ya kutoka nje kama walivyokuwa wakifanya na madiwani wake.

“Nitashiriki kwenye vikao vya halmashauri endapo kikao cha kamati kuu ya CHADEMA kitakachokaa mwezi huu kitaturuhusu mimi na madiwani wenzangu. Ingawa tuko wachache baada ya kuwatimua wengine lakini tunataka ufanyike uchaguzi halali wa Meya,” alisema.

Alisema kuwa yuko tayari kushirikiana na viongozi wote wa serikali wilaya na mkoa isipokuwa hataki kuona uonevu kwa kina mama wauza mboga sokoni wakipigwa viboko na mgambo ukiendelea.

Lema aliongeza kuwa neno ‘Machinga’ limekuwa likitumika kuwanyanyasa wafanyabiashara wadogo ambao wengi ni chini ya umri wa miaka 18 ambao alidai wanatokana na kushindwa kuendelea na elimu ya sekondari.

Aliwataka viongozi hao wa mkoa kumshauri Rais Jakaya Kikwete kufuta hati ya kiwanja kilichokuwa eneo la wazi la Kilombero lililouzwa kifisadi na kulirudisha kwa wananchi ili liweze kutumika na Machinga hao.

Katika hatua nyingine, Lema aliitaka Tume ya Uchaguzi (NEC) kutangaza uchaguzi mdogo kwa kata tano za Kimandolu, Sombetini, Themi, Erelai na Kaloleni ambazo zimekuwa wazi kwa kipindi kirefu baada ya madiwani wake kuvuliwa uanachama na CHADEMA na yule wa Sombetini kujitoa CCM.

Alisema kuwa CHADEMA itaadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja ya vifo vya watu watatu walioaga dunia wakati wa maandamano yao ya Januari 5 , 2011 kwa kufanya mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Ngarenaro.

Source: Tanzania Daima

Washirikishe Google Plus

About SeriaJr

SeriaJr will keep you updated with all current political news countrywide "Ndiye "Bosi" Mzito Arusha255" Karibu Tuhabarike!.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 maoni:

TANZANIA, THE HOME OF KILIMANJARO